Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga, Nabi ilikuwa lazima, muda uliruhusu

Nabi Na Rais Hersi Said Nasreddine Nabi na Injinia Hersi

Sat, 24 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwanza nina mkataba na Porto, pili nina ofa kutoka klabu mbalimbali ambazo itabidi niziangalie kisha nifanye maamuzi. Napenda kuondoka Porto. Nitamweka wazi rais wangu wa klabu ili niweke sawa mustakabali wa taaluma yangu."

Hayo yalikuwa ni maneno ya Jose Mario dos Santos Mourinho Felix wakati akiwa Kocha Mkuu wa Porto ya Ureno aliyotatoa kwenye mkesha wa fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, mnamo Mei 2004 kati ya timu hiyo dhidi ya Monaco ya Ufaransa iliyokuwa chini ya nahodha wa zamani wa Ufaransa Didier Deschamps.

Mourinho alianza kuifundisha timu hiyo ya nchini kwao mwaka 2002 na katika miaka miwili akafanikiwa kuipa Kombe la Uefa, Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na ubingwa mara mbili wa Ligi Kuu ya Ureno ambayo ndiko nyumbani kwa kocha huyo mwenye maneno mengi.

Kama alivyoahidi, baada ya Porto kuchukua ubingwa dhidi ya Monaco, Mourinho aliondoka timu hiyo na kwenda kujiunga na Chelsea ya London, England iliyokuwa na mmiliki mpya mwenye fedha nyingi Mrusi Roman Abramovic.Y aliyofuata baada ya hapo ni historia.

Nimekumbuka hadithi ya Mourinho 'The Special One' kufuatia maoni na malalamiko ya wapenzi wa soka hasa wale wa Yanga baada ya timu hiyo kuachana na kocha Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyeitumikia kwa mafanikio klabu hiyo tangu Aprili 2021.

Katika misimu yake miwili pale Jangwani, Nabi ameipa yanga ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC) mara mbili mfululizo na kilele cha mafanikio kikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF Confederation Cup) ambako ilifungwa na USM Alger ya Algeria kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mikondo miwili ya fainali.

Kwa klabu ya Yanga hayo yalikuwa ni mafanikio ambayo hawajawahi kuyafikia na kwa kweli ni klabu pekee isiyotokea taifa la kiarabu iliyoweza kufika fainali za Afrika msimu huu.

Katika taarifa yake ya baadae, Nabi aliweka wazi kwamba aliutaarifu uongozi wa Yanga asingeingia kandarasi mpya baada ya kufuzu hatua ya makundi.

Kama kwa Mourinho au kwa kocha yeyote wa kizazi hiki alijua wakati muafaka wa kuondoka ni wakati wa mafanikio. Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema wakati sahihi wa kuondoka jukwaani kwa mcheza ngoma ni wakati bado unapigiwa makofi.

Nabi asingesubiri azomewe ndio aondoke Yanga. Mafanikio aliyoyapata na Yanga yawezekana hata yeye hakuyatarajia. Mafanikio hayo yanampa nguvu ya kukaa mezani kwa kujiamini pindi klabu yoyote itakapohitaji huduma yake.

Kizazi hiki cha viongozi wa soka na hata tuseme kizazi hiki cha wapenzi wa mchezo huo hakina nafasi kwa kina Sir Alex Ferguson ya kukaa na timu miaka 20. Ni kizazi kisicho na uvumilivu na makocha; watawashangilia timu inapofanya vizuri na kuwazomea na kuwazodoa timu inapoyumba kidogo. Wanataka timu isiyofungika na inapofungika basi kocha ndiye hufanywa mbuzi wa kafara.

Ni mazingira magumu ya mazungumzo kwa kocha anayeomba kazi baada ya kufukuzwa kazi ukilinganisha na kocha anayetafutwa baada ya kufanya vizuri.

Kocha aliyefanya vizuri atatafutwa kwa dau kubwa, pia kupata starehe ya kuweka masharti yake kama kuchagua wasaidizi wake; Nabi angetaka nini zaidi ya hapo?

Ni siri iliyo wazi kwamba Yanga walimpa kazi Nabi wakimjaribu uwezo na mwenendo wake. Kama si hivyo, basi kocha huyo aliingia Yanga akijaribu kina cha maji.

Nadharia hizo mbili zinathibitishwa na ukweli kwamba Nabi alitia sahihi mkataba wa kwanza wakati anaingia na mwingine mwaka mmoja baadae. Mikataba miwili katika miaka miwili. Hakuna aliyetegemea ndoa ya kikatoliki kati ya Yanga na Nabi. Kwa mashabiki kama walivyo siku zote, wangependa kocha aendelee kuwepo milele ilimradi anawapa furaha.

Siamini kama uongozi wa Injinia Hersi Said uliweka matumaini yao yote ya mafanikio kwa ‘Profesa Nabi’. Lilikuwa ni suala la kusubiri na kuona kitakachozaliwa.

Yanga wamewahi kuwa na makocha mahiri kama Tambwe Leya na Raoul Shungu kutoka Zaire (Congo DRC), Dk Victor Stanculescu kutoka Romania, Nzoyisaba Tauzan kutoka Burundi na wengineo ambao pamoja na majina yao kuandikwa katika vitabu vya historia ya klabu, lakini wakati ulipofika kila mmoja alifunga vilivyo vyake na kuondoka.

Tofauti pekee ya Nabi na waliotangulia ni kiwango cha mafanikio alichokipata hasa kwa kucheza fainali ya Afrika. Hata huyo anayekuja wakati ukifika ataondoka.

Kwa klabu, mafanikio ya Nabi yanaweza kuwa chambo cha kuvutia makocha wazuri. Mafanikio ya Nabi na Yanga yanapeleka taswira ya klabu yenye malengo ya kufanikiwa. Sidhani kwa sasa kama Injinia Hersi kama Rais wa klabu atapata ugumu wa kuleta kocha mzuri, kwani mafanikio ya klabu yapo na yanajieleza vya kutosha.

Ni wakati sahihi kwa Yanga kutafuta kocha na kumtwisha majukumu kuanzia alikoishia Nabi, ikiwa ni pamoja na kuhusika katika zoezi zima la usajili wa wachezaji na benchi la ufundi ambalo litahitaji kusukwa upya kwani wengi wameshatangazwa kuondoka.

Katika hali ya kufanana, Nabi ameondoka Yanga lakini bado hajatangazwa rasmi na klabu aliyokuwa na mazungumzo nayo ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku Yanga ikiwa haijatangaza rasmi nani anaenda kuwa mrithi wa Nabi.

Ni suala la muda kujua nani anaenda kuishi na nani baada ya kutamatika kwa ndoa kati ya Yanga na Nasreddine Nabi.

Mwisho wa siku kila upande una cha kuonyesha kama kumbukumbu ya kufanya kazi pamoja japo wakati umewatenganisha.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: