Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watumiaji wa vifungashio waelimishwe vilivyohalalishwa

A720a9e91d2c3a0fd4fad51df525ae9a.png Watumiaji wa vifungashio waelimishwe vilivyohalalishwa

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ZIMEBAKI siku 26 kufikia mwisho wa matumizi ya vifungashio vilivyokatazwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira na Kanuni za Katazo la mifuko ya plastiki ya mwaka 2019.

Januari 8 mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu alisema kumeibuka wimbi la mifuko ya plastiki kwa kisingizio cha vifungashio wakati vingi havikidhi vigezo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Katika hilo, alitoa siku 90 kwa wauzaji na wafungashaji wa bidhaa wanaotumia vifungashio hivyo kuwa ndani ya muda huo wahakikishe kama wana akiba wavitumie viishe, vinginevyo baada ya katazo hilo hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Alisema licha ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki lakini siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya ‘tubings’ visivyokuwa na sifa na hivyo kutokidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) .

Hayo yasemwayo yana ukweli kwa sababu maeneo mengi hivi sasa mfano kwenye masoko makubwa watengenezaji wa vifungashio vya plastiki vidogovidogo vya kufungia karanga, ubuyu, kripsi na vitu vya namna hiyo vimekuwa vikizalishwa kwa wingi bila kufuata kanuni na viwango vya TBS.

Uzalishaji huo huenda kwa njia moja au nyingine ukafanywa na watu kama njia ya kujipatia kipato na kutoa ajira kwa wengine lakini pia wakawa hawana maarifa ya kutambua viwango vya plastiki vinavyotakiwa ni vipi.

Hivyo basi, wakati zikiwa zimebaki siku hizo 26 kufikia mwisho wa matumizi ya vifungashio hivyo ni vyema wataalamu wakiwemo watu wa TBS, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakaendelea kuwaelimisha wazalishaji na watengenezaji jinsi ya kutambua malighafi zinazokubalika kutengeneza vifungashio vya plastiki vyenye ubora.

Nasema hivyo kwa sababu katika kutekeleza Sheria ya Mazingira na Kanuni za Katazo la mifuko ya plastiki ya mwaka 2019 sio watu wote wanafahamu inataka nini na inakataza vitu gani na pia kanuni zake zikoje, hivyo wataalamu kutoka taasisi tajwa wana wajibu wa kuelimisha umma ili kuwa na uelewa na wakati wa kutekeleza katazo hilo kusiwepo na malalamiko.

Wananchi wanapenda kufanya kazi na biashara katika mazingira ya amani na hakuna aliye juu ya sheria, wote wanapenda kufuata sheria na kanuni, hivyo basi kwenye hilo la katazo la vifungashio ni vyema pia umma ukajulishwa na kuelimishwa aina ya vifungashio vinavyokubalika na kama vina alama ni zipi ili kutofautisha na vifungashio visivyo na ubora.

Mara kadha wa kadha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka amekuwa aliwataka wenye viwanda vinavyozalisha vifungashio ambavyo vinakidhi viwango, vinarejelezeka pamoja na kuwa na lebo iwe rahisi kumtambua mzalishaji na kudhibiti usambaaji wa vifungashio hivyo katika mazingira yetu.

Dk Gwamaka katika hilo alibainisha kuwa vifungashio vingi vinavyozalishwa havina lebo ya mzalishaji wala bidhaa inayokusudiwa kufungashiwa na pia haviwezi kurejelezeka, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kusema hatua hiyo inachafua mazingira na pia inaondoa usawa wa kibiashara kwa wale ambao wamekuwa wakizalisha vifungashio mbadala ambavyo ni rafiki kwa mazingira.

Hivyo basi pamoja na hayo yote, tuendelee kusisitiza na kuelimisha umma, wazalishaji na wauzaji wa vifungashio aina ya vifungashio vinavyokubalika na visivyokubalika na kama vina alama za utambuzi ili kuzibaini ni zipi kumsaidia mtumiaji kuepuka usumbufu.

Sote tunapenda mazingira yetu yawe rafiki, hatutaki matumizi ya vifungashio vyenye madhara kwa afya zetu na mazingira yetu, hivyo jukumu la elimu ya utambuzi wa vifungashio rafiki na vile visivyo rafiki ni la msingi zaidi ili kuyalinda mazingira yetu nayo yatutunze.

Columnist: www.habarileo.co.tz