Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ZeKICK: Mayele mkali kila kona

Mayele Mbele Fiston Mayele

Sun, 30 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wale waliokuwa wakiibeza Yanga wakati ikitangaza kumsajili straika Fiston Mayele, huenda kwa sasa wanazificha sura zao, kutokana na kazi kubwa anayofanya Mkongomani huyo ndani ya timu hiyo.

Kwani kwa sasa Mayele (27) ndio jina linalotamba nchini kutokana na kasi yake ya upachikaji mabao katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu akiwa na kikosi cha Yanga.

Nyota huyo kutoka DR Congo, ndiye kinara wa ufungaji katika ligi hadi sasa akiwa amefumania nyavu mara sita kwenye mechi 13 alizoitumikia Yanga.

Uwezo mkubwa wa kuwahi kufika katika nafasi sahihi pindi wanapolishambulia lango la timu pinzani, shabaha ya goli na mikimbio mizuri, ni baadhi ya sifa ambazo zimemfanya Mayele awe adui wa nyavu za timu pinzani kila zikutanapo na Yanga.

Kwa wafuatiliaji wa mechi za Ligi Kuu Bara, hapana shaka hakuna atakayepinga ubora wa Mayele na ni wazi kwa uwezo aliouonyesha hadi sasa, timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo tofauti na Yanga, zinatamani kuwa na nyota huyo wa zamani wa AS Vita Club.

Anafunga, anapika mabao

Akiwa na mabao sita (6) kwenye Ligi Kuu hadi sasa, Mayele amekuwa tegemeo la Yanga sio tu katika kufumania nyavu bali pia hata kupika mabao jambo ambalo huwa ni adimu kwa mastraika wengi wa kati kama ilivyo yeye.

Mshambuliaji huyo amelidhihirisha hilo katika mechi alizoichezea timu hiyo hadi sasa na mbali ya mabao aliyofunga, anashika nafasi ya pili kwa kupiga pasi nyingi za mwisho hadi sasa akiwa amepiga pasi mbili za mabao.

Nyota wanaoongoza katika kupiga pasi za mwisho, kila mmoja amefanya hivyo mara tatu na miongoni mwao ni beki wa kushoto wa Dodoma Jiji FC, abubakar Ngalema.

Mchawi wa kipindi cha kwanza

Mayele amekuwa hatari zaidi wa kufumania nyavu katika dakika 45 za kwanza za mchezo na kipindi cha pili amekuwa sio tishio sana jambo analopaswa kulifanyia kazi.

Mabao yote sita ambayo Mayele ameifungia Yanga katika Ligi Kuu hadi sasa, yamepatikana kwenye kipindi cha kwanza na hajafunga lolote katika dakika 45 za mwisho.

Nyota huyo amefunga mabao hayo sita kwenye mechi dhidi ya KMC, Azam, Mbeya Kwanza, Biashara United, Dodoma Jiji na Coastal Union.

Bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu alifunga dhidi ya KMC katika dakika ya nne, linalofuata akapachika dhidi ya Azam FC kwenye dakika ya 36 na dhidi ya Mbeya Kwanza akafumania nyavu dakika ya 25.

Bao dhidi ya Biashara United alifunga katika dakika ya 40 na mechi dhidi ya Dodoma Jiji pamoja na Coastal Union alifumania bao dakika ya 41 katika kila mchezo.

Dakika 1000 za dhahabu

Mayele ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Yanga ambao wamecheza mechi zote za Ligi Kuu hadi sasa na hajakosa wowote huku mingi akianza katika kikosi cha kwanza.

Mshambuliaji huyo amecheza jumla ya dakika 1002 ikiwa ni wastani wa dakika 77 kwa kila mechi na ni mechi moja tu aliingia akitokea benchi nayo ni ile ya ugenini dhidi ya Prisons aliyocheza kwa dakika 23.

Kati ya mechi 13 alizoichezea Yanga za Ligi Kuu msimu huu, mechi nne amecheza kwa dakika zote 90 kwa kila mchezo huku mechi nane akifanyiwa mabadiliko ambayo mara kwa mara amekuwa akipishana na Heritier Makambo.

Anakufunga hewani na ardhini

Mayele ameonyesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu kwa kutumia kichwa na miguu yote miwili kwa ufasaha jambo ambalo sio rahisi kuliona kwa mastraika wengi nchini.

Katika mabao sita aliyopachika kwenye Ligi Kuu hadi sasa, moja amefunga kwa kichwa, manne kwa mguu wa kulia na moja amepachika kwa mguu wa kushoto.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz