Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Weka niweke! Argentina, Ufaransa chagua basi la kupanda

France Vs Argentina.jpeg Argentina vs Ufaransa leo

Sun, 18 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Leo ni fainali ya Kombe la Dunia 2022. Ndiyo, ni leo, Jumapili siku ya kukunja jamvi huko Qatar. Baada ya hapo, tutasubiri miaka minne - ambapo fainali zake zitafanyika huko Canada, Mexico na Marekani.

Lakini, macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye Uwanja wa Lusail nchini Qatar kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kufahamu kitakachojiri. Zamu ya nani leo? Argentina au Ufaransa? Lionel Messi au Kylian Mbappe?

Mambo ni moto. Fainali za Kombe la Dunia 2022 zimevunja rekodi nyingi, kumekuwa na matukio ya kushangaza na kuhuzunisha, lakini mwisho ni Ufaransa waliofanikiwa kutinga fainali wakijaribu kutetea taji la ubingwa wa dunia kama ambavyo Brazil walifanya mwaka 1962.

Argentina imetinga fainali baada ya kuwachapa waliokuwa namba mbili 2018, Croatia 3-0, shukrani kwa mabao ya Messi na Julian Alvarez, aliyefunga mara mbili.

Ufaransa wao wamerejea fainali kwa fainali za pili mfululizo baada ya kuikamua Morocco, waliotinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza 2-0, mabao ya Theo Hernandez na Randal Kolo Muani.

Utamu wa fainali ya Kombe la Dunia 2022 itamshuhudia Messi, moja ya wanasoka mahiri kabisa kwenye soka duniani, akiingia uwanjani kukipiga dhidi ya kipaji maridhawa kabisa cha kijana, Mbappe. Wawili hao, wanachezea klabu moja ya Paris Saint-Germain ya Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1).

Kama vita yao ya kwenda jino kwa jino kwenye fainali, wawili hao wapo kwenye mchakamchaka mwingine wa kusaka Kiatu cha Dhahabu, ambapo kila mmoja amefunga mabao matano - hivyo kufunga tena kwenye mchezo wa fainali kutakuwa na umuhimu mkubwa katika kujihakikisha ubingwa wa taji na ushindi wa Kiatu cha Dhahabu.

Katika kuelekea mchezo huo wa fainali, wakati mashabiki wakisubiri kumpata bingwa mpya wa dunia, hebu tuangazie takwimu za miamba hiyo miwili kwenye fainali, imevuna nini uwanjani katika mechi zao sita zilizopita hadi kufikia kilele huko Qatar.

Ufaransa inasaka nafasi ya kuwa timu ya kwanza kwenye kipindi cha miaka 60 kutetea taji la ubingwa wa dunia.

Wakati mashabiki wa Les Bleus wakisubiri kuona kile itafanya timu yao, hizo hapa namba matata za Ufaransa uwanjani:

Imecheza mechi: 6

Kadi nyekundu: 0

Kadi za njano: 5

Mabao ya kufunga: 13

Mabao ya kufungwa: 5

Mechi bila kufungwa: 1

Mashambulizi golini: 91

Mashambulizi yaliyolenga goli: 30

Mabao mengi: Kylian Mbappe (5)

Mashambulizi mengi: Kylian Mbappe (25)

Asisti nyingi: Antoine Griezmann (3)

Pasi nyingi: Aurelien Tchouameni (399)

Pasi za jumla: 3140 (zilizofika 2773)

Krosi nyingi: Antoine Griezmann (37)

Kucheza eneo kubwa: Aurelien Tchouameni (63.4km)

Kwa Ufaransa kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2022 huko Qatar mbele yao amesimama Messi na Julian Alvares, ambao shughuli yao kwenye fowadi ni balaa kubwa. Chama lao la Argentina limetinga fainali na hii hapa ni takwimu zake katika mechi sita ilizocheza hadi kufikia hatua hiyo wakisubiri kucheza mchezo wa soka wa mwisho kwenye fainali hizo. Takwimu za Argentina wakiingia fainali hizi hapa:

Imecheza mechi: 6

Kadi nyekundu: 0

Kadi za njano: 12

Mabao ya kufunga: 12

Mabao ya kufungwa: 5

Mechi bila kufungwa: 3

Mashambulizi golini: 83

Mashambulizi yaliyolenga goli: 39

Mabao mengi: Lionel Messi (5)

Mashambulizi mengi: Lionel Messi (27)

Asisti nyingi: Lionel Messi (3)

Pasi nyingi: Rodrigo de Paul (476)

Pasi za jumla: 3727 (zilizofika 3157297)

Krosi nyingi: Angel di Maria (24)

Kucheza eneo kubwa: Rodrigo de Paul (61.03km).

Columnist: Mwanaspoti