Napenda jinsi walivyo. Genge fulani hivi la washikaji ambalo limetawaliwa na watu wenye akili nyingi. Wanaishi katika dunia yao. Wanafanya mambo yao kivyao. Wana akili nyingi halafu wapo pamoja. Wameshikana mikono.
Nilikuwa nafikiria mechi ya kwanza ya jana ya kitu kinachoitwa African Football League.
Michuano mipya ya CAF ambayo pambano la kwanza lilichezwa pale Temeke. Arsene Wenger alitarajiwa kuwepo. Gianni Infantino alitarajiwa kuwepo. Kila mtu mkubwa wa mpira alitarajiwa kuwepo. Kuanzia Fifa hadi CAF.
Wazungu wa Ulaya walijaribu kuanzisha hiki kitu ambacho wangekiita Super League. UEFA ilikataa. Klabu zilikataa. Hiki kitu kingezima Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wazungu wenye mpira wao walikataa. Florentino Perez alijaribu kuwaunganisha wenzake lakini ilishindikana. Mashabiki waligoma kabisa.
Mashabiki walidai ni ubinafsi wa hali ya juu. Kwamba Ligi ya Mabingwa ilitosha tayari. Kuanzisha michuano hii Ulaya kungezidi kutengeneza pengo kati ya walionacho na wasionacho. Jaribu kufikiri, kwa wenzetu tajiri bado anamtetea maskini.
Huku kwetu tulikubali. Sio mbaya. Hatuna utajiri huo. Lakini wakubwa wamejaa katika hoteli zetu pale Posta na jana wameshuhudia pambano la kwanza la African Football League kati ya Simba dhidi ya Al Ahly. Unadhani ni kwa bahati mbaya kwamba kila mkubwa wa mpira amelala katika hoteli za Posta mpya kwa ajili ya kushuhudia mtanange huu? Kuna mambo kadhaa yapo nyuma ya pazia.
Kwanza kabisa wanajaribu kuweka presha kwa Wazungu kwa Ulaya kwamba michuano hii haina ubaya. Lakini pia wanatimiza ule msemo wao kwamba wao ni familia. Watu wa mpira wajanja sana. Unadhani kwamba waliichagua Tanzania kupiga filimbi ya michuano hii kwa bahati mbaya? Hapana. Mara nyingi wana makusudi yao.
Kusudi lao la kwanza siku zote ni kulinda kura zao. Kila nchi ijisikie ipo katika mpira. Rais wa nchi husika au ukanda husika unajihisi kuwa sehemu ya mpira. Sio kwa bahati mbaya sana hili linatokea. Kama kuna mambo tungekuwa tunayafuatilia na kuyawekea mkazo, basi mchezo wa soka ungekuwa unachezwa sehemu chache.
Kwanini tusianzie Misri ambako kuna uchumi mkubwa na hawakuhitaji marekebisho mengi ya uwanja wao wa Taifa? Kwanini tusianzie Afrika Kusini ambako pambano lolote la soka linaweza kuchezwa muda wowote ule? Hawahitaji kuufumua Uwanja wa Soccer City pale Soweto ili kuandaa pambano hili.
Kwanini wasianzie Morocco pale kwa Wydad? Hapana. Wao ni familia. Wameamua tu tuanzie Temeke ili na sisi tujisikie tupo katika familia. Nawakubali hawa watu. Huwa wana tabia hii. Ni ngumu kulivunja hili dude linaloitwa Fifa au lile linaloitwa CAF. Wanataka kila mmoja awe familia. Ili mradi uwe mpigakura na uwe mwenzao.
India sio nchi ya soka. Ukiamua kupeleka michuano mikubwa ya mpira wa miguu katika akili ya kawaida hauwezi kuipeleka India. Subiri kwanza, wao wana akili zaidi yetu. Hapa karibuni tu michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 17 ilifanyika India. Hizi ndio akili zao.
Ingekuwa akili ya kawaida kwa kule Asia ungeweza kuipeleka Dubai au Kuwait. Wao walipeleka India.
Wanautawanya mpira kwa akili ya makusudi tu kwa ajili ya kujenga uhusiano wa karibu na wapiga kura. Kwanini uiwaze India katika akili ya kawaida wakati wao mchezo wao ni kriketi?
Walipoamua kufanya mkutano mkuu wa Fifa wenye ajenda ya uchaguzi ungeweza kudhani wangeupeleka Rio de Janeiro au London ama New York au Melbourne ama Munich. Hapana. Wao wakaupeleka Kigali pale kwa Paul Kagame. Unaona jinsi akili zao zilivyo?
Wangeweza kwenda katika hoteli za kifahari, miji ya kifahari, yenye wanawake warembo na kila kitu ambacho mwanadamu anaweza kupata. Hapana. Wao wakachagua Kigali. Wakafanya mkutano wao, wakapiga kura zao kisela wakatawanyika. Leo wamekuja tena hapa kwa ajili ya pambano la Simba na Al Ahly. Nani anaweza kudai kwamba ukanda huu haupendwi na watu wakubwa wa huko duniani?
Niliwaambia watu kwamba Tanzania, Uganda na Kenya zina nafasi kubwa ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027. Ni kwa kupitia siasa hizi hizi tu niliuona huu wepesi. Nilijua wangetaka kuutawanya mpira kwa mara nyingine tena.
Sikiliza, mwakani 2024 fainali hizi wamezipeleka Ivory Coast. Mwaka 2025 wamezipeleka Morocco. Kwanini mwaka huu
wasizilete huku? Hesabu zilikuwa rahisi tu. Mwakani wamepeleka fainali hizi Afrika Magharibi. Mwaka 2025 wamezipeleka Afrika Kaskazini, kwanini mwaka 2027 wasizilete Afrika Mashariki?
Baada ya hapo hazitaweza kurudi katika pande hizi tatu. Wanaweza kwenda Afrika Kusini au kuna kina Madagascar na Shelisheli kama watamudu. Hivi ndivyo washikaji wanavyouendesha mpira. Kwanini usiiirudishe michuano hii Afrika Kusini ambao wapo tayari ukaamua kuwasubiri Watanzania wajenge viwanja vyao?
Wazungu wanaichukia Fifa Kwa sababu hii. Hawa rafiki zangu UEFA wangependa kuimiliki Fifa na kuumiliki mpira lakini kwa bahati mbaya wapo wachache kuliko mataifa mengine. Kila kura ni moja ndani ya Fifa. Hawana uzito wa kiasi cha kubembelezwa sana. Rwanda ni sawa na Ufaransa linapokuja suala la Fifa.
Kama tungewaachia rafiki zetu Wazungu wamiliki hiki chombo hiki leo Waingereza wangekuwa wameandaa tena Kombe la Dunia. Lakini mara ya mwisho wao kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1966 wakati Sir Alex Ferguson alipokuwa anamuoa mkewe kipenzi, Cathy ambaye alifariki dunia majuzi pale Uingereza.
Tuendelee tu kuwaona masela wakiendesha chombo chao kadiri wanavyojisikia. Ni familia haswa. Majuzi nimesikia wanataka kuandaa Kombe la Dunia la aina yake tangu mwaka 1930. Eti kwamba wanataka kuadhimisha miaka 100 ya Kombe la Dunia kwa kuandaa michuano hii katika mabara matatu tofauti.
Ni katika mwendeleo uleule wa kumgusa kila anayehusika. Kuanzia Temeke hadi Sao Paulo washikaji wanataka kumgusa kila mtu.
Kuanzia Mombasa hadi Tokyo washikaji wapo na wanataka kumgusa kila mtu katika soka. Binafsi sina shida nao. Acha waendelee tu.