Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Zamu ya Martinez kuingia katika mtego wa Ronaldo

Martinez X Ronaldo Portugal Zamu ya Martinez kuingia katika mtego wa Ronaldo

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wikiendi zinapita halafu zinapita tena. Halafu zinakuja nyingine zinapita tena. Roberto Martinez anakuwa ofisini kwake akishuhudia ligi mbambali kubwa barani Ulaya. Halafu huwa anawasha TV yake kushuhudia Ligi Kuu Saudi Arabia kumtazama nahodha wake, Cristiano Ronaldo.

Mechi za kimataifa zinapowadia anakaa ofisini kwake pale Lisbon kwa ajili ya kuchagua kikosi chake cha timu ya taifa ya Ureno. Mtihani mwepesi kwake kwa wachezaji wa Kireno wanaocheza katika ligi kubwa za Ulaya. Kina Bruno Fernandes, Rafael Leao, Bernardo Silva na wengineo lazima wawepo.

Halafu Cristiano Ronaldo naye lazima awepo. Mtihani unakuwa hapa. Kasi imepungua katika miguu ya Ronaldo. Tuliona tangu katika Kombe la Dunia lililopita. Lakini kadri kasi inavyopungua katika miguu ya Ronaldo ndivyo hamu ya kucheza soka inavyoongezeka.

Amegombana na kocha wa Manchester United, Erik Ten Hag kwa sababu ya hamu hii ya kupenda kucheza. Hataki kuwekwa benchi, hataki kutolewa. Anataka kucheza mechi zote. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 37.

Baada ya hapo akaenda zake Qatar akagombana na kocha wa timu ya taifa, Fernando Santos. Kisa kilikuwa kilekile tu. Ronaldo alikuwa hataki kukaa benchi na alikuwa hataki kutolewa ‘sub’. Siku moja aliwekwa benchi dhidi ya Uswisi halafu aliyepangwa Goncalo Ramos akafunga mabao matatu ‘hat trick’.

Majuzi Santos amekaririwa akidai kwamba Ronaldo hajawasiliana naye tangu baada ya fainali za Qatar. Ni wazi kwamba amemnunia. Katika umri huu bado Ronaldo ana kiu ya hali ya juu kuingia uwanjani kucheza soka.

Na sasa mzigo huu umemwangukia Martinez. Kocha wa kwanza asiye Mreno wala Mbrazili kufundisha kikosi cha timu ya taifa ya Ureno. Analazimika kushughulika na mchezaji mwenye jina kubwa ambaye amegoma kustaafu. Mchezaji ambaye taifa lake linamhusudu.

Kazi ingekuwa ndogo kwa Martinez kama Ronaldo angeamua kustaafu mwenyewe. Wakati mwingine kocha anataka kukisuka kikosi chake upya kwa wachezaji wenye damu changa, lakini mchezaji kama Ronaldo anapogoma kuvua viatu unachanganyikiwa.

Mchezaji mkubwa, aliyetwaa mataji matano ya mwanasoka bora wa dunia. Aliyetwaa mataji 34 ya michuano mbalimbali ikiwemo matano ya Ligi ya Mabingwa. Aliyetwaa Euro. Mchezaji ambaye anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika kikosi cha timu ya taifa, lakini pia anaongoza kwa kufunga mabao mengi kwa timu za taifa kwa ujumla duniani kote.

Zaidi ya yote ni nahodha. Amegoma kustaafu. Mpaka sasa anapocheza mechi ya kufuzu dhidi ya vikosi dhaifu vya Lichtenstein, Cyprus na Malta huwa anafunga kama kawaida. Unaweza kufanya nini zaidi kwa mchezaji huyo?

Unajua wazi kwamba katika mechi za ushindani miguu tayari imemsaliti Ronaldo. Ronaldo halisi asingekuwa anatolewa katika mechi ngumu ya Kombe la Dunia pale Qatar. Hilo jambo lisingefirika. Lakini Santos aliamua kuchukua uamuzi mgumu na amenuniwa mpaka leo.

Angekuwa kocha wa kariba ya Jose Mourinho angeweza ‘kumng’ata jongoo kwa meno’ na kuchukua uamuzi mgumu wa kumpumzisha Ronaldo nyumbani kisha kuanzisha kizazi kipya cha Ureno.

Lakini Martinez amelaza shingo upande.

Upande mmoja naupenda ushujaa wa Ronaldo. Nawajua mastaa ambao wameachana na mpira wakiwa na miaka 33 huku wakiwa hoi na hawana hamu na soka. Hii sio kwa Ronaldo. Tatizo nahisi anawapa wakati mgumu makocha ambao wanahofia Uronaldo wake.

Nilimsifu alipoamua kwenda kucheza Al Nassr pale Saudia. Kule Ronaldo anacheza muda wote na anafunga vizuri tu. Ligi sio ngumu na anapata pesa nyingi za pensheni. Kama Ronaldo angeendelea kubaki Ulaya nadhani angesumbuana na makocha tu.

Mambo hufika mwisho. Kwa Ronaldo sidhani kama yanafika mwisho. Nadhani kwa sasa ananyatia kucheza michuano ya Euro 2024. Kwa jinsi watu wanavyoshindana barani Ulaya halafu yeye anacheza Saudi Arabia sioni namna gani atakuwa katika nafasi ya kushindana zaidi wakati huo.

Hata hivyo Martinez atalazimika kumpanga. Ni nahodha na anamuhofia pia kutokana na historia yake ya soka. Mmoja kati ya wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika uso wa ulimwengu. Ana kiu ya kucheza kila siku na anawaweka makocha katika wakati mgumu.

Wakati mwingine wachezaji wakubwa kama Pele, Diego Maradona, Johan Cruffy waliwasaidia makocha wa timu zao za taifa kwa kuamua kustaafu wenyewe. Wasipostaafu majina yanakuwa makubwa kwa kocha kuwaweka nje. Hasa pale wanapong’ang’ania kucheza.

Hasimu wake Lionel Messi naye miguu imeshamsaliti. Tofauti yake na Ronaldo ni kwamba wakati wakiwa Qatar yeye alikuwa na miaka 35 na alikuwa amechangamka zaidi ya Ronaldo. Wakati Ronaldo akilumbana na Santos, Messi alikuwa akiiongoza Argentina kufika fainali na kutwaa taji lenyewe.

Tayari Messi ameweka wazi kwamba hatashiriki katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia ambayo itafanyika Marekani, Canada na Mexico. Lakini pia ameweka wazi nia yake ya kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Argentina baada ya michuano ya mataifa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa Amerika ambayo nayo itafanyika mwakani.

Wakati huo Messi atakuwa na umri wa miaka 37 na akiendelea zaidi ya hapo atakuwa kama Ronaldo tu. Atakuwa anamuweka kocha wake katika wakati mgumu kwa sababu ni ngumu kumuweka Messi benchi. Unaweza kumtoa uwanjani lakini ni ngumu kuanza mechi bila ya Messi akiwa fiti kama ni mzee.

Tutaendelea kutazama sinema ya Martinez na Ronaldo itakapoishia lakini kwa sasa sioni kama Ronaldo ana nia yoyote ya kutangaza kustaafu. Muda mzuri zaidi kwake ilikuwa ni baada ya Ureno kutolewa katika michuano ya Kombe la Dunia pale Qatar.

Columnist: Mwanaspoti