Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watoto wa wakimbizi Kigoma wameanza ‘kuisumbua’ dunia?

Bernard Kamungoo Vs Messi Watoto wa wakimbizi Kigoma wameanza ‘kuisumbua’ dunia?

Sat, 25 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

IMEANZA kuwa mazoea katika mtandao wa wikipedia. Umri? Miaka 23. Sehemu ya kuzaliwa? Kigoma, Tanzania. Umri? Miaka 20. Sehemu ya kuzaliwa? Kigoma Tanzania. Zamani ilikuwa Yaounde, Accra, Dakar, na kwingineko Afrika. Sasa hivi Kigoma imejiunga katika mbio.

Watoto wa wakimbizi waliozaliwa katika kambi za wakimbizi pale Kigoma wameanza kukimbiza Ulaya na kwingineko. Tuanze na nani? Huyu hapa. Nestory Irankunda. Wiki iliyopita alisajiliwa na Bayern Munich akitokea klabu ya Adelaide ya Australia. Ni mwepesi na ana jicho la lango. Mtandao wa wikipedia unaonyesha alizaliwa Kigoma Februari 9, 2006.

Kama tungekuwa na sheria ya uraia pacha, basi Irankunda alikuwa na uwezo wa kucheza Tanzania, Australia au Burundi ambako wazazi walitoroka vita kuja kuishi katika kambi za wakimbizi pale Kigoma. Nasikia Warundi wanataka kumrudisha kwao lakini ni dili kwa Waustralia kwa sababu pia ameshaichezea timu yao ya vijana.

Kuna huyu hapa, Bernard Kamungo. Naye alizaliwa katika kambi ya wakimbizi pale Kasulu Kigoma. Wazazi wake walitokea Burundi. Ameibukia Marekani katika jiji la Texas. Na sasa anatamba katika klabu ya FC Dallas. Pambano dhidi ya kina Lionel Messi Inter Miami ambalo walifungwa 3-2 yeye alitupia bao moja.

Aliwahi kuitwa hapa kuichezea timu ya taifa akaja, lakini hakuweza kucheza. Uraia pacha ulisumbua. Sasa hivi Wamarekani wameamua kumchukua jumla na tayari wamemuita katika kikosi chao kitachoshiriki michuano ya Olimpiki. Ni wazi kwamba Kombe la Dunia 2026 ambalo Mmarekani atakuwa mwenyeji linamsubiri.

Kuna huyu hapa Charles M’mombwa ambaye aliifungia Taifa Stars dhidi ya Niger pale Morocco. Huyu historia inasoma kwamba alizaliwa Congo, lakini akakulia Kigoma katika kambi za wakimbizi kabla ya kwenda zake Australia. Ameamua kuichezea Tanzania lakini angeweza kukipiga Congo au Australia.

Watoto hawa ni matokeo ya vita vilivyotokea katika nchi za Burundi na Rwanda wakati ule wa mauaji ya kimbari Aprili 1994. Wazazi wao walitoroka na kuwazaa Kigoma. Lakini wale wa Congo ni wale ambao daima wametorokea hapo kwa sababu Congo kamwe haijawahi kuwa salama.

Nini kinatokea? Hawa watoto wanadhihirisha tofauti iliyopo baina yetu na wazungu. Sio ubaguzi lakini ni ukweli. Katika hizi kambi za wakimbizi kunakuwa na mpango maalumu wa kuzihamishia familia za wakimbizi kwenda kuishi Ulaya, Marekani au Australia. Ni mpango maalumu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi.

Sio wote wanafia nchini. Kuna familia nyingi tu ambazo zinatafutiwa makazi katika nchi zilizoendelea kwa ajili ya kuipunguzia mzigo Tanzania. Hapa ndipo hawa rafiki zetu wanakopata zali ya kwenda nje na kung’arishwa katika vipaji vyao. Wakati mwingine inafikirisha kama wangebakia nchini wangeweza kutoboa katika maisha kupitia katika vipaji vyao.

Wanapofika nchi hizo wanapelekwa katika shule mbalimbali na vipaji vyao huwa vinatambulika zaidi katika michezo shuleni. Sidhani kama itabakia katika soka tu. Nadhani itakwenda mbali zaidi hata katika michezo mingine wataibuka wanamichezo wengine ambao wamezaliwa Kigoma.

