Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wenye ligi yao wamerudi

Cd82545842cec774cc2aa4c3235b0011 Wenye ligi yao wamerudi

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MZUNGUKO wa nne wa Ligi Kuu soka Tanzania bara umemalizika juzi ambapo taswira imeanza kuonekana namna wakongwe wanavyorejea taratibu katika uongozi.

Awali, timu zilikuwa zinapishana katika uongozi kwa vipindi tofauti, zipo timu zilianza kwa moto kama KMC, Azam, Dodoma Jiji, Biashara, Simba na Yanga lakini kadiri wanavyocheza wengine wameshuka na kupanda.

Katika mzunguko huu, waliopanda Azam FC kutoka nafasi ya pili ilimng’oa KMC hadi ya kwanza. Ni baada ya kushinda mchezo wa nne mfululizo na kujikusanyia pointi 12 huku mshambuliaji wake, Prince Dube akionekana moto wa kuotea mbali akifikisha mabao matatu.

Azam FC ilishinda dhidi ya Tanzania Prisons mchezo uliochezwa Nelson Mandela, Sumbawanga. Kwa upande wa KMC baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0 ikashuka hadi nafasi ya nne.

KMC ilishushwa na Simba ambao wamepanda hadi nafasi ya pili baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Gwambina mabao 3-0 na kufikisha pointi 10 sawa na Yanga iliyopanda hadi nafasi ya tatu ikitoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa.

Kabla ya kupanda, Simba ilikuwa inashika nafasi ya tatu na Yanga ya tano katika mzunguko wa tatu. Mwingine aliyeshuka ni Dodoma Jiji iliyokuwa inashika nafasi ya nne imeshuka hadi ya sita.

Ni kutokana na kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania mabao 3-0. Matokeo hayo yaliifanya Polisi Tanzania kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya tano.

Kwa muonekano huo ni dhahiri kuwa wakongwe wamerudi katika uongozi ingawa ni mapema kusema kuwa watadumu kwani ligi ni ngumu na kila timu inaonesha ushindani wa hali ya juu hivyo huenda msimamo ukabadilika au ukabaki kama ulivyo.

Ukiachilia matokeo wanayopata na namna wanavyopambana, hizo ndio timu zenye usajili mzuri wa wachezaji zikifuatia nyingine. Ubora wao uwanjani unaonekana.

Wachezaji ambao wameng’ara kwa upande wa Simba naYanga ni Chris Mugalu, Meddie Kagere na Lamini Moro wenye mabao mawili kila mmoja.

Bado hali ni mbaya kwa Mbeya City ikiwa ndio timu pekee haijashinda mchezo wowote mpaka sasa ikishika mkia bila pointi ikifuatiwa na Gwambina yenye pointi moja katika michezo minne.

Ihefu timu iliyoanza kwa kasi inazidi kushuka iko katika nafasi ya 16 kwa pointi tatu ikifuatiwa na Mwadui huku Coastal ikijikongoja taratibu baada ya kushinda mchezo uliopita na kufikisha pointi nne sawa na JKT, Kagera na Tanzania Prisons.

Timu zilizopo katikati kuna Ruvu, Mtibwa, Namungo na Biashara. Kuna nafasi ya kupishana kulingana na matokeo ya michezo ijayo.

Michezo ijayo, Azam FC itacheza na Kagera Sugar, Yanga dhidi ya Coastal Union, JKT Tanzania dhidi ya Simba, KMC dhidi ya Polisi Tanzania, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons, Namungo dhidi ya Mwadui, Gwambina dhidi ya Ihefu na Dodoma dhidi ya Ruvu Shooting

Columnist: habarileo.co.tz