Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Xavi, ghafla ukuta umekutana na ukuta

Xavi Hernandez Goal Xavi, ghafla ukuta umekutana na ukuta

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Neno maarufu zaidi wakati huo lilikuwa ‘tena’. Na lilipotamkwa kwa Kiingereza lilitukosha wengi. Again. Raha iliyoje kusikia namna Xavi Hernandez alivyokuwa akituletea neno ‘again’. “It’s Xavi to Messi, to Xavi again.”

Wachezaji wenzake walimgeuza kuwa ukuta. Kama vile kijana aliyekuwa hana mtu wa kucheza naye akachukua mpira wake na kwenda ukutani. Anaugongesha mpira katika ukuta kisha unamrudia. Hii ndio ilikuwa kazi ya Xavi katika kikosi cha Barcelona. Alikuwa alama ya soka la Barcelona ile ya Pep Guardiola.

Angeweza kupiga pasi hata 200 peke yake. Alichofanya kilikuwa rahisi tu. Anakupa mpira anasogea kando unampa tena anatafuta mtu mwingine wa kumpa. Mpira unakuwa rahisi na Barcelona wanaendelea kuwa nao kwa muda mrefu wa mchezo huku wapinzani wakisaka vivuli.

Barcelona ile na kisha timu ya taifa ya Hispania msingi wao ulikuwa Xavi Hernandez. Barcelona wakatwaa mataji lukuki halafu Hispania wakatwaa kombe la dunia na Euro. Xavi ndiye aliyekuwa alama na kielelezo cha soka lenyewe. Aliuvumbua mpira mpya ambao unatamba hadi sasa.

Wakati kina Zinedine Zidane, Ronaldinho, Andre Pirlo na wengineo wakisifika kwa kanzu, tobo na chenga za madaha, Xavi alisifika kwa pasi nyingi uwanjani. Pasi ambazo zilirahisisha mambo uwanjani. Zamani tulikuwa tunachukulia kawaida lakini sasa hivi katika dunia ya takwimu na data Xavi ameendelea kusimama kama alama ya namna ambavyo kiungo wa soka anatakiwa kuwa.

Baadae nyakati zilimpita. Alijikuta akiangukia Qatar kumalizia soka lake. Ndiyo, pesa nyingi soka kidogo. Ukweli usiopingika. Baada ya kutamba kidogo aliamua kutundika daluga na kwenda katika kazi ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa kazi ngumu duniani. Ukocha. Alianzia kazi hii katika ardhi ya Waarabu halafu Barcelona wakamrudisha nyumbani.

Katika msimu wake wa kwanza Xavi alitwaa La Liga na kombe la mfalme. Kwa tunaoifahamu La Liga ukweli ni Xavi alitwaa taji hilo kutokana na kuanguka kwa soka la Hispania kwa sasa. Sio kwamba Barcelona ilirudi katika ubora wake kama ilivyokuwa katika zama zake. Hapana. Wapinzani wao wakiongozwa na Real Madrid walikuwa wachovu zaidi.

Msimu huu Barcelona imedorora. Tupo Machi lakini tayari wameshaachwa pointi 10 na viongozi wa ligi ambao ni wapinzani wao wakuu katika soka la Hispania. Kama vile haitoshi mwanzoni mwa wiki hii, Xavi ametangaza kuachana rasmi na kikosini cha Barcelona mwishoni mwa msimu huku akimlaumu kila mtu kuwa mbaya.

Huu ni mwisho wa ndoa. Nimekumbuka mambo mengi. Cha kwanza ni namna ambavyo Pep Guardiola ametuletea makocha wengi katika soka la kisasa lakini kumrithi sio kazi nyepesi. Akina Vicent Kompany wote wanasuasua kurithi akili yake. Mikel Arteta anajaribu kwa mbali.

Najua Pep ndiye mtu ambaye karibu kila kocha anajaribu kumuiga. Hata hivyo, Pep anaonekana kuwa maji marefu kufuata nyayo zake. Naweza kukuhesabia makocha wengi wanamuona Pep kama shujaa wao. Ni hawa kina Mikel Arteta na wengineo. Hata makocha wengi wa Kiingereza ambao walitawala soka la Kiingereza kwa sasa wamerudi nyuma.

Lakini kuondoka kwa Xavi kumenikumbusha namna ambavyo wakati mwingine hadithi nzuri huwa inaishia sehemu mbovu. Wakati mwingine bora uendelee kuota ndoto tu. Kwamba ulikuwa mchezaji mahiri wa klabu hiyo. Baada ya hapo funga milango. Wengi wamejaribu kuwa mashujaa katika kazi mpya wa ukocha kama walivyokuwa mashujaa wakati wanacheza. Ilishindikana.

Mfano wa karibu ni Frank Lampard na Chelsea yake. Alionekana kuwa shujaa haswa baada ya kuibuka kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu yao akaamua kurudi klabuni hapo kama kocha akaambulia aibu. Namna walivyomweka moyoni halafu akaibuka katika kazi ya ukocha mara mbili kisha mara zote akatimuliwa...inatia huzuni.

Mwingine ni Ole Gunnar Solskjaer. Namna alivyokuwa shujaa wa Manchester enzi hizo. Halafu baadaye akapewa ukocha ambao ulimwacha akiwa mtu aliyedharaulika klabuni. Hakuwa na namna zaidi ya kupunga mkono na kuondoka zake kwa kasi ya ajabu. Mifano hii ni mingi kwa wapenzi wawili.

Kitu kingine nilichojifunza kwa Xabi ni namna ambavyo sio lazima mchezaji mzuri awe kocha mzuri. Nimewatazama wote Xavi pamoja na Guardiola wakicheza soka ukweli ni Xavi alikuwa na kipaji kikubwa. Lakini je, leo unajua wamepoishia? Guardiola amekuwa kocha bora wakati Xavi akisuasua.

Sasa Xavi ambaye uwanjani alionekana kuwa ukuta enzi zake wakati anacheza sasa amekutana na ukuta wa ukweli. Nyakati zimefika mwisho kwake Barcelona na anaondoka kinyonge, huku mashabiki wa timu yake wakimzomea katika viunga mbalimbali vya Camp Nou.

Nadhani huu ni mwisho wa enzi kwake. Sijui kama atarudi timu kubwa, lakini kwa sasa anaonekana hana jipya katika kazi yake. Mashabiki walimsubiri kwa hamu aliporejea wakiamini kama yeye alikuwa mwanafunzi mtiifu kwa Pep Guardiola basi angeweza kuwa kama yeye katika kazi ya mpira. Inaonekana haitawezekana.

Amegonga ukuta baada ya muda mrefu kugeuzwa ukuta na wenzake pale Barcelona. Angetamani iwe ndoto njema kama ilivyokuwa kwa mkongwe wa zamani wa Barcelona, Joan cruyff ambaye alipata mafanikio makubwa kama kocha na mchezaji pale Barcelona. Ni kama ilivyo kwa Guardiola tu. Lakini sasa inaonekana yupo chali.

Columnist: Mwanaspoti