Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wazazi wana nafasi adhimu suluhisho dawa za kulevya

C8d0fb399515de2f5ce497301824ce92 Wazazi wana nafasi adhimu suluhisho dawa za kulevya

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

I NAELEZWA kwamba matumizi ya dawa za kulevya ni moja matendo ya kale zaidi kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo ambayo wakati fulani hupungua na kisha kuibuka.

Tatizo la dawa za kulevya pia linatajwa kama janga la kidunia kutokana na ongezeko la makundi ya vijana yanayotumia dawa hizo. ‘Kokeini yapatikana katika chupa za divai,’ ni kichwa cha habari cha taarifa moja inayoeleza jinsi polisi jijini Johannesburg, Afrika Kusini walivyopata kasha kubwa lenye chupa 11,600 za divai kutoka Amerika Kusini.

Miongoni mwa chupa hizo kulikuwa na kilogramu takribani 180 za kokeini. Inaaminika hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha kokeini kuwahi kuingizwa nchini humo. Japokuwa huenda ugunduzi huo ukaonesha kwamba mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafaulu, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba polisi hukamata kati ya asilimia 10 hadi 15 tu ya dawa za zite kulevya ulimwenguni kwa mwaka.

Hilo ni sawa na mkulima anayekata majani machache ya magugu hatari yanayomea haraka na kuacha mizizi yake ikiendelea kusambaa ardhini. Mhariri gazeti la Afrika Kusini la Saturday Star katika maoni yake baada ya shehena hiyo kubwa ya dawa za kulevya alionesha wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya vijana wanaotumbukia katika janga la matumizi ya dawa za kulevya nchini humo, hatua inayowaharibu na kushindwa kutoa mchango wao katika uchumi.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi barani Afrika zenye idadi kubwa ya vijana wanaotumia dawa za kulevya. “Tujue kwamba watoto wetu wanapojiingiza katika kutumia dawa za kulevya sisi wazazi hatuwezi kukwepa lawama na jamii kwa ujumla,” anasema mhariri na kufafanua kwamba wazazi wengi wamekalia kutafuta mali na kusahau jukumu la malezi mema kwa watoto wao.

Ndipo mhariri huyo anahoji: “Je, sisi hupata wakati wa kufanya nao mambo yanayowanufaisha? Kuwapa pesa ni rahisi kuliko kuwasikiliza kujua matatizo yao, matumaini yao, na mahangaiko yao. Leo usiku, tunapoketi mgahawani au tunapotazama televisheni, je, kweli tunajua mambo wanayofanya? Au huenda tukauliza, je, tunajua wanachofikiria? Tunajua marafiki zao mashuleni?” Tanzania yapiga hatua Kwa upande wa Tanzania, tangu serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, wimbi la dawa za kulevya limepungua kutokana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanavyofanyika.

Mwenyekiti wa kundi la viongozi wa dini wanaopambana na tatizo la dawa za kulevya nchini, Shehe Alhad Musa Salum, anaipongeza Serikali Tanzania kwa namna inavyoendelea kutokomeza dawa za kulevya nchini.

Alhad ambaye pia ni Shehe Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam anasema uwepo wa nyumba maalumu jijini Dar es Salaam, Zanzibar na maeneo mengine zinazotoa ushauri kwa waathirika na kuwajengea maarifa ya kufanya kazi halali imesaidia vijana kurejea katika shughuli halali.

Mwenyekiti huyo anasema yeye binafsi na na timu yake, wajibu wao ni kutembelea nyumba hizo na kutoa ushauri kwa Serikali, wazazi na mamlaka za kupambana na dawa za kulevya ili kutokomeza kabisa janga hili.

Ripoti nchini Kenya zinaonesha kwamba serikali hivi karibuni iliwataka wazazi kuzingatia malezi na kuchunghuza tabia za watoto badala ya kuwaachia walimu pekee majukumu ya ulezi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mazingira ya baadhi ya shule za msingi na sekondari si salama sana katika kusaidia watoto wasikutane na watoto wenzao ambao wameshaathirika na matumizi ya dawa za kulevya na kuwashawishi.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni iliwalaumu wazazi kwa kuwatelekeza watoto wao wanapowalea na kuwa chanzo cha kujiingiza katika matendo yasiyofaa ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.

Ripoti hiyo inaonesha kwamba wanafunzi 500,000 wa shule za sekondari wamewahi kutumia dawa za kulevya nchini Kenya na kwamba wanafunzi 370,000 wamewahi kutumia mirungi.

Taarifa inaonesha kwamba wanafunzi 314,000 wamewahi kutumia tumbaku ilihali 162,000 wamekiri kuvuta bangi, 50,000 wamevuta petroli na wanafunzi 26,058 wametumia dawa za kulevya aina ya heroine.

Waeleza walivyoanza kuvuta bangi “Nilipokuwa na umri wa miaka 13, dada wa rafiki yangu alinialika kwao. Baada ya muda nikiwa pale nikaona kila mtu anaanza kuvuta bangi.

Mwanzoni nilikataa lakini kutokana na ushawishi mwishowe nilionja kidogo,” anasema Michael (si jina lake halisi). Anasema huo ndio ulikuwa mwanzo wake wa kuvuta bangi ambapo mwanzoni aliona kama anaonjaonja tu lakini akajikuta akiikosa anajisikia vibaya.

Lakini Darren (si jina halisi) anasema alianza kuvuta bangi na baadaye kutumia dawa nyingine za kulevya kwa namna hii: “Familia yetu ilizingatia mno desturi za kale na tulipenda muziki wa zamani.

Kwa vile nilikuwa ninapenda muziki nikajiunga na bendi ya muziki. Siku moja, mwanamuziki mwenzangu alivuta bangi wakati wa mapumziko, alinishawishi kuvuta bangi na ndio nikaanzia hapo.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wawili hao hawakuishia kwenye bangi pekee bali walianza pia kutumia dawa nyingine za kulevya. Kijana mwingijne aitwaye Michael anasema: “Sik siku ningetumia dawa za kulevya.

Tatizo lilikuja kwamba sikuwa na marafiki wengine zaidi ya hao watuamiaji na mimi kama utani nikatumbukia huko” Tukirudi kwa Darren anasema: “Baada ya kuwa mraibu wa dawa za kulevya nikatamani kuacha.

Kwa miezi miwili au mitatu nilijaribu kuacha lakini marafiki wangu hawakuniruhusu. Nikaendeleza matumizi ya dawa hizi. Nilianza kusoma Biblia kabla ya kulala huenda ikanisaidia.

Mimi na mshirika wangu tulilewa chakari baada ya kutumia dawa ingawa nilimweleza kuhusu Biblia. “Asubuhi iliyofuata alimpigia simu ndugu yake mmoja wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova, alituelekeza kwa shahidi mmoja jirani yetu nikaenda kuonana naye. Lakini haikuaidia,” anasema.

Kikwazo cha faida Jitihada za serikali mbalimbali duniani katika kukomesha utengenezaji na uuzaji wa dawa za kulevya, hupunguzwa nguvu na faida kubwa inayotokana na uuzaji wa dawa hizo.

Inakadiriwa kwamba dawa za kulevya zenye thamani ya mabilioni ya dola huuzwa na kununuliwa kila mwaka nchini Marekani.

Kutokana na pesa nyingi zinazotokana na dawa hizo si ajabu polisi na maofisa wa Serikali, hata wa vyeo vya juu, kutumbukia katika mtego wa kunufaika na janga hili.

Alex Bellos, mtangazaji na mwandishi wa gazeti la The Guardian la Uingereza anaripoti kutoka Brazili kwamba uchunguzi wa Bunge nchini humo ulionesha kwamba wabunge watatu, wasaidizi 12 wa serikali na mameya watatu walitajwa kwenye orodha yenye zaidi ya watu 800 ambao wanashukiwa kushirikiana na magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya nchini humo.

Orodha hiyo ilikuwa pia na majina ya maofisa wa polisi, wanasheria, wafanyabiashara na wakulima kutoka majimbo 17 kati ya majimbo 27 nchini humo. Profesa mmoja wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha Brasília anasema: “Matokeo hayo yanaonyesha hali ya ujumla ya jamii nchini Brazili.”

Mbinu za kupambana Mwandishi mmoja, Luigi Zoja anaona kwamba kumsaidia mraibu kuacha mazoea fulani ni kazi bure iwapo hatasaidiwa kubadili kabisa njia yake ya kufikiri. Bodi ya kimataifa ya kuzuia dawa za kulevya (INCB) imezitaka serikali kuanzisha mifumo ya kitaifa ya data ili kufuatilia mwelekeo wa matumizi ya dawa zenye uraibu miongoni mwa vijana.

Wito wa bodi hiyo umo katika ripoti yake ya 2019 ikiangazia uhusiano kati ya matumizi ya pombe, tumbaku, bangi na kokeini miongoni mwa watoto na vijana barubaru.

Bodi hiyo imesema kuwa uwepo wa mfumo huo utawezesha kuwa na mipango ya kinga inayozingatia tafiti na mashuhuda, mipango ambayo inaweza kutekelezwa kipindi ambacho mtoto au kijana hajaanza kutumia dawa hizo.

Rais wa Bodi hiyo, Cornelis de Joncheere, amenukuliwa kwenye ripoti hiyo akisema kuwa, mara nyingi “matumizi ya pombe na tumbaku hutangulia matumizi ya bangi na dawa nyingine za kulevya.

“Tafiti ambazo zimefuatilia watoto hadi utu uzima zimedhihirisha kuwa pindi mtoto anapoanza kutumia pombe, tumbaku na bangi akiwa na miaka 16 hadi 19, kuna uwezekano mkubwa wa kutumia dawa za kulevya endapo atakutana na marafiki wa aina hiyo.”

Kwa mantiki hiyo, INCB kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) wamependekeza familia kuzingatia stadi za malezi, kuhamasisha ushiriki chanya katika maisha ya watoto, mbinu thabiti za mawasiliano ikiwemo kuweka kanuni.

Wanahimiza pia mitaala ya shule isaidie kuimarisha stadi binafsi na za kijamii za wanafunzi ikiwemo jinsi ya kufanya maamuzi na kuweka malengo ya maisha ili waweze hata kukataa matumizi ya dawa zenye uraibu wanapokutana na marafiki wabaya.

Serikali zinatakiwa kufanya ushirikishaji wa shule katika kuchunguza na kutathmini matumizi na hata kutoa ushauri nasaha na ufuatiliaji.

Lingine linalopendekezwa ni serikali kusimamia sheria ili kudhibiti kiwango cha matumizi ya bidhaa zinazochochea uraibu baadaye kama vile tumbaku, pombe na bangi miongoni mwa watoto na vijana wadogo.

INCB imependekeza pia serikali ziwekeze kwenye maendeleo ya utalaamu kwenye nyanja ya matumizi ya dawa za kulevya, kinga na matibabu kwa kumulika zaidi vijana.

Hii inapaswa kujumuisha mafunzo ya kitaifa na kuwapatia leseni watendaji wote wanaohusika na utoaji wa maamuzi, uandaaji na utekelezaji wa mipango kuhusu dawa za kulevya.

Columnist: www.habarileo.co.tz