Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wenye nyumba za kupanga washiriki  kukuza pato la taifa

F83e1c3581fd87c438d91ae0d428e61b Wenye nyumba za kupanga washiriki  kukuza pato la taifa

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UCHUNGUZI wangu usio rasmi umebaini kuwa, miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa ambao hawajafikiwa na mamlaka husika ili wachangie ukuzaji wa pato la taifa, ni wamiliki wa nyumba wanaofanya biashara ya kupangisha.

Si siri kuwa wengi wa wamiliki hawa kama si wote, ni kama vile biashara yao ya kupangisha nyumba au vyumba imepewa msamaha wa kodi jambo ambalo kimsingi, si kweli wala si jema.

Kimsingi, wapo wenye nyumba wanaopangisha watu kwa ajili ya makazi, na wenye nyumba wanaopangisha watu wanaofanya biashara.

Karibu wote hawa, hawalipi kodi ya mapoato kutokana na biashara zao za kupangisha, bali wanacholipa kila mwaka ni kodi ya majengo labda na kodi ya pango la ardhi.

Mamlaka husika zinaweza kuchukua mfano wa mtu mwenye nyumba ya vyumba kumi vya kupanga na kila kimoja kinalipiwa mathalani wastani wa Sh 40,000 kwa mwezi (Sh 480,000 kwa mwaka) kwa kila chumba sawa na Sh 4,800,000 kwa vyumba vyote kwa mwaka.

Kama mfanya biashara huyo hafikiwi ili alipe kodi ya biashara yake, lakini ‘mmachinga,’ analipia kitambulisho cha Sh 20,000, wakusanya kodi hawalitendei haki taifa na juhudi za Rais John Magufuli kuimarisha uchumi na pato la taifa zitakuwa zinahujumiwa na aliowaamini.

Wapo pia wenye nyumba mbili au zaidi katika moja. Mathalani hiyo iwe ni ya kuishi familia mbili.

Kutegemea hali na ukubwa wa nyumba, wanatoza kuanzia Sh 3,000,000 na kuendelea kwa mwaka.

Hivyo, huyo aliyepangisha familia mbili anapata Sh 6,000,000 kwa mwaka, lakini analipa kodi ya jengo na pango la ardhi; halipii hiyo ya biashara, hii si sahihi.

Katika mitaa ya mjini vilipo vyumba vya biashara maarufu fremu, wamiliki wengi wa nyumba wanalipa kodi ya jengo na pango la ardhi; hawalipii kodi ya biashara yao ya upangaji na badala yake, wanaolipa kodi kutokana na biashara zao, ni wale wapangaji ambao kila mmoja ana biashara yake yakiwamo maduka.

Maeneo hayo fremu moja hupangishwa kwa wastani wa si chini ya Sh 100,000 kwa mwezi. Kwa wasiolipa, kama mathalani ana fremu tano, kila mwezi ana kipato cha Sh 500,000 ni (Sh 6,000,000) kwa mwaka.

Kama wafanyabiashara hao wa kupangisha hawalipi kodi ama kwa kupuuzwa, kusahaulika au kushindwa kuwafikia, basi ni wazi taifa linapoteza fedha nyingi kwa ‘msamaha’ usio rasmi.

Ndiyo maana ninasema, mamlaka husika ziangalie kwa makini jambo hili ili kila mwenye uwezo wa kufanya kazi na afanye kazi na mwenyebiashara ya namna yoyote kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, afikiwe ili kupitia kodi ya mapato, ashikiri kukuza uchumi wa taifa.

Columnist: habarileo.co.tz