Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

38 wajitokeza kujenga viwanda vya dawa nchini

5782 TIC TZW

Thu, 5 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

WAWEKEZAJI 38 wamejitokeza papo kwa hapo na kuahidi kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni moja ya hatua ya utekelezwaji wa kufi kia uchumi wa viwanda.

Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimetakiwa kuwasaidia wawekezaji, kuhakikisha wanafanikisha malengo yao, kwa kuwa yapo maeneo ambayo uwekezaji wake vifaa vyake vina msamaha wa kodi. Kadhalika, serikali imesema inatarajia kupeleka muswada bungeni mwaka huu, utakaoweka bayana kuwa bima ya afya ni lazima kwa kila Mtanzania. Hata hivyo, Watanzania waishio nchini Marekani wameeleza masikitiko yao ya kukosa uraia pacha, ambao ungewezesha kuunga mkono jitihada za serikali za kufikia uchumi wa viwanda, na kwamba wanao uwezo wa kuwa na mtaji unaoanzia dola milioni tano hadi 100 na kuwekeza katika vifaa tiba.

Hayo yalibainika jana Dar es Salaam katika kongamano la wawekezaji wenye nia ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa nchini, ambapo mawaziri wawili kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage waliongoza uhamasishaji. Wawekezaji katika sekta hiyo ya dawa na vifaa tiba, wakiwemo wataalamu walijitokeza kwa wingi kuitika mwito wa uanzishwaji wa viwanda vya dawa nchini, ambavyo vitasaidia kuongeza ajira, lakini pia kuboresha huduma za afya na kupunguza gharama za kuagiza dawa kutoka nje ya nchi. Kuhusu uwekezaji, Waziri Ummy alisema ni asilimia sita pekee ya dawa, ndiyo inayopatikana nchini, huku nyingine ikitegemea kutoka nje ya nchi.

Alisema changamoto kubwa ni katika fedha za dawa, ambayo ni lazima kubadilishwa na kuwa katika mfumo wa dola ya Marekani, ambapo badala ya kiwango kilekile kutumika hupungua huku pia uagizwaji wa dawa ukichukua miezi sita hadi tisa bila ya kufika nchini. Alisema hali hiyo husababisha serikali kununua dawa nyingi ikiwemo za miezi tisa ambazo zinaweza kukaa muda mrefu, hivyo kujikuta wakilipia gharama kubwa huku uhifadhi wake ukiwa na changamoto zinazoweza kusababisha dawa nyingine kuharibika, ikiwa ni karibu Sh bilioni 4.

Alisema ni vyema wawekezaji kufahamu kuwa lipo soko katika kuwekeza katika sekta hiyo, ambapo idadi ya watanzania kwa sasa inafikia milioni 55 na kiwango cha kukua kwa uzalishaji ni asilimia 5.2, ikiwa na maana kuwa watoto watano huzaliwa na kila mwanamke wa Kitanzania. Alisema katika Sh bilioni 269 za dawa zitokanazo na bajeti, pia zipo Sh bilioni 500 kutoka katika Mfuko wa Wafadhili kwa mwaka.

Kiwango kingine hutoka katika mfuko wa pamoja wa afya, ambazo zote kwa pamoja huingizwa katika kuboresha huduma za afya nchini. Ummy alisema uwekezaji wa waliojitokeza, utakuwa ni wenye manufaa na kusaidia kuboresha huduma za afya nchini. Kwa upande wake, Waziri Mwijage alisema lengo la uwekezaji katika sekta hiyo ni utengenezwaji wa sekta binafsi imara ya Tanzania. Kwamba serikali itatoa wataalamu watakaowaeleza taratibu nzima za uwekezaji nchini ili ifikapo 2025 dawa zitengenezwe nchini. Alisema wizara hiyo ina maeneo mbalimbali kila mkoa, mfano ina eneo la viwanda Kibaha mkoani Pwani ekari 40, Bagamoyo ekari 461 na Kurasini jijini Dar es Salaam ekari 62.

Mwijage alisema hadi sasa viwanda vilivyopo nchini idadi yake inafikia 13, vitano kati yake vikiwa ndio vinavyofanya kazi na viwili havifanya vizuri. Aliviagiza kuanza mara moja uzalishaji, kwa kuwa serikali ina mkono wake. Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe alisema kituo hicho ni muhimu kwa kusaidia wawekezaji, kuwapunguzia gharama za awali za uwekezaji wao.

Alisema katika eneo la famasia, vifaa vinavyoingizwa nchini vimesamehewa kodi mbalimbali ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika vifaa kama mashine na usimikwaji wa mitambo kwa ajili ya eneo hilo. Magari yatakayohusika katika uwekezaji katika viwanda vya eneo hilo, yamesamehewa kodi kwa asilimia 75. Aliwataka wawekezaji hao, kufahamu kuwa ili kuandikisha mradi TIC kwa mwekezaji wa ndani, lazima awe na mtaji zaidi ya dola 100,000 na kwa mwekezaji wa nje kuanzia dola za Marekani 500,000.

Chanzo: habarileo.co.tz