Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wizara ya Afya izingatie agizo la Rais

07be3665713c6f0e44d1fbaf76fb187d Wizara ya Afya izingatie agizo la Rais

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA hotuba yake wakati akizindua shamba la miti wilayani Chato, mkoa wa Geita juzi, Rais John Magufuli aliiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufanya utafiti kwanza na kujiridhisha kuhusu chanjo mbalimbali zinazoingizwa nchini kabla ya kutumika kwa wananchi.

Hatua hiyo imetokana na kubainika kuna baadhi ya wananchi wanakwenda ughaibuni kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yasiyoeleweka wakidhani kuwa watabaki kuwa salama dhidi ya magonjwa hayo.

Matokeo yake wamekuwa ndio chanzo cha wao kuleta magonjwa hayo yasiyoeleweka nchini na kusababisha wananchi wengi kuishi kwa mashaka baada ya magonjwa hayo kusambaa nchini na kuleta taharuki.

Awali, mwaka jana wakati wimbi la ugonjwa wa corona duniani likiwa limetamalaki hususani hapa nchini, Rais Magufuli aliwahi kutoa agizo kwa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kutekeleza majukumu yao kwa kutafiti kirusi cha ugonjwa huo na hatimaye taasisi hiyo kuja na dawa ya Nimrcaf ambayo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kupunguza makali ya magonjwa hayo yasiyoeleweka ikiwamo corona.

Aidha, alikitaka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambacho kimepekewa jukumu la kuzalisha wataalamu wa magonjwa mbalimbali pamoja na kutafiti tiba na dawa mbalimbali za binadamu, kuisaidia serikali kufanya utafiti wa magonjwa hayo ya ajabu nchini.

Endapo taasisi hizi mbili pamoja na nyingine zenye jukumu la aina hii zingetekeleza majukumu yao kwa dhati, ingewezekana kabisa kuiweka nchi hii na wananchi wake kutokuishi kwa taharuki na wasiwasi juu ya magonjwa haya yasiyoeleweka, hali iliyosababisha Rais Magufuli katika hituba yake ya juzi kutoa tena agizo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kujiridhisha na chanjo mbalimbali zinazoletwa nchini kwa ajili ya wananchi.

Tumsaidie Rais Magufuli na serikali kwa ujumla. Yeye peke yake hawezi kutekeleza majukumu haya bila ya msaada wa taasisi zenye jukumu la kuhakikisha nchi inaondokana na taharuki hizi kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Taasisi hizi, mathalani MUHAS ambayo inazalisha wataalamu wa magonjwa mbalimbali na tiba za kibinadamu kila mwaka, zisaidie nchi hii kuja na majibu ya magonjwa yasiyoeleweka.

Halikadhalika, NIMR imsaidie Rais Magufuli na serikali yake kutafiti magonjwa haya yasiyoeleweka kwa kuja na majibu ya uhakika kuhusu kinga na dawa badala ya kuyaachia mataifa makubwa duniani kuipangia nchi aina ya chanjo za kutumia kwa wananchi wake.

Haiwezekani nchi hii ambayo imekuwa na utamaduni mzuri wa wananchi wake kuishi kwa amani na usalama tangu enzi na enzi na bila ya hofu yoyote, leo hii iingie katika mkumbo wa nchi nyingine Afrika na duniani wa kuishi maisha ya taharuki.

Taasisi zilizopewa jukumu la kuwafunda wataalamu wa magonjwa ya kibinadamu na zile za kutafiti dawa zimsaidie Rais John Magufuli na serikali kwa ujumla kutafuta majibu ya magonjwa haya yasiyoeleweka kwa ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla ili nchi ifikie malengo yake ya maendeleo iliyojiwekea.

Columnist: habarileo.co.tz