Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga wameanza vizuri, kazi bado

Yanga Squad Final Kikosi cha Yanga

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwalimu wangu wa somo la jiografia katika darasa la nne alitufundisha wakati ule kwamba kadri unavyosafiri kwenda juu zaidi kutoka usawa wa bahari ndivyo hali ya hewa inakuwa ya baridi zaidi na wepesi wa kupumua unakuwa mgumu zaidi.

Unaweza kusema hivyo hata katika mashindano ya michezo hasa mpira wa miguu kwamba timu inavyozidi kusonga mbele kwenye mtoano na upinzani pia unakuwa mgumu.

Mchezo wa juzi wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya kombe la shirikisho Afrika (Caf Confederation Cup) kati ya Young Africans na Marumo Gallants ya Afrika Kusini uliofanyika kwenye uwanja wa Benjamini mkapa unaweza kuthibitisha ukweli huo.

Tangu msimu huu wa mashindano ya Afrika uanze,Young Africans hawajawahi kupata majaribu makubwa nyumbani kama waliyopata dhidi ya marumo Gallants.

Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi alikiri wazi, ulikuwa ni mchezo mgumu sana na timu haikuanza kama alivyopangilia.

Marumo ni wazuri na hawajabahatisha kufika hapo walipo.Marumo ni kielelezo cha mabadiliko makubwa yanayotokea katika ligi na klabu za Afrika Kusini kiasi cha kutishia utawala wa vilabu vya kaskazini mwa Afrika.

Mwisho wa siku Yanga wanajivunia matokeo ya 2-0 waliyoandikisha kupitia magoli ya Aziz Ki na Bernad Morrison.

Pamoja na kushinda mchezo wa Dar es Salaam, bado Yanga wana kibarua kizito kuhakikisha wanamaliza mchezo na kutinga nusu fainali watakapokutana tena juma lijalo nchini Afrika Kusini.

Wapinzani wa Yanga wana rekodi nzuri wanapocheza nyumbani na bila shaka Yanga ili wanalijua na wanapaswa kuchukua taadhari kubwa.

Hata hivyo,Yanga pia wana rekodi ya kushinda ugenini hata dhidi ya timu ambazo hapo kabla ziliaminika kuwa hazishindwi nyumbani kama Rivers United ya Nigeria.

Uwezo wa kocha Nabi katika kusoma mchezo wa adui ni moja ya silaha ambazo Yanga wanazo. Kwa waliofuatilia mchezo wa juzi watakuwa walishangazwa na kocha kufanya mabadiliko ya kuwatoa wachezaji wanne na kuwaingiza wanne wengine na hivyo kuirudisha timu mchezoni na kuupeleka mchezo mpaka mwisho na kuibuka na ushindi huo wa 2-0.

Mchezo huo unakuwa ni kama dakika 90 za kwanza na bila shaka kocha mkuu atakuwa amemsoma adui yake kwa manufaa ya mechi ya marudiano Mei 17.

Ushindi wa 2-0 ni ushindi mkubwa lakini si hakikisho la kusonga mbele hivyo Yanga lazima wajipange kuanzia uongozi,benchi la ufundi na wachezaji wenyewe kuhakikisha mchezo unaofuata wanauchukulia kama ndio fainali.

Yanga wana uongozi makini, benchi la ufundi pana na lenye uwezo mkubwa chini ya Nasredine Nabi na pia kikosi kipana ambacho hakina tofauti kubwa kati ya wachezaji wanaoingia na wanaotoka.

Hao wote wajue kuwa wanawawakilisha wanayanga lakini zaidi watanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu ushiriki wa timu za Tanzania na pia kwa motisha ambayo amekuwa akitoa zawadi ya fedha maarufu kama goli la mama ambazo Yanga tayari wameweka milioni 20 kibindoni kwa magoli mawili ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imetamka bungeni juu ya kufurahishwa na ushindi wa Yanga na kuwatakia safari njema kuelekea fainali.

Mchezo wa marejeano dhidi ya Marumo Gallants ni mgumu, lakini Yanga wana kila kitu cha kuwawezesha kushinda mchezo huo na kutinga fainali hata kuchukua ubingwa. Hatua waliyofikia kijiografia inatia baridi na ina ugumu wa kupumua lakini mwendo na kazi iliyofanyika huko nyuma ni kubwa kuliko iliyobaki.Ni timu mbili tu zimesimama kati ya Yanga na Kombe la Shirikisho.

Ni malumo Gallants na mshindi kati ya Asec Mimosa na USM Alger wanaoitenganisha Yanga na ubingwa wa Afrika.

Nionavyo mimi Yanga wanaweza na mara nyingi wameonyesha uwezo wa kufanya jambo sahihi panapotakiwa hata wakipita katika mazingira magumu,muhimu kila mhusika atimize wajibu wake.

Columnist: Mwanaspoti