Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wauza mafuta ya kupikia msipandishe bei kuumiza walaji

C85157f164d68d135dbd51e190f30fc3 Wauza mafuta ya kupikia msipandishe bei kuumiza walaji

Thu, 28 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, kumekuwa na upungufu wa mafuta ya kupikia jambo lililosababisha baadhi ya bidhaa nyingine zinazotegemea kutumia mafuta kuwa na mabadiliko mbalimbali katika bei na hata upatikanaji wake kuwa wa gharama kubwa zaidi.

Inafahamika kuwa mafuta ya kupikia ni kiungo muhimu kwa mwili wa binadamu, ingawaje wataalam wa afya wanashauri pia kutumika kwa mpangilio maalum usioweza kuleta madhara kiafya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe anasema nchi haina uhaba wa mafuta ya kupikia na kuwataka watakaopandisha bei ya bidhaa hiyo kufutiwa leseni.

Amewaonya mawakala na wafanyabiashara wa jumla kuhakikisha kuwa bei ya bidhaa hiyo haitopandishwa, jambo litakalosababisha wananchi kuendelea kuhangaika kwa ajili ya upatikanaji wake.

Kauli ya Waziri huyo inatia moyo wananchi ambao kila kukichwa wamekuwa wakiulizana namna ya kupatikana kwa bidhaa kwa gharama halisi ambayo hata wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya kutengenezea bidhaa zao.

Kwa mfano mjasiriamali aliyekuwa akiuza andazi moja kwa shilingi 100 amejikuta akipandisha na kuuza kwa sh 200, kadhalika aliyekuwa akikaanga samaki naye akiwa na gharama zake kulingana na alivyoweza kuipata bidhaa hiyo lakini pia kwa mamalishe chakula kuwa na tofauti.

Aidha, katika mitandao mbalimbali ya kijamii, hoja ya kukosekana kwa mafuta imekuwa ikijadiliwa kila kona ya nchi, huku wanawake mbalimbali wakiulizana kutaka kujua kama kuna unafuu wa bei kwa bidhaa hiyo kwa walioko mikoa mingine ili kuona uwezekano wa kuifikia na kuendelea na shughuli zao za mara kwa mara.

Kutokana na hali hiyo, ni muhimu mawakala wa bidhaa hiyo kutambua kuwa serikali imeshakiri kuwa hakuna uhaba wa mafuta na tayari zimeingizwa tani 48,250 kati ya Desemba mwaka jana na januari mwaka huu ilhali mahitaji ya nchi ni tani 30,000 kwa mwezi.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja zimeingizwa meli mbili moja ikiwa na tani 21,800 na nyingine ikiwa na tani 26,450, lakini pia Februari 17 mwaka huu itakuja meli nyingine na mafuta hayo ni tofauti nay ale yanayozalishwa nchini.

Pamoja na tani hizo kuingizwa nchini, lakini bado katika kipindi hicho kwenye masoko mbalimbali bado walaji wamekuwa wakiipata bidhaa hiyo kwa gharama kubwa tofauti na hali ilivyokuwa awali, jambo ambalo wafanyabishara na mawakala wanahitajika kuliangalia kwa umakini.

Ikumbukwe kuwa mafuta hayo yalipanda kutokana na bidhaa hiyo kupanda katika soko la dunia ambapo kulichangiwa na kushuka kwa uzalishwaji kutokana na kuibuka kwa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo nchini mbalimbali zilifunga utendaji na usafirishaji jambo lililopunguza bidhaa hiyo inayoingizwa nchini.

Ni vyema kwa wakati huu, mawakala kuonesha ushirikiano wa kusambaza bidhaa hiyo hatua itakayoondoa mwanya kwa wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kuendelea kupandisha bei ya bidhaa hiyo huku wananchi wakiendelea kuipata kwa gharama iliyo kubwa.

Aidha ni vyema mamlaka zitakazobaini kuwepo kwa mawakala watakaohusika kupandisha bei hiyo ya mafuta kuhakikisha inawafutia leseni jambo ambalo litakuwa fundisho kwa wengine kuacha vitendo hivyo ambavyo ni vya kuwalaghai wananchi.

Kadhalika wafanyabiashara nao wasitumie fursa hiyo kuficha bidhaa hiyo wakidhani kuwa ni eneo ambalo wataweza kujipatia fedha zaidi, badala yake washiriki bega kwa bega kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia wananchi kwa gharama ambazo sio za kuwaumiza bali zile ambazo ni halisi.

Columnist: habarileo.co.tz