Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga ifanye ya Kagame 1993

IMG 4174.jpeg Yanga ifanye ya Kagame 1993

Sun, 28 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Historia inakwenda kuandikwa leo Jumapili pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Klabu ya Yanga leo Jumapili inaanza kucheza fainali yake ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi USM Alger ya Algeria.

Fainali ya pili itachezwa Juni 3 Algeria, jijini Algiers ambapo mshindi wa jumla atakabidhiwa taji la ubingwa huo.

Mara nyingi timu zetu ni nadra sana kufika katika hatua kama hizi. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1993 ambapo Simba Sports Club ilifika hatua kama hii wakati wa Kombe la CAF (lililounganishwa na Kombe la Washindi na kuzaa Kombe la Shirikisho Afrika).

SIMBA ILIFELI WAPI?

Timu kama Yanga inapofikia hatua kama hii lazima tuangalie historia ya nyuma inasemaje. Tuangalie makosa ambayo yalifanyika na ikiwezekana tuweze kuyaepuka ili timu yetu ibebe taji la Afrika. Kumbuka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ni Gor Mahia tu ndio iliyobeba taji kubwa la Afrika, miaka 36 iliyopita pale ilipotwaa Kombe la Washindi Afrika.

Katika mchezo wa fainali Gor Mahia ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Esperance Sportive de Tunis jijini Nairobi na ilipoenda Tunisia ikapate sare ya mabao 2-2.

Baada ya hapo ni Sports Club Villa ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1992, katika mchezo wa kwanza ilitoka sare tasa uwanjani Nakivubo mchezo wa pili kufungwa ugenini maboao 2-0 na Shooting Stars na Nigeria.

Ndipo mwaka 1993, Simba ilipofika fainali dhidi ya Stella Abdjan. Simba ilikuwa na mazingira mazuri ya kubeba taji lakini ikafeli. Kwanza ilianza mchezo wa kwanza ugenini na kutoka sare tasa, kisha ikaja kuchapwa 2-0 nyumbani.

AHADI NYINGI SANA

Kwa mujibu wa watu waliokuwa karibu na timu, inadaiwa wachezaji wa Simba walikuwa hawakuwa na utulivu kambini. Viongozi walikuwa wakipishana kutaka kuzungumza na wachezaji huku kila mmoja wao akitoa ahadi yake.

Ilifika hatua wachezaji walipokuwa wamepumzika waliamshwa ili viongozi hao watangaze ahadi zao. Hata wachezaji waliamini wanakwenda kuandika historia kubwa baada ya kufanya vizuri ugenini. Wachezaji waliamini walikuwa ni kama wameshapata ahadi iliyotolewa na aliyekuwa mfadhili wa timu hiyo, Azim Dewji ya Toyota KIA.

Wengi wao walikuwa wakifikiria jinsi ya kuyatumia magari hayo na wengine wakianza kutafuta wateja wa kuwauzia.

Kingine ambacho kilichangia Simba kupoteza mchezo huo ni mambo ya ndumba na ngai. Kuamini katika mambo ya nje ya uwanja na kusahau ufundi na ujuzi. AHADI YA TV MWAKA 1993

Hapa ndipo ilitakiwa Yanga wajifunze jinsi walivyoweza kubeba taji la Kombe la Kagame Uganda ndani ya Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala.

YANGA ILIKUWA HOI

Wakati wanakwenda Uganda, Yanga ilikuwa imekimbiwa na wafadhili wake wakiongozwa na mfadhili Mkuu, Abbas Gulamali.

Wafadhili wengine walikuwa ni Murtaza Dewji, Muhsin Hassanali, Mohamed Virani ‘Babu’ na Ramesh Patwa. Wakati mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, Simba wakipanda ndege, Yanga ilipanda treni hadi Mwanza na kusafiri kwa meli hadi Jinja walikopanda basi hadi Kampala, kwa msaada wa mfanyabiashara, Reginald Mengi.

Wakati Yanga ikifika Uganda, Gulamali akiwa Afrika Kusini kwenye mkutano wa mawakala wa Leyland Daff, alinukuliwa akisema ni Simba ambayo ingeweza kuleta taji hilo nchini.

Kama haitoshi mfadhali huyo ambaye kwa sasa ni marehemu akaongeza laiti kama Yanga ingeleta kombe la hilo basi angetoa TV kwa kila mchezaji.

NINI KILITOKEA

Katika Kundi A Yanga ilikuwa na SC Villa na Malindi. Mechi ya kwanza ilishinda dhidi Malindi mabao 2-1na kufungwa na SC Villa 3-1. Nusu fainali Yanga ikaifunga Express ya Uganda mabao 3-1 na kutinga fainali.

Unaambiwa baada ya kipigo dhidi ya Villa timu hiyo ikahama kambi na kurudi nyuma ya jiji la Kampala ili kujihami zaidi. Na baada ya hapo mechi zote zilizofuata Yanga ikashinda. Baada ya kuingia fainali dhidi ya SC Villa, Gulamali akaenda Uganda kuongeza nguvu kambini.

NZOISABA AMZUIA

Hata hivyo, jitihada za mfadhili huyo kutaka kuingia kambini ziligonga mwamba baada ya Kocha wa Yanga Nzoysaba Tauzany kumzuia kuingia kambini.

Inadaiwa kocha huyo alimwambia Gulamali subiri kutimiza ahadi yako Yanga ikashinda mabao 2-1 na kubeba taji hilo. Na Gulamali akatimiza ahadi yake. Tafsiri ya kumbukumbu hii ni kama Yanga ilijipanga vizuri kisaikolojia na ufundi wa Kocha Nasrudinne Nabi basi wanaweza kuandika historia.

Lakini kama iliwasumbua wachezaji kwa kuwapelekea waheshimiwa wengi kambini wa kutoa ahadi na kuamini mambo ya nje ya uwanja tuandike maumivu.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: