Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga ilikuwa sawa kwa Mukoko Tonombe?

Mukoko.png?fit=735%2C424&ssl=1 Mukoko Tonombe

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama kuna kosa kubwa ambalo Yanga wamefanya katika miaka miwili ya hivi karibuni kwenye usajili basi ni kuwaacha Mukoko Tonombe na Said Ntibazonkiza. Mukoko aliondoka Yanga akiwa mchezaji bora ndani ya kikosi. Saido aliondoka Yanga akiwa Mchezaji bora pengine namba mbili ndani ya timu nyuma ya Fiston Mayele.

Kwa timu ambayo inajengwa haikupaswa kuwaacha watu hawa. Kwa sababu ya uwepo wa Feisal Salum 'Fei Toto' na ujio wa Aziz KI unaweza kujifariji kuwa walau pengo kubwa la Saido halionekani. Kama kuna kitu ambacho bado kinawatesa Yanga hadi leo basi ni kuondoka kwa Mukoko.

Yanga bado hawajapata dawa ya Mukoko kwenye eneo la kiungo la timu. Baada ya kumleta Yannick Bangala kidogo timu ilionekana kuimarika. Bangala kafanya kazi kubwa ya kuunganisha timu. Kawafanya washambuliaji kuwa na amani kwa sababu yuko nyuma yao. Kawafanya walinzi kuwa na amani kwa sababu yuko mbele yao.

Lakini, baada ya kuanza kutumika na hasa kwenye mechi dume kama mlinzi wa kati, pengo la Mukoko limerudi palepale. Hapa lazima Yanga wakubali tu kuwa yalifanyika makosa kumuacha kiungo aina ya Mukoko. Wachezaji wa aina hii hawakupaswa kuachwa bila sababu za msingi za kiufundi.

Nimeona ujio wa Mudathir Yahya pale Jangwani. Ni mchezaji mzuri. Ana nguvu. Ana kasi. Anakaba na msambazaji mzuri wa mipira pale kati. Atawasaidia sana. Ni eneo lilelile ambalo alikuwa anacheza Mukoko. Ni eneo lile ambalo halijawahi kuzibwa vizuri tangu aondoke.

Hapa Yanga walichemka sana kumuacha mchezaji wao bora kwenye idara ya kiungo. Mpira wa miguu unabadilika kila siku, lakini wachezaji bora kwenye timu bora huwa hawaondoki kirahisi. Wapo aina ya wachezaji ni ngumu sana kuziba nafasi zao labla kwa kuwarudisha wenyewe. Unadhani ni muda sahihi wa kumrudisha Mukoko Jangwani? Sina hakika. Sijui yuko wapi. Sijui ana hali gani.

Kumrudisha mchezaji wa aina hii ni kucheza kamari mpya mjini. Ni bora kusonga mbele na Mudathir ambaye unajua alikuwa wapi. Ni bora kusonga mbele na Mudathir kwa sababu unajua alikuwa kwenye hali gani. Ni uamuzi mgumu kidogo. Lakini viongozi wa Yanga lazima wakubali kuwa kumuachia Saido na Mukoko ni moja ya makosa ya kiufundi waliyofanya siku za hivi karibuni kwenye ujenzi wa kikosi cha ushindani.

Mukoko angecheza kwenye mzunguko wa Fei Toto na Khalid Aucho Yanga ingekuwa bora sana. Aucho ni bora sana kwenye kupiga pasi zenye macho. Fei ni mzuri sana kwenye kusukuma mashambulizi mbele. Mukoko ni mzuri sana kwenye kuleta uwiano mzuri wa timu. Atakaba sana wakati timu inashambuliwa.

Atasukuma sana mipira mbele wakati timu inamiliki mpira. Bado Yanga wanapambana kujaza nafasi ya mwamba huyu. Baada ya kufuzu kucheza makundi Kombe la Shirikisho Afrika watu kama kina Mukoko ni lazima wakujie tu akilini. Hatua ya makundi unahitaji ukamilifu karibu kila eneo.

Watu wanakuja wamejiandaa anayefanya makosa machache uwanjani ndiye yuko kwenye uwezekano mkubwa wa kushinda mechi. Unahitaji watu waliokamilika zaidi uwanjani kama Mukoko. Mudathir ni suala la muda tu anaweza kuwa usajili mzuri sana kipindi hiki. Anahitaji kuzoea kidogo ndani ya timu.

Uzoefu wake wa mechi za kimataifa akiwa mchezaji wa Taifa Stars unaweza kumsaidia sana kwenye mechi za makundi akiwa na Yanga. Huko Afrika ukionyesha udhaifu eneo moja tu wahuni hawakuachi. Utapigwa kama ngoma. Huko Afrika sio sehemu ya kwenda kupata uzoefu. Ni mashindano ya timu bora za Afrika. Watu hawana utani watu wako kazini.

Yanga imeendelea kuwa bora miaka mitatu ya hivi karibuni. Ngoja tuone mwendelezo wa ubora wao. Ni hatua nzuri kwenda makundi Afrika. Ni hatua nzuri kuendelea kuongoza Ligi Kuu Bara, lakini tabia ya kuachana na wachezaji wako bora kikosini kuna namna inawarudisha nyuma.

Mtu kama Mukoko na Saido walipaswa kuwa sehemu ya kikosi hiki. Kwa ubora wao na uzoefu kuna kitu cha tofauti wangeongeza kwenye timu. Huwezi kuwalaumu Yanga kuondoka sana kwa Bernard Morrison na hata ikitokea Fei anaondoka, lakini kwa Mukoko na Saido lazima wasiwe na sababu ambazo haziepukiki.

Wananchi wana matarajio makubwa kwenye timu yao. Wananchi wanataka kuona timu inatetea ubingwa wa ndani na kuvuka hatua ya makundi Afrika. Kazi ya kuyafanikisha mambo haya yote mawili sio rahisi. Unahitaji vidume hasa kwenye timu.

Unahitaji wanajeshi hasa wa kupambana bila kuchoka. Uamuzi wa kumuacha Mukoko na Saido haujawahi kutibiwa ndani ya timu yenu. Huenda Mudathir atapunguza machungu kwa Mukoko. Huenda Aziz KI akapunguza machungu ya Saido. Nani atapunguza machungu ya Fei Toto? Nimekaa paleeee!

Columnist: Mwanaspoti