Sio hawa tu, mchezaji mahiri kama Alphonso Davies wa Bayern Munich alizaliwa katika kambi ya wakimbizi pale Ghana. Wazazi wake walikuwa wamekimbia vita nchini Liberia. Baadaye ukafanywa mpango na UNHCR familia yake ikapelekwa Canada katika kambi ya wakimbizi.

Staa wa zamani wa Ligi Kuu ya England, Saido Berahino naye alikimbia vita Burundi mwaka 1997 wakati baba yake alipouwawa. Akaenda Kigoma kabla ya kusafirishwa kwenda Birmingham, England. Akaingia katika shule na kucheza soka. Baadaye akaamua kuichezea timu ya taifa ya Burundi. Soka la vijana alichezea timu ya England.

Vipi kuhusu Eduardo Camavinga? Huyu huyu staa wa Real Madrid. Yeye alizaliwa katika kambi ya wakimbizi pale Cabinda ,Angola. Wazazi wake walikimbilia Ufaransa akiwa na umri wa miaka miwili tu. Kipaji chake ndio kimebadilisha maisha ya familia yake. Angeweza pia kuichezea timu ya taifa ya Angola kama angetaka.

Usinikumbushe kuhusu mchezaji aliyeitwa Rio Mavuba. Staa wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa. Huyu naye wazazi wake walitoroka Angola kupitia njia ya bahari huku mama yake akiwa mjamzito. Akamzaa baharini katika kina kinene. Hadi leo sehemu ya kuzaliwa katika pasipoti yake imeandikwa ‘at the sea’ kwa maana ya kwamba ‘amezaliwa baharini’.

Tuendelee tu kuwapokea hawa wakimbizi wanaokuja Stars. Wengine wataamua kucheza huko huko kama wakiwa wazuri zaidi lakini wengine wapo katika viwango vyetu na watataka kuichezea timu ya taifa kwa ajili ya kupata nafasi ya kutia uzito katika wasifu wao. Wanapitia mambo mengi na ishu kadhaa ambazo zinawaimarisha kuja kuibuka bora zaidi siku za usoni.

Tatizo la umaskini wetu au ukosefu wa mipango ni kwamba hatuwapi kipaumbele watu wa michezo mingine. Nani atakuja kubeba bendera ya taifa na kutuwakilisha katika ndondi kwa sababu amezaliwa Kigoma? Nani atakuja kutuwakilisha katika riadha kwa sababu amezaliwa Kigoma? Hii michezo mingine hatujaiendeleza vya kutosha kiasi cha mtu kujisikia fahari kuiwakilisha Tanzania.

Soka walau inajitutumua na ndio maana vijana hawa wanafikiria kurudi nchini. Lakini ni vizuri kwao kuitumia Taifa Stars kwa ajili ya kujijengea wasifu ambao utawarahisishia kupata timu mbele ya safari. Wale wazuri zaidi kama Kamungo wataamua kucheza Marekani lakini ambao wanahisi watapata nafasi ngumu kucheza mataifa ya huko watacheza huku.

Katika michezo mingine haijalishi upo taifa gani lakini wasifu wao utajitegemea kutokana na uwezo wako binafsi. Huku katika soka tuwategemee hawa watoto warudi kwa sababu wana sababu nyingi za kurudi ikiwemo kupata nafasi kwa urahisi zaidi. Soka ni mchezo wa watu wengi uwanjani. Ngumi ni mchezo wa mchezaji mmoja.

Pale Ulaya kuna wachezaji kibao wazungu ambao baba zao walikuwa wakimbizi. Mfano ni watoto wa Ulaya Mashariki ambao walikimbilia Ulaya Magharibi wakikwepa vita kadhaa zilizowahi kutokea Ulaya Mashariki kama ile vita ya Kosovo. Hawa wengi wameshuka chini huku na wametuama katika michezo mbalimbali.

Granit Xhaka wazazi wake walikimbia vita kule Albania kisha wakamzaa yeye katika jiji la Basel pale Uswisi. Ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Uswisi kwa sasa.

Xherdan Shaqiri yeye alizaliwa Kosovo wakati huo ikiwa eneo la Yugoslavia. Baadaye wazazi wake walikimbilia Uswisi ambako aliibukia kuwa staa wa soka.

Columnist: Mwanaspoti