Mabinti 165,304 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 wamepatiwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi (HPV) mkoani Mara katika kipindi cha miaka sita iliyopita
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 85 ya lengo la chanjo hiyo ambapo katika kipindi hicho mkoa ulilenga kuchanja jumla ya wasichana 193,380.
Akizungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo kwa mwaka huu, leo Aprili 24, 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu amesema mwaka huu wanatarajia kuchanja wasichana 229,249 katika wilaya zote za mkoa wa Mara.
Amesema chanjo ilianza kutolewa Aprili 22, 2024 na inatarajiwa kutolewa kwa muda wa siku tano mfululizo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya chanjo duniani, ingawa chanjo hiyo itatolewa hadi Desemba mwaka huu kwa awamu hii.
“Mwaka huu chanjo ni dozi moja, sio kama ilivyokuwa ya awali ambapo mlengwa alikuwa anachanjwa mara mbili. Niwahakikishie tu kuwa hii chanjo ni salama na imethibitishwa na mamlaka zote za kimataifa hadi za hapa kwetu,” amesema Dk Masatu.
Amesema chanjo ya mwaka huu, walengwa wake ni kuanzia miaka tisa hadi 14 na kwamba kwa umri huo walengwa wengi wanapatikana kwenye shule za msingi na sekondari.
“Chanjo itatolewa kwenye shule zote za msingi na sekondari, za umma na binafsi na maandalizi yamekamilika lakini pia chanjo hii itatolewa katika ngazi ya jamii kwa wale ambao kwa namna moja ama nyingine, hawatakuwa shuleni basi watapata kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya,” amesema.
Akizindua chanjo hiyo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Ally Mwendo, ameitaka jamii kushiriki kikamilifu ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
“Chanjo hii ni salama na inatolewa bila malipo yoyote, niwaombe wazazi na walezi tushirikiane pamoja na tuepuke aina yoyote ya upotoshaji ili twende sawa,” amesema.
Mwendo pia ametoa wito kwa wanawake wote ambao wanahisi kuwa na dalili za ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kufika mara moja kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya, kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya kitaalamu.
Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Musoma wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu juu ya masuala ya chanjo, ili kuondokana na dhana na imani potofu juu ya chanjo.
“Hakuna chanjo iliyowahi kupokelewa kwa moyo mmoja, lazima kunakuwepo na maneno mengi ya kuogopesha lakini ni vema elimu ikaendelea kutolewa ili watu waelewe na kuachana na upotoshaji,” amesema Veronica Juma.
Kwa upande wake, Mjora Masinde amesema: “Sasa hivi kuna uelewa sio kama zamani wakati tunakua,hali ilikuwa mbaya nadhani mafanikio haya yametokana na elimu. Naomba elimu iendelee kutolewa ili jamii nzima ipate uelewa.”