Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga hawataki faida ya mapato ya klabu? - Mdau

Yanga Mkutano Mkutano Mkuu wa Yanga

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumamosi tarehe 24 Juni 2023, klabu ya soka ya Yanga (Young Africans Sports Club) imefanya mkutano wake mkuu wa mwaka katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Miongoni mwa mambo yaliyogusa vichwa vya watu wengi ni takwimu za mapato na matumizi ambayo klabu hiyo imeyapata kwa msimu wa 2022/2023.

Kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said inaonesha kuwa klabu hiyo iliingiza jumla ya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 17.8 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 17.3 katika ligi, FA na mashindano ya kimataifa.

Kutokana na matumizi hayo, klabu ya Yanga inaelezwa kubakiwa na kiasi cha shilingi milioni 581 kama faida.

Baadhi ya wanayanga wamekuwa wakihoji na kushangaa matumizi hayo ya fedha.

Kimsingi, kwanza wanayanga hawa walipaswa kuushukuru uongozi wa klabu yao kwa kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato badala ya kushangaa matumizi.

Nadhani walipaswa washukuru kwamba, uongozi wa Yanga umejitahidi kuwa uongozi wenye uwazi (transparency) kwenye mapato na hata mikataba mbalimbali ambayo klabu imeingia.

Ikumbukwe kuwa, hata Rais wa heshima wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji (Mo) alipata kusema wakati fulani kuwa suala la kuendesha klabu ni gumu na limekuwa likimtia hasara sana.

Nadhani haya yamedhihirika kwenye hesabu za mapato na matumizi za klabu ya Yanga.

Hivyo basi, badala ya baadhi ya wanayanga kutilia shaka hesabu hizo wanapaswa wafikiri namna gani ya kuweza kuisaidia klabu yao ili iweze kupata faida kubwa zaidi.

Ni dhahiri kuwa, kwa umri ambao Yanga inao ni aibu kutokuwa miongoni mwa vilabu tajiri barani Afrika.

Ni aibu kuona wakati huu wa usajili tukisikia baadhi ya wachezaji wanahisiwa kutaka kuondoka.

Na itakuwa aibu zaidi kama wanayanga wanaendelea kubakia kuwa watu wa kuuza maneno tu pasina kuchukua hatua. Ni aibu kwa kweli!

Kwa bahati mbaya sana, wanayanga wengi hawana mapenzi na Yanga tofauti na wanavyojinasibu mitaani.

Najua hili litawakera wengi lakini huo ndiyo ukweli.

Ukweli ni kwamba huwezi kuwa mwanayanga mwenye mapenzi ya kweli na Yanga halafu ukaenda kununua jezi feki!

Huwezi kuwa mwanayanga kindakindaki na huna kadi ya uanachama ya Yanga!

Huwezi kuwa mwanayanga damu na huku huendi uwanjani kuisapoti klabu yako!

Huwezi kuwa mwanayanga na hununui hata bidhaa yoyote ya klabu. Wewe si mwanayanga!

Ikiwa hayo yote hufanyi au mojawapo kati ya hayo, unapataje nguvu za kulalamika klabu kuingiza faida ya milioni 500?

Hivi hamuoni aibu kwamba licha ya kutajwa kuwa ni klabu yenye washabiki wengi nchini lakini wanachama hawazidi hata laki moja?

Hamuoni aibu kweli kwamba licha ya kujinasibu kote kuwa mpo wengu lakini mpaka sasa wanachama waliosajiliwa ni takribani elfu hamsini tu!!! Hii ni aibu!

Kwa klabu ambayo tunaelezwa kuwa ina mashabiki takribani milioni 3, 4 hadi 5 nchi nzima tulitarajia walau basi wanayanga milioni 1 wangekuwa wamejisajili kidijitali, lakini badala yake mpaka sasa hawazidi elfu hamsini. Bado mnamtafuta mchawi wenu wakati wachawi ni ninyi wenyewe!?

Mnajua kuwa mngekuwa mmejisajili angalau wanayanga milioni moja tu, klabu ingiengiza mapato ya kiasi gani?

Ni kwamba Yanga ingeweza kuingiza takribani bilioni 29 kutoka kwa wanachama.

Je kwa kiasi hicho mngeshindwa kuwa miongoni mwa vilabu tajiri Afrika?

Hivyo basi, kama kweli hamtaki kupata faida ya milioni 500, yawapasa kubadilika sasa!

Jisajilini sasa kupitia CRDB, NBC na NMB ili muweze kuondokana na haya mashaka ya kubaki na faida ya milioni 500, vinginevyo wachawi wa mafanikio ya Yanga mtakuwa ninyi wenyewe wanayanga.

Asanteni.

Columnist: www.tanzaniaweb.live