Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

204 wafanyiwa upimaji wa moyo

1c90e5315d12be36270f1f3d38df2bec.jpeg 204 wafanyiwa upimaji wa moyo

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI 204 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo katika maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoanii Dar es Salaam, Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Samwel Rweyemamu, alisema upimaji uliofanyika ni wa kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, umeme wa moyo, urefu, uzito, shinikizo la damu na kiwango cha sukari mwilini.

Upimaji huo wa siku moja ulifanywa na wataalamu wa JKCI, kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo na upimaji ulifanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo eneo la Luguluni.

"Kati ya watu tuliowapima 30 hadi 40, walikuwa na shida ya shinikizo la juu la damu lililosababisha misuli yao ya moyo kutanuka na wote hawa hawakuwa wanajijua kama wana matatizo mbalimbali katika mioyo yao," alisema Dk Rweyumamu.

"Wengine tuliowapima tuligundua wana shida kwenye valvu, moyo kutanuka, umeme wa moyo, matundu kwenye moyo na mmoja alikuwa na shida ya mshipa mkubwa unaosambaza damu sehemu zote za mwili (aorta) ulikuwa umevimba.”

“Huyu tuliyemkuta na matundu kwenye moyo ni mtu mzima wa miaka 45." Alibainisha Dk Rweyemamu.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ubungo, Dk Peter Nsanya, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kuadhimisha siku hiyo na kwenda kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo kwa wananchi wa Manispaa ya Ubungo na vitongoji vyake.

"Kila mwananchi alipimwa wingi wa sukari mwilini, urefu na uzito na wengine ambao walionekana kuwa na dalili za ugonjwa wa moyo, walifanyiwa vipimo zaidi,” alisema Dk Nsanya.

Alisema waliofanyiwa kipimo cha ECHO walikuwa 133, ECG 75, waliopewa dawa walikuwa 132 na 34 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa, hivyo wakapewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Aidha, kati ya watu 204 waliofanyiwa upimaji, 38 pekee ndio hawakuwa na matatizo yoyote ya moyo.

Ofisa Lishe wa JKCI, Husna Faraji, alisema katika upimaji huo walitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi na kuwaeleza umuhimu wa lishe katika afya zao na familia zao.

"Nilipata muda wa kutoa ushauri nasaha kwa mtu mmoja mmoja; wengi kati ya niliowaona, walikuwa na tatizo la uzito uliokithiri na hawakuwa wanatambua kuwa ni tatizo katika afya zao.”

“Wengine walikuwa hawajijui kama wana shida ya shinikizo la juu la damu na walikuwa wanatembea na kufanya shughuli zao kama kawaida," alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz