Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watetezi wa uhai wafurahishwa na Rais kutosaini kinyongo

Bddc3c88d32349d601c97900e022fd52 Watetezi wa uhai wafurahishwa na Rais kutosaini kinyongo

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Kutetea Uhai (Prolife)-Tanzania, limesema limefurahishwa na uamuzi wa Rais John Magufuli kuwapunguzia adhabu wafungwa 256 kutoka kunyongwa mpaka kufa na kuwa kifungo cha maisha.

Mwenyekiti wa Prolife Tanzania, Emil Hagamu alisema jana kuwa, hatua hiyo chini ya mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa sheria, inaonesha namna Rais Magufuli alivyo na utashi mkubwa na wa dhati kutetea na kulinda uhai wa watu wakiwamo wafungwa, wenye ulemavu, wazee na watoto kwa kuzuia mauaji dhidi yao.

“Kitendo hiki kinaonesha utashi mkubwa wa kulinda uhai wa watu katika taifa hili analoliongoza maana katika hotuba na kauli zake nyingi anaonesha wazi namna alivyo mtetezi mkubwa wa uhai hata kwa kupinga kwa nguvu utoaji mimba na mbinu za kudhibiti uzazi,” alisema Hagamu.

Desemba 9, mwaka huu wakati Rais Magufuli akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri aliowateua baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020, alitangaza kuwapunguzia adhabu wafungwa hao na sasa watatumikia kifungo cha maisha huku wakifanya kazi, badala ya kunyongwa hadi kufa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Magufuli alisema inabidi asamehewe kwa kuwa hayuko tayari kusaini kutekeleza hukumu ya kuwanyonga wafungwa hao 256 kwani kufanya hivyo atakuwa ameua zaidi.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano hadi sasa, alitakiwa kuwa amesaini utekelezaji wa kunyongwa hadi kufa kwa watu 256 waliohukumiwa kunyongwa, lakini hajamnyonga hata mmoja.

“Kwa hