Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

1,000 wasaidiwa tiba ya mabusha

46d317dff53398289416150d5099c234 Mgonjwa wa Busha

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Equinor ya Tanzania imefanikiwa kuwasaidia wagonjwa 1,000 wenye mabusha, matende na ngiri maji kufanyiwa upasuaji mkoani Lindi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kambi ya matibabu hayo, Naomi Makota kutoka Equinor alisema kampuni hiyo imekuwa ikifadhili wagonjwa wa aina hiyo kwa miaka sita mfululizo.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia kitengo chake kinachokabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

Kambi inayoendelea hivi sasa ilianza Jumatatu wiki hii na inatarajiwa kumalizika Julai 21 mwaka huu, ambapo jumla ya wagonjwa 170 watapatiwa huduma hiyo.

Naomi alisema mradi huo ulianzia katika Mkoa wa Mtwara mwaka 2015 na baadaye kutekelezwa mkoani Lindi kuanzia mwaka 2017. Alisema mradi huo umekuwa ukipatiwa msaada wa Equinor kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Aidha, Naomi alisema madaktari hao wamekuwa wakiweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine mkoani Lindi na kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa mabusha na ngiri.

“Equinor na wadau wote katika mradi huu wanafurahia mafanikio ambapo kwa mfululizo wa miaka sita, wameweza kuwafikia wagonjwa zaidi 1,000 na kufanyiwa upasuaji huo na kwa wiki hii wagonjwa 170 wanatarajiwa kupata huduma hii,” alisema.

Naoni alisema kwa kipindi cha miaka sita ya utekelezaji wa mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni 500 za Tanzania ambazo ni msaada kutoka Equinor.

Equinor ni kampuni ya nishati yenye makao makuu katika mji wa Stavanger, nchini Norway na kwa hapa nchini inaendesha kitalu namba 2 cha gesi ikishirikiana na Exxonmobil na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Chanzo: habarileo.co.tz