Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ZeKICK: Huyu Mkude kashindikana

Mkude Simba SC Kiungo wa Simba, Jonas Mkude

Sun, 17 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashabiki wa Simba huwaambii kitu kwa Jonas Mkude a.k.a Nungunungu. Achana na ishu zake za utovu wa nidhamu ambazo kila mara zinamtia matatani kwa mabosi wao, lakini umahiri wake wa kuibeba timu ndio unaowapa furaha mashabiki hao.

Ukiachana na hilo, lakini katika kikosi cha sasa cha Simba kinachoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kilichotinga robo fainali ya Kombe la ASFC na Kombe la Shirikisho Afrika, Mkude ndiye mchezaji mwandamizi.

Utabisha nini wakati ni zaidi ya miaka 10 yupo kwenye kikosi hicho? Mkude ameanza kuitumikia timu ya vijana Simba U20 iliyombeba kutoka kwenye michuano Rolling Stone jijini Arusha na kupandishwa timu ya wakubwa tangu Januari, 2011 na amesalia hadi sasa licha ya ingia toka ya wachezaji mbalimbali.

Historia ya Mkude na Simba inaanzia wakati akicheza timu ya vijana, wakati huo ikinolewa na Selemani Matola akisaidiana na Amri Said ‘Jaap Stam’ chini ya Meneja Patrick Rweyemamu.

Kiungo huyo fundi kwenye majukumu ya kukaba amekuwa muhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Simba, akiletewa mastaa wengi kutoka mataifa mbalimbali lakini amehimili ushindani na kubaki kuwa namba moja hasa linapokuja suala la nani aanze kikosi cha kwanza eneo la kiungo mkabaji.

Mwanaspoti linakuletea mastaa waliopita Simba na kumkuta na baada ya mikataba yao kuisha wakaondoka huku wengine wakiondoka kutokana na majeraha na kukosa nafasi ya kucheza.

TADDEO LWANGA

Ni kiungo aliyesajiliwa Simba na kumpa changamoto Mkude kwa kumuweka benchi kutokana na ubora aliokuwa nao, lakini mara baada ya kuumia tu alimpisha tena kiungo huyo ambaye hadi sasa ndiye anayecheza kikosi cha kwanza.

Katika dirisha dogo msimu uliopita Simba walimsajili Lwanga kama mchezaji huru akitokea nchini Misri na mwanzo alipokuwa akikitumikia kikosi hicho alionekana mchezaji wa daraja la kawaida, ila baada ya kuzoea alionyesha ubora wa hali ya juu na kumfanya Mkude kuwa mchezaji wa kawaida.

Tangu alipoumia amemrudisha Mkude kwenye ufalme wake na kumfanya Mganda huyo kuwa mchezaji wa kusubiri nje nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba. Upepo umebadilika. Mfalme kwenye kiungo cha ulinzi cha Simba sasa ni Mkude. Hii ni taa nyekundu kwa Lwanga.

JAMES KOTEI

Ilikuwa ni vita kati yake na Mkude kila mmoja alikuwa anahitaji namba kikosi cha kwanza, lakini ubora wa Mkude ulidhihirisha kuwa ni bora kuliko Kotei baada ya kocha Patrick Ausems kupitisha jina lake kwa uongozi kuwa ni moja ya wachezaji ambao hawatakiwi kuongezwa mikataba na dirisha la usajili walimuongeza Sharaf Shiboub ili kusaidiana na Mkude.

GERSON FRAGA

Maumivu ya goti yaliyomfanya akae nje ya uwanja mwaka mzima yalimuondoa Simba kwani alijaribu kumpa changamoto Mkude, lakini bahati haikuwa upande wake baada ya mkataba wake kwisha Simba hawakuonyesha nia ya kumuongeza kutokana na ubora wa kiungo wao mzawa.

SAID NDEMLA

Ndemla ametemwa Simba mwanzoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kwisha na kutimkia Mtibwa Sugar, lakini hakuwa na ufalme Msimbazi kama ilivyo Mkude na kutokana na uwezo wake alikuwa anabahatisha nafasi za kucheza.

MWINYI KAZIMOTO

Atua Simba msimu wa 2011/12 akicheza kwa mafanikio msimu mmoja na baadaye kutimkia Al Markhiya ya Qatar alikocheza misimu miwili na msimu wa 2015 alirudi Simba hadi alipoamua mwenyewe kuondoka na kwenda JKT Tanzania ambayo anaitumikia hadi sasa.

JUSTICE MAJABVI

Ni kiungo aliyependekezwa na kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr, lakini hakusajiliwa moja kwa moja, bali alifanyiwa majaribio na baadaye kupewa mkataba wa mwaka mmoja na baada ya kumalizika hakuongezwa mwingine kutokana na utovu wa nidhamu.

ABDALLAH SESEME

Ni zao moja na Mkude kutokana na wote kuanzia timu ya vijana na baadaye kupandishwa, lakini hakuwa bora sana na ndipo uongozi ulipoachana naye na sasa anakipiga Kagera Sugar akiwa na uwezo wa kawaida tofauti na Mkude ambaye amekuwa akikutana na changamoto nyingi, lakini bado anapambana Msimbazi.

MUSSA NDUSHA

Usajili wake ndani ya kikosi cha Simba ulikuwa na mgogoro na timu ya FC Renaissance ya RD Congo hadi kufikishana Fifa kutokana na waajiri wake hao wa zamani kugoma kutoa ITC, lakini pamoja na vurugu hizo hakutoa changamoto kutokana na kiwango chake kuwa cha kawaida.

PATRICK MAFISANGO

Mei 17, 2012 ndio ulikuwa mwisho wa kiungo huyu fundi na kipenzi cha mashabiki baada ya kupata ajali na kufariki dunia papohapo jijini Dar es Salaam, ambapo aliacha kumbukumbu nzuri Simba kutokana na umahiri wake uwanjani.

ABDULSWAMAD KASSIM

Alisajiliwa na Simba dirisha dogo la usajili uliopita, lakini ubora aliokutana nao Simba ulimtisha kiungo huyo na kuamua kuomba kutolewa kwa mkopo na sasa anakipiga Ruvu Shooting.

MATOLA ATIA NENO

Akimzungumzia Mkude, Matola ambaye ni kocha msaidizi wa Simba anasema: “Nakumbuka nilimuona Jonas Mkude kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya Rolling Stone yaliyofanyika Arusha, nikiwa na Patrick Rweyemamu (meneja wa sasa Simba). Tuliona ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na angeweza kutusaidia kwenye mashindano ya vijana, kwa hiyo tulimchukua na kuungana naye kwenye timu yetu ya Simba B.

“Tulifurahi alikuwa mchezaji muhimu kwenye timu na aliisaidia sana. Tuliishi naye kwenye timu ya vijana kwa miaka mitatu kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa.”

Matola anasema: “Kocha Patrick Phiri ndiye alimchukua (timu ya wakubwa), baadaye Phiri aliondoka timu ikawa haina kocha ikabidi nichukuliwe kutoka timu ya vijana nikaenda kusaidia timu ya wakubwa kwa muda, kwa hiyo tukakutana tena na Mkude.

“Tangu alivyopandishwa alikuwa bado hajaanza kucheza, mimi ndiye nilikuwa mwalimu wa kwanza kumpa nafasi Mkude kwenye timu ya wakubwa. Ilikuwa Simba dhidi ya Moro United baada ya Mwinyi Kazimoto kuumia.”

Kocha huyo anaongeza kuwa: “Alivyoingia alionyesha uwezo mkubwa sana na hapo ndipo ilianza safari ya Mkude kuchukua nafasi kwenye timu ya wakubwa hadi leo. Juhudi na uwezo ndio vinamfanya adumu hadi leo. Amekuwa mchezaji muhimu ambaye kacheza kwa muda mrefu.”

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz