Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yafaa kuwekeza, kutambua, kutibu saratani watoto wenye ualbino

ZER.webp Yafaa kuwekeza, kutambua, kutibu saratani watoto wenye ualbino

Tue, 16 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WATOTO wenye ualbino ni miongoni mwa watu wanaopitia changamoto nyingi zikiwamo za kiafya, kunyanyapaliwa kwenye jamii na hata kuuliwa na viungo vyao kuuzwa ili kwa imani kuwa vikitumiwa huleta mafanikio.

Leo, tunapoadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ni vyema kuwatambua wenye ualbino, ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu hali hiyo, kuwathamini na kuwasaidia zaidi.

Ualbino ni kukosa rangi ya asili au melanin kwenye ngozi, nywele na macho. Mwenye ualibino ni sawa na wengine kiutendaji bila kuangalia utofauti wa rangi licha ya kwamba ana uoni hafifu na ngozi inayoathiriwa haraka na mionzi ya jua.

Akizungumza na Nipashe wakati wa Siku ya Kitaifa ya Kuongeza Uelewa wa Ualbino ambayo hufanyika Juni 13 kila mwaka, Ofisa Huduma, Chama cha Watu Wenye Ualbino (TAS), Christina Silas, anasema tunapoadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, kuna mitizamo mingi kuhusu wenye ualbino.

“Wapo wasiojali tofauti ya rangi lakini wengine wanawachukulia wenye ualbino kuwa ni tofauti tena hawafai kushirikishwa katika masuala mbalimbali ya kijamii,” anasema Christina.

Katika kuadhimisha siku hii, anaipongeza serikali kwa kuhakikisha haki ya watoto wenye ualbino kupata elimu inazingatiwa tofauti na zamani.

“Sasa hivi idadi inayoandikishwa shule, imeongezeka kuanzia elimu ya awali na wanaendelea vizuri kama wengine wasio na ualibino tofauti na miaka ya nyuma, wazazi wengi walikuwa wakihofia kuwapeleka shule kuogopa mauaji na ukatili mwingine waliokuwa wakifanyiwa,” Christina anaongeza.

Akizungumzia elimu anasema, serikali inaendelea kujumuisha mahitaji ya wenye ualbino wanapokuwa shuleni mfano vifaa vya kujifunzia na kufundishia na TAS imeona hatua hizi baada ya kufanya utafiti mikoa ya kanda ya ziwa.

Mbali na hilo, kila mwaka serikali inaongeza walimu wa elimu maalumu ambao wanafundisha wanafunzi kulingana na ulemavu ambao huwasaidia wenye ualbino.

KUTIBU SARATANI

Christina anasema saratani ya ngozi ni tatizo kwa wenye ualbino na husababisha vifo kwenye umri mdogo, hivyo TAS, serikali na wadau wengine wamefanikisha kupata vifaa tiba vya saratani ya ngozi katika hospitali za rufani za Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Iringa, Singida, Mara na Unguja.

“Lengo ni kusaidia watoto na watu wazima wenye ualbino kupata ushauri, uchunguzi wa awali pamoja na tiba ya saratani mapema kwenye mikoa yao.”

Pia, kuboresha takwimu na taarifa zote zinazohusu saratani ya ngozi kwa wenye ualbino.

Mwenyekiti wa TAS Wilaya ya Tarime, Joseph Sinde, anasema ingawa Tanzania inashiriki maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, umaskini vijijini unakwamisha wazazi kuwatunza watoto wenye ualbino.

“Umaskini unakwamisha wazazi na walezi kuwapeleka kwenye kliniki kuchunguzwa afya ya ngozi. Wengi wanaotoka vijiji vya mbali kufuata huduma za afya mijini. Kuna wanaotembea kilomita 50, au kulipa nauli ya kati ya Sh 5,000 hadi 10,000 kufikia kituo cha afya.Wengine wanashindwa matokeo yake wanakosa haki ya huduma za afya,” anasema.

Hata hivyo, TAS Tarime inashindwa kuwafikia walio ya mbali ili kuwaelimisha kutunza watoto wenye ualibino, kuchunguza afya mapema, kufahamu saratani ya ngozi na kujikinga kwani hakuna vitendea kazi hasa usafiri na pesa.

Anawakumbusha kuwa kila baada ya miezi mitatu inakuwepo kliniki ya kuchunguza ngozi inayoendeshwa na Shirika la Standing Voice la Mwanza.

WITO WA ELIMU

“Sisi TAS Tarime tunatoa wito kwa serikali iendelee kutoa vipaumbele kwa watoto wenye ualbino kupata elimu ili wajimudu kimaisha kwa sababu asilimia kubwa ya wenye ulbino miaka ya nyuma walikuwa hawapati elimu na kupelekea wengi kuishi maisha ya kuombaomba na utegemezi. Yote yamesababisha unyanyapaa, ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wenye ualbino,”anasema Sinde.

Anaona kuwa wengi wakisoma na kuwa na elimu bora wataajirika au kujiajiri, watasaidia kuchangamana na jamii katika shughuli mbalimbali kama za kiuchumi na kisiasa.

MATIBABU MUHIMU

Sinde anataja changamoto ya upatikanaji wa mafuta kinga ya kuzuia mionzi ya jua kwa watoto wanaotoka kwenye kaya masikini kuwa ni hitaji la lazima kwa sasa.

“Upatikanaji wa mafuta haya ni shida sana ingawa tunapata kwa uchache kutoka serikalini na baadhi ya wadau wengine. Familia nyingi zilizo na watoto wenye ualbino haziwezi kununua vifaa vya kujikinga na mionzi ya jua kama vile miwani, kofia na mafuta,” anasema.

Mafuta kinga yanauzwa ghali na asilimia kubwa ya wazazi kwenye familia maskini hawawezi kumudu na hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa watoto kupata kansa ya ngozi.

Katibu Mkuu wa TAS, Mussa Kabimba, akizungumzia uchunguzi na tiba ya saratani ya ngozi kwenye mikoa iliyopewa vifaa vya uchunguzi anasema, kufikia Juni 4 mwaka huu, wenye ualbino waliochunguzwa ni 1,501.

Kati ya hao 873 walikuwa wameungua na jua, 437 hawakuwa na tatizo, 235 walipatiwa tiba ya dalili za saratani ya ngozi na 68 walipewa rufaa kwa ajili ya msaada zaidi.

“Chama kinapenda kuufahamisha umma kuwa mauaji pamoja na vitendo vya kikatili vilivyokuwa vinawakabili wenye ualbino wakiwamo watoto havihusiani na masuala ya uchaguzi wa tiba. Hivyo wanaomba watu waache kupotosha jamii kwamba watu wenye ualbino wapo hatarini kwa sababu huu ni mwaka wa uchaguzi.”

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kulisimamia hili na mpaka sasa tunaona na kushuhudia watu wenye ualbino wanashirikishwa na kujumuishwa kwenye mambo mbalimbali hivyo kujenga uelewa na kuondoa imani potofu iliyokuwa inasababisha kundi hili kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwamo unyanyapaa,” anasema

Columnist: www.tanzaniaweb.live