Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

186 wakutwa na TB

Tb Pic Data 186 wakutwa na TB

Sun, 19 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Zaidi ya watu  8,388 wamefanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kupitia kliniki tembezi ya hospitali maalumu ya tiba ya magonjwa ambukizi ya Kibong'oto katika kipindi cha miezi minne na watu 186 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo.

Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Kibong'oto, Dk  Leonard Subi wakati akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake akibainisha kuwa  wameendelea kuimarisha na kupanua wigo wa huduma na wanaifikia jamii kupitia kliniki tembezi.

Amesema hospitali ya Kibong'oto inasimamia gari moja lenye kliniki tembezi na wamekuwa wakienda maeneo ya machimbo ya madini kwa wachimbaji  ambao huathirika zaidi na kifua kikuu .

Amesema tayari wameenda  kwenye mikoa mingi ikiwemo Kilimanjaro, Manyara, Singida, Shinyanga, Tabora, Mwanza, Kagera na Mara na  katika kipindi cha miezi minne iliyopita wameweza kuchunguza zaidi ya wagonjwa 8,388 kati yao 186 waligundulika kuwa na kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu.

“Serikali imenunua magari makubwa matano yenye kliniki tembezi yana vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu na yamekuwa yakitumika kwenda katika jamii kufanya uchunguzi na kutoa matibabu  huko wananchi walipo na hopitali ya Kibong'oto tunasimamia gari moja.”

“Sisi tukigundua mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ni jambo kubwa sana kwa sababu mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ana uwezo wa kuambukiza  zaidi ya watu 10 hadi 20 kwa mwaka hivyo kwa kuokoa watu 186 na kuwaweka kwenye matibabu ina maana tumeokoa watu zaidi ya 2000 ambao wangeweza kuathirika kwa kuambukizwa kifua kikuu," amesema.

Dk Subi amesema mbali na kuendelea kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wagonjwa pamoja na kuwezesha upatikanaji wa dawa, pia kumekua na kiwango kikubwa cha uponaji wa kifua kikuu, ambapo tayari wameshafikia viwango vinavyokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Kwa upande wa kifua kikuu ya kawaida uponaji ni zaidi ya asilimia 90 hivyo mtu akipata kifua kikuu na kuanza matibabu kwa wakati ana uhakika wa kupona lakini kwa kifua kikuu sugu uponaji ni zaidi ya asilimia 75 ambapo viwango hivi vimepita viwango vya WHO,” amesema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz