Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

40,000 huugua saratani kila mwaka nchini

#LIVE: Ummy Mwalimu Anasoma Muswada Wa Bima Ya Afya Kwa Wote Bungeni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kati ya asilimia 28 na 30 ya wagonjwa wa saratani ndio wanaofika kwenye vituo vya, huku 40,000 wakikadiriwa kuugua ugonjwa huo kila mwaka.

Mwalimu ameyasema hayo jana Ijumaa Aprili 5, 2024 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo aliyehoji kama Serikali inaona umuhimu wa kupeleka huduma ya mionzi katika Hospitali ya Kanda ya Kusini.

“Wagonjwa wengi wa saratani wanaenda hospitali wakati hali imekuwa mbaya, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha iwafikie wanawake wengi ambao wako vijijini ili waweze kutibiwa magonjwa haya kwa wakati," ameuliza Malapo

Akijibu swali hilo Waziri Ummy amesema inakadiriwa kila mwaka nchini kuna wagonjwa wapya wa saratani 40,000 lakini wanaofika kupata huduma ni kati ya asilimia 28 hadi 30.

Kutokana na takwimu hizo, amesema suala la kutoa elimu kwa Watanzania ni la msingi.

“Asilimia 70 wanafika wakati saratani ikiwa katika hatua ya tatu au ya nne ambayo ni ngumu kutibu au matibabu kutumia muda mrefu, hivyo tunahitaji elimu kwa wananchi ya kuwakumbusha kupima saratani kwa sababu inatibika ikigundulika mapema," amesema.

Pia amesema Serikali ina mpango wa kujenga huduma za saratani kwa njia ya mionzi kwenye hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara kwa mwaka 2025/26 na kwa sasa wanakamilisha katika hospitali ya kanda ya nyanda za juu kusini na ile ya KCMC.

Katika swali la msingi, Tunza ametaka kujua ni hospitali ngapi zinatoa huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani hapa nchini.

Akijibu swali hilo, Ummy amesema kwa sasa Serikali ina jumla ya vituo vinne ambavyo vinatoa huduma ya matibabu ya saratani nchini kwa njia ya mionzi ambavyo ni Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Kanda Bugando, Hospitali ya binafsi Besta na Hospitali ya Good Sammaritan (St. Fransis Ifakara).

Amesema Serikali inaendelea na taratibu za uwekezaji kwa kuongeza vituo vingine vitatu (Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC na Hospitali ya Kanda Mbeya) kwa Tanzania Bara na kimoja kwa Visiwani Zanzibar katika Hospitali ya Binguni, kwa kujenga majengo na kuviwezesha vifaa vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa saratani kwa njia ya mionzi.

Chanzo: Mwananchi