Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga wana matatizo gani Afrika?

Yanga Mguu Sawa Kikosi cha Yanga Afrika

Thu, 13 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna ubishi Yanga ndiyo timu bora nchini kwa sasa. Hakuna ubishi. Tayari wamecheza mechi 42 za Ligi Kuu bila kupoteza. Sio jambo dogo. Tayari wanamiliki taji la ligi na lile la FA. Sio jambo dogo.

Ufalme wa ndani sio stori tena kwa Yanga, shida kubwa ya Yanga iko Kimataifa. Shida kubwa ya Yanga ipo kwenye ushiriki wao kwenye michuano ya CAF.

Wikiendi iliyopita walikuwa Uwanja Mkapa wakiikaribisha Al Hilal kutoka nchini Sudan. Pamoja na ubora wote walikuwanao Yanga, mechi ilimalizika kwa sare tu.

Sio aina ya matokeo mazuri na hasa kwenye soka la Afrika. Yanga wanakosea wapi Kimataifa? Naomba tushirikiane kwenye mjadala huu. Mpira wa Afrika bado haujafikia kuwa Sayansi kwa 100%.

Nadhani kuna upande wa Sayansi, na kuna upande wa siasa. Upande wa Sayansi ni rahisi kwa sababu unahusisha maandalizi ya timu. Kuanzia kuwa na wachezaji bora, kambi bora na makocha bora.

Sina tatizo kabisa na Yanga kwenye eneo hili. Uwepo wa Fiston Mayele, Aziz KI, Feisal Salum ni uthibitisho Yanga imekalimilika. Vipi kuhusu upande wa siasa za Afrika?

Hapa ndiko ninakoona mapungufu makubwa. Bado siioni timu imara ya Yanga kwenye kucheza siasa za Soka la Afrika.

Mpira wa Afrika una utamaduni wake wa kitofauti. Ni mchezo ambao zaidi ya asilimia 90, kila timu inayocheza nyumbani hulazimisha kushinda.

Sio mara zote timu za nyumbani hushinda lakini ni kwa asilimia kubwa. Timu zote zinazofanya vizuri kwenye michuano hii ya Afrika ni zile zenye uwezo wa kushinda nyumbani.

Yanga wana timu bora sana nchini kwa sasa lakini hiyo sio sababu pekee ya kufanya vizuri Afrika.

Kuna 50% nyingine ambayo Yanga wanaikosa. Bao la Mayele lililokataliwa kwa Mkapa, kama watafunga Wasudani kwenye mechi ya marejeano, si ajabu Yanga wataitwa kati.

Sio ajabu mwamuzi ataliruhusu. Hizi ndiyo Siasa za Afrika ambazo nadhani Yanga bado hawajakomaa.

Huku ndiko Yanga anakozidiwa na Simba. Yanga wameandaa timu yao Kisayansi lakini ili kufanya vizuri Afrika ni lazima ujiandae kucheza siasa za soka letu.

Pamoja na kuwa Simba inaonekana kuwa kidogo chini ya Yanga kiubora lakini kama wangecheza na wale Wasudani kwa Mkapa, Mnyama angetaka tu. Sisemi kwamba Simba anashinda kila mechi kwa Mkapa, hapana.

Tunajua pia kuwa ameshatolewa mara nyingi tu nyumbani lakini huwa kwa sababu nyingine. Unadhani kuna sababu nyingine iliyochangia Yanga kutoka sare kwa Mkapa wikiendi iliyopita? Niandikie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba Yangu ya simu hapo juu.

Ni miaka 24 sasa tangu Yanga anafuzu mara ya mwisho kwenda hatua ya Makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni umri wa mtu mzima. Ni umri wa mtu mwenye mke na watoto. Ni umri ambao kijana anamaliza Chuo Kikuu!

Yanga wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kununua wachezaji wazuri na kuajiri makocha wazuri lakini, hawajawekeza vya kutosha kwenye siasa za soka la Afrika.

Bado wana nafasi ya kujirekebisha kuelekea mechi ya marudiano na Al Hilal pale Sudan ingawa haitakuwa rahisi.

Simba anaweza kuwa na timu inayosua sua hapa ndani lakini anafanya vizuri Kimataifa. Unajua ni kwa nini? Ni rahisi tu.

Simba wana timu ya watu wanaojua kucheza siasa za mpira wa Afrika.

Yanga wanachoweza kwa uhakika kwenye zama hizi ni kuifunga Simba tu! Al Hilal wana uwekezaji mkubwa kuliko Yanga.

Al Hilal wana rekodi nzuri sana kwenye michuano ya CAF kuliko Yanga.

Unapokutana na timu ya aina hii, unapaswa kutumia kila faida unayoiona mbele yako.

Yanga wanaweza kufuzu Sudan lakini wamefanya makosa makubwa kutopata ushindi nyumbani.

Hakuna jambo gumu Afrika kama kwenda kushidna ugenini kwenye timu ambayo inakuzidi pia kila kitu. Hakuna kitu kigumu Afrika kama kutegemea wachezaji tu.

Pamoja na uwekezaji mkubwa wa Al Ahly kwa wachezaji na benchi la Ufundi, wamewekeza pia kwenye kutengeneza timu ya kucheza siasa za soka letu na ndiyo maana wamefanikiwa. Yanga bado hajakomaa kwenye eneo hili.

Ukiona Simba anasafiri na kwenda kushinda nchini Angola, usidhani kuwa ni rahisi. Simba amewekeza sana kwenye siasa za Afrika. Kuna watu wengi sana wako nyuma ya CEO, Barbara Gonzalez.

Yanga wasione aibu wakati mwingine wa kuzungumza na Simba. Utani wa Jadi uko pale pale lakini kwenye kusaka ushindi wasione shida kujifunza. Mechi ya marudiano kule Sudan, Yanga watapelekewa moto sana.

Ni mahali ambapo timu zote zinapaswa kucheza sambamba. Timu ya ndani ya Uwanja na ile ya siasa za Afrika.

Yanga wanahitaji kuwa wa kwanza kufunga bao. Wakiruhusu bao la mapema, presha itakuwa kubwa sana kwao. Bado nafasi ipo. Kama siasa za soka letu hazitowaathiri, Yanga wana wachezaji wengi tu wakubwa wa kushinda mechi ya Sudan.

Mechi kubwa kama hizi wakati mwingine huamuliwa na wachezaji wakubwa. Unapokuwa na Bernard Morrison kwenye ubora wake, unapokuwa na Fei Toto kwenye kiwango kizuri, muda wowote wanaweza kukubeba.

Kazi kubwa ya viongozi kwenye mechi ya marudiano, ni kucheza na siasa za soka la Afrika. Ndani ya Uwanja nawaona Yanga wamekamilika kupambana na Al Hilal.

Columnist: Mwanaspoti