Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Zinchenko, tulidhani tulichokiona kimetosha, kumbe bado

Zichenko Zinchenko, tulidhani tulichokiona kimetosha, kumbe bado

Sun, 5 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 pale Mtwara tulikuwa na beki hodari aliyeitwa Jacob Peter. Kwa sasa ni marehemu. Maisha yake ya siku za mwisho yalisikitisha. Hayakuakisi kipaji ambacho Mwenyezi Mungu alimpa. Aliishi kimaskini.

Lakini huyu ndiye aliyekuwa beki wa kwanza kutua katika mboni za macho yangu nikimuona kile ambacho baadaye mabeki wa pembeni walikuja kufanya baadaye. Alikuwa anapanda kwa kasi kwenda kushambulia. Kwenda kupiga krosi.

Wakati mwingine wakati anavuka katika mstari wa katikati tulikuwa tunampigia kelele asivuke. Kisa? Tuliamini kwamba kazi ya beki wa pembeni na safu nzima ya ulinzi ilikuwa ni kuzuia tu.Mambo ya kushambulia yalikuwa ya mawinga na washambuliaji.

Miaka mingi baadaye limekuja jambo la kawaida kwa mabeki kufanya kile ambacho marehemu Jacob alifanya zamani. Lakini kama nilidhani nilichokiona kimetosha basi kumbe nilikosea. Kuna watu wanajiona wataalamu wa mpira wameleta mambo mengine kabisa ambayo hata marehemu Jacob hakujua kama yangefanyika.

Nilikuwa nalitazama bao la kwanza la Arsenal dhidi ya Everton Jumatano usiku katika Uwanja wa Emirates. Oleksandr Zinchenko alimpasia mfungaji wa bao, Bukayo Saka huku yeye akiwa amesimama kama kiungo wa upande wa kulia.

Beki wa kushoto anafikaje pale ambapo Zinchenko alikuwa amesimama? Hakukuwa na faulo wala kona kwamba labda ni mpira ambao ulikuwa umemrudia. Hapana, alijikuta pale kwa sababu ya maarifa ya makocha wetu wapya kina Pep Guardiola.

Ndio, unaanza kumtaja kwanza Pep kisha unakuja kumtaja Mikel Arteta. Pep ni mwalimu wa Arteta. Alikuwa msaidizi wake pale Manchester City. Sina uhakika kwamba lilikuwa wazo la Arteta kwamba beki wa kushoto awe anakuja kucheza kama kiungo wakati mpira ukiwa upande wa kulia. Lakini kwa sababu Arteta alikuwa msaidizi acha tuseme kwamba lilikuwa wazo la Pep.

Na sasa mpira umefika hapa. Beki wa kushoto anakuja kuzurura kama kiungo kwa muda mrefu wa mchezo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba timu inakuwa na viungo wengi na kuwaelemea wapinzani wakati wao wakiwa na mpira.

Wakati mpira ukiwa katikati na Zinchenko yupo katikati mlinzi wa Brazil, Gabriel anakwenda kuibia upande wa kushoto kwa ajili ya kulinda nafasi ile kama kuna dharura itatokea. Hawa kina Pep sijui wanatuharibia mpira au wanatutengenezea mpira. Tunaishi katika dunia ambayo wamebadili kila kitu.

Kama kila kocha akibadili staili na kutaka beki wa kushoto aingie katikati nadhani maisha yatakuwa magumu kwa baadhi ya watu. Mfano, pale pale Arsenal, beki mwingine wa kushoto, Kieran Tierney ameshaathirika na mabadiliko haya.

Tierney ana kipaji maridhawa lakini maskini kijana wa watu kutoka Scotland alizaliwa na kukua katika namna ambayo mlinzi wa kushoto kazi yake ni kuzuia na kupandisha mashambulizi mbele. tayari alishakuwa beki wa kisasa katika kuzalisha mashambulizi ya hatari upande wa kushoto.

Leo hana nafasi katika kikosi cha Arteta kwa sababu Zinchenko anaonekana kuwa hodari katika kuingia ndani na kucheza kama kiungo wakati soka likiendelea uwanjani. Sidhani kama Tierney anaufurahia mfumo huu lakini ndio tayari umeshaletwa.

Kama kila kocha akiuchukua mfumo huu ina maana kuna wachezaji wengi wazuri wa nafasi hiyo tunaweza kuwapoteza. Haitashangaza sana kwa sababu tayari kuna wachezaji wengi wa nafasi nyingine tumewapoteza katika nafasi zao kutokana na mabadiliko ya mfumo kutoka kwa makocha hawa wajuzi wa mambo ambao wanataka kuubadili mchezo wenyewe.

Mfano katika nafasi ya kipa. Siku hizi kama hauwezi kucheza vizuri kwa miguu unaonekana haufai. Sisi kwa miaka mingi tuliamini kazi ya kipa ni kudaka au kupangua mipira ya hatari. Leo kazi ya kipa ni kuanzisha mipira kwa miguu kwa ustadi kuelekea mbele. Hakuna kubutua.

Ni katika namna hiyo hiyo wakati Waingereza waliamini kwamba Joe Hart alikuwa kipa mzuri kwao, Pep akaja na kumuondoa katika lango la Manchester City akiamini kwamba alikuwa hawezi kutumia miguu yake vema. Kwa waliofariki kabla ya hapo leo wakiamka hawawezi kuamini kwamba moja kati ya sifa kubwa ya kipa ni kutumia miguu yake vema kucheza mpira kama ilivyo kwa wachezaji wa ndani.

Lakini tunaishi katika dunia mpya ambayo winga anayetumia mguu wa kushoto inabidi acheze kulia. Zamani kazi ya winga ilikuwa kupiga majalo kwa ajili ya washambuliaji wawili wanaokaa ndani. Leo mambo yamebadilika.

Mchezaji anayetumia mguu wa kushoto alipaswa kukaa kushoto kwa ajili ya kupiga krosi. Kina Edibily Lunyamila walikuwa wanafanya hivyo. Lakini leo kina Lionel Messi, Saka, Riyad Mahrez, Mohamed Salah na wengineo kibao wanakaa upande wa kulia.

Krosi zimekuwa sio habari ya mjini tena. Unakaa kulia, unapiga chenga unaingia kwa ndani na unakuwa katika nafasi nzuri ya kufunga. Msimu uliopita wakati City wakichukua ubingwa mfungaji wao bora alikuwa Mahrez ambaye alikuwa anatokea kulia akitumia mguu wake wa kushoto.

Lakini Messi amefunga mabao mangapi katika dunia hii akitumia upande huo? Salah kwa misimu mitano akiwa na Liverpool amekuwa akifunga mabao 20 na zaidi katika kila msimu na daima amekuwa akitokea upande huo. Saka ndiye mfungaji bora wa Arsenal msimu uliopita amekuwa akifunga akitokea upande wa kulia.

Na upande wa kushoto wanacheza watu wanaotumia miguu ya kulia. Ndio hawa kina Gabriel Martinez. Mchezo umebadilika jumla siku hizi. Wachezaji wanaomudu kucheza kwa sasa ni wale ambao wanaendana na mabadiliko ya mchezo wenyewe.

Unaweza kuwa na kipaji kikubwa lakini kama hauendani na mabadiliko ya mchezo wenyewe basi unaishia kukaa benchi tu. Tupo katika mfumo ambao mshambuliaji wa kati sio lazima afunge. Inabidi afanye kazi nyingi uwanjani na pia kuwawezesha wengine kufunga.

Kombe la Dunia mwaka 2018 pale Moscow, Olivier Giroud hakufunga bao hata moja lakini kocha, Didier Deschamps alikuwa anamuona shujaa kwa namna ambavyo alikuwa anaunganisha mchezo kwa wenzake. Zamani enzi za kina Pele sifa kubwa ya mshambuliaji ilikuwa kufunga mabao.

Sisi ambo tuliishi tangu zamani na kuuona mchezo ukibadilika wakati tukiamini kwamba tumeshuhudia mabadiliko mengi ya mchezo wenyewe, kumbe ndio kwanza mabadiliko yanaanza. Tulidhani tulichokiona kimetosha, kumbe bado.

Columnist: Mwanaspoti