Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yajue maajabu ya pilipili

5787 PILIPILI MBUZI TZW

Thu, 5 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

UNAPOZUNGUMZIA jamii ambayo watu wake wengi wanaaminika kuwa wapenzi wa kula pilipili, bila shaka jibu litakalotoka kwa watu wengi hasa Watanzania ni Wahindi.

Hii imetokana na ukweli kwamba kwenye mlo wa Wahindi pilipili haikosekani. Tunawaona namna wanavyopenda kula pilipili kutokana na kuishi nao, kutazama kwenye filamu zao, tunapokwenda nchini mwao au kusikia kwa wale walio karibu nao. Wenzetu hawa hadi kwenye vyakula vyenye sukari wao wanaweka pilipili kama pipi na jamu na hata unapokwenda nchini mwao chakula kinachotambuliwa kwamba hakina pilipili, usidhani kwamba hakuna kabisa, bali huwa nayo angalau kidogo. PILIPILI NA IMANI ZA WAHINDU Kutokana na imani, Wahindi wengi hutumia pilipili kuzuia miungu wa mikosi kuingia ndani ya nyumba au kwenye sehemu ya biashara kama duka na hivyo si ajabu kuona mlangoni pamening’inizwa pilipili saba pamoja na ndimu.

Mkazi wa Upanga, Dar es Salaam, Ajay Prakash anasema: “Mungu Alakshmi tunaamini sisi Wahindu kuwa analeta mikosi dukani hivyo nimening’iniza pilipili saba na ndimu kwani yeye anazipenda hivyo akija atakula, ataondoka na hataingia dukani kwangu kuleta mikosi.” Prakash anasema kwa mujibu wa imani za Wahindu, Alakshmi anapenda vitu vichachu, vichungu na vikali hivyo akifika mlangoni akala vyakula vyake hivyo anavyopenda huondoka. Hata hivyo, anabainisha kuwa uzi unaotumika kuning’inizia pilipili na ndimu kisayansi unanyonya asidi kutoka kwenye matunda, hii inawafanya wadudu kukimbia na kutoingia kwenye nyumba, dukani au sehemu yoyote kutakaponing’inizwa pilipili na ndimu.

KUKIMBIZA WANYAMA SHAMNBANI

Mbali na mikosi, pilipili inatumika pia kukimbiza wanyama waharibifu kama tembo. Wanyama hawa wamekuwa wakiharibu mazao ya wakulima, makazi na hata kuua watu barani Afrika na Asia na mateso hayo yamewafanya wakulima watumie pilipili kuwafukuza. Wataalamu wanasema tembo hawapendi kemikali aina ya Capsaicin ambayo ipo ndani ya pilipili na ndiyo inayoifanya iwe kali. Kwa kuwa mfumo wa tembo wa kunusa harufu una nguvu, harufu ya pilipili inawafanya wakose raha na kuwazuia kula mazao, hivyo wakulima wamebuni njia ya kupanda pilipili kuzunguka mazao yao na wanyama hao wanakimbia na kuyaacha mazao yakiwa salama. Hata hivyo ndege hawapati athari na kemikali ya Capsaicin hivyo hawaogopi pilipili, wanaila sana na hii inaathiri wakulima.

MAGONJWA YA NGOZI

Mbali na faida hiyo, pilipili inayochukua miezi miwili hadi minne kuvunwa inatumika kutengeneza dawa za magonjwa ya ngozi hasa yale ya muwasho pamoja na mafua. Kemikali ya Capsaicin inasaidia kuondoa muwasho na kuifanya ngozi iwe nzuri. KUTIBU SARATANI Kemikali hiyo hiyo ya Capsaicin imegunduliwa na wanasayansi katika tafiti mbalimbali ilizofanyika kuwa inasaidia kupambana na saratani, kwani inaua chembe hai zinazosababisha saratani. Wanasayansi hao wanasema kemikali hiyo ya Capsaicin inaweza kusaidia katika kupata tiba ya saratani kama utafiti zaidi utafanyika. Aina za saratani ambazo zinaonekana kusaidiwa sana na pilipili ni ya matiti, mifupa, utumbo mpana na kongosho.

Hata hivyo, wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Ruhr cha Bochum, Ujerumani wanasema kemikali ya Capsaicin haifai kuliwa, kuvutwa au kuchomwa kama sindano na watafiti wanadhani inafaa zaidi itumike kama kidonge kinachokwenda sambamba na dawa nyingine zenye lengo la kuuwa chembechembe za saratani. Dk Lea Weber wa chuo hicho kikuu anaandika katika jarida la Breast Cancer - Targets and Therapy kuwa ‘Capsaicin’ inaua chembe hai zinazosababisha kifo, inazuia chembe hai za saratani kuweza kuendelea kukua na chembe hai hizo ni zile zinazosababisha saratani ya mifupa, kongosho na utumbo mpana huku chembe hai za kawaida zikiendelea kuwa salama bila kuathirika. Kadiri chembe za saratani zinavyokufa, uvimbe wa saratani unasita kukua.”

KUUA WADUDU MASHAMBANI

Mtafiti mmoja wa masuala ya kilimo, John Julius Bakari, wakati wa maonesho ya Nanenane miaka miwili iliyopita alikuja na ugunduzi wake wa dawa za asili za kuua wadudu waharibifu wa mazao hususani korosho. Katika dawa hizo kuna mchanganyiko wa pilipili na mazao mengine yenye harufu kali ikiwemo karafuu, vitunguu swaumu, mshubiri pori na magadi. Baadhi ya mashuhuda walisema kwamba dawa hizo zinafanya kazi vizuri kuliko dawa za viwandani. “Unajua, mdudu anayeshambulia mimea unaweza kummaliza kwa njia tatu na hata fomula ya dawa zote ni hiyo.

Mosi, ni kwa njia ya kumgusa. Yaani anapopambana na dawa inayomwasha mwilini basi huepuka eneo hilo na pilipili ama dawa nyingine tunazochanganya huwawasha wadudu wengi ikiwemo minyoo. Pili ni harufu. Mdudu anapokutana na harufu kali katika mmea anaotaka kula basi anapata shida na kuondoka. Njia ya tatu ni ladha, kwamba mdudu anapotafuna ladha isiyo ile inayomvutia kwenye mmea fulani basi huhisi mmea ule siyo chakula chake,” anasema Bakari.

KUONDOA MWASHO WA PILIPILI

Mbali na tiba, pilipili ambayo inatumika sana kwenye mlo wakati mwingine inakuwa kero pindi inapoliwa au inaposhikwa kwa wingi kiasi cha kumfanya mtu kuchanganyikiwa. Hata hivyo, wengi hawafahamu namna nzuri na rahisi ya kuondoa mwasho huo kwenye ngozi au mdomoni. Njia rahisi ya kumaliza mwasho wa pilipili ni kwa kunywa maziwa na si maji. Pia unaweza kunywa mtindi au kula ice cream. Maziwa au mtindi na mafuta yanayopatikana ndani yake yanaondoa kemikali ya Capsaicin hivyo ule ukali unamalizika kwa kipindi kifupi.

Ndani ya maziwa kuna protini inaitwa Casein inayoondoa kabisa Capsaicin. Maji ya nazi au madafu nayo yanasaidia sana kuondoa muwasho na ukali huo mdomoni. Hata hivyo, wengi wanapendelea kunywa maji wakati maji ni ‘sumu’ kubwa kutokana na kwamba ukali wa pilipili ndiyo unasambaa zaidi kwa kuwa Capsaicin inasambazwa kwa haraka zaidi na maji. Soda na kahawa nazo hazisaidii bali huwa kichocheo cha muwasho na ukali. Unaweza kuondoa mwasho na ukali mdomoni baada ya kula pilipili nyingi kwa kupakaa kwenye ulimi mafuta ya zaituni au yoyote ya mboga, kula siagi ya karanga, vyakula vyenye wanga mwingi, matango, ndizi, chokoleti na karoti.

Kwa upande wa ngozi iliyoguswa na pilipili kama mikononi unaweza kuondoa mwasho wake kwa kuosha kwa sabuni, pakaa mchanganyiko wa maji na dawa ya madoa, osha kwa pombe kali kama vodka, mchanganyiko wa baking soda na maji na uache ikauke kisha osha kwa maji safi.

HISTORIA YA PILIPILI

Historia ya pilipili inaonesha kwamba zao hilo lilianza kulimwa na kutumiwa nchini Mexico miaka 3500 iliyopita kabla Kuzaliwa Kristo. Ilienezwa sehemu mbalimbali duniani na Christopher Columbus aliyegundua bara la America mwaka 1493. Takwimu za mwaka 2014 zinabainisha kuwa mwaka huo kulizalishwa tani milioni 32.3 za pilipili huku nusu ya pilipili hizo zikizalishwa nchini China.

Pilipili ina vitamin A, B6 na C. Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala haya kuwa India ndiyo nchi inayomjia kwa haraka kichwani Mtanzania kwa matumizi makubwa ya pilipili lakini zipo nchi nyingine ambazo katika kila mlo ni lazima pilipili iwemo nazo ni pamoja na Mexico, Thailand, China na Bhutan, nchi ambayo inapakana na Tibet na India. Kwa Afrika Wanigeria na Ghana ndio wanaotajwa kutumia pilipili kwa wingi katika vyakula vyao.

Columnist: habarileo.co.tz