Watu zaidi ya 400 wakiwamo madereva wamepatiwa huduma ya upimaji macho katika maadhimisho ya wiki ya ugonjwa wa presha ya macho katika kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Zoezi hilo la siku sita kuanzia Machi 10 hadi 16, pia linahusisha baadhi ya wananchi waliofika kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli Mbezi Luis kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 9 alasiri kati ya Machi 12 hadi 18.
Huduma hiyo inatolewa na hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na Hospitali ya Polisi Kilwa Road ambapo wanatoa ushauri bila malipo kwa madereva wa mabasi yaendayo mikoani kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli.
Upimaji wa afya ya macho, pia utaambatana na upimaji wa bure wa magonjwa mbalimbali ya figo, presha, sukari na uchangiaji damu.
Daktari wa macho, Erick Raphael kutoka Hospitali ya Polisi Barrack Kilwa Road, akimhudumia mmoja wa wananchi waliofika kupata huduma katika kituo kikuu cha mabasi Magufuli Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Ugonjwa wa presha ya macho unatajwa na wataalamu wa afya ya macho duniani kuwa wa kwanza kusababisha upofu usiotibika na hutokea pale mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano kwenye ubongo unaposhambuliwa kutokana na presha kali.
Daktari bingwa wa magonjwa ya macho katika hospitali ya CCBRT, Dk Katuta Ramadhani, amesema dalili za kwanza ni kupoteza uwezo wa kuona na hiyo ni hatua za juu.
“Baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata dalili kama kuona rangi za upinde wa mvua anapoangalia taa, kupoteza uoni kabisa, uoni hafifu, kupungua uwezo wa kuona kwa pembeni, na maumivu ya kichwa,” amesema.
Dk Katuta ambaye pia ni mkuu wa idara ya macho hospitalini hapo, amesema watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo, kama ilivyo kwa wale ambao wazazi wao au ndugu zao wa kuzaliwa wamewahi kuwa na ugonjwa wa presha ya macho.
“Mara nyingi tunapokea wagonjwa wakati ugonjwa umeshakuwa mkubwa, wakati mwingine bila hata wao kujua. Nawahimiza Watanzania wenzangu tujenge utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya ya macho yetu mara kwa mara hii, itapunguza athari kubwa zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huu,” amesema.
Amesema CCBRT kuna kliniki maalumu ya presha ya macho mara tatu kwa wiki na katika kila kliniki wanapokea wagonjwa wa presha ya macho kati ya 40 hadi 45 na wengine hujitokeza siku zisizo za kiliniki wakihitaji kuonana na daktari wa macho kwa shida hiyo.
Dk. Katuta amesema mtu anaweza kujikinga na ugonjwa huo kwa kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya ya macho mara kwa mara pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya dawa za macho kadri inavyoshauriwa na daktari.
“Utaratibu wa upimaji macho ni kila baada ya miaka miwili ikiwa una umri wa miaka 40, kwa wale wenye umri wa miaka zaidi ya miaka 40 hadi 64 wafanye uchunguzi wa macho kila mwaka, na umri zaidi ya miaka 64 wafanye hivyo kila baada ya miezi sita,” amesema.
Amesema presha ya macho hutibiwa kwa vidonge vya kumeza, dawa ya matone kudondoshea kwenye macho, upasuaji, matibabu kwa njia ya kipandikizi na mionzi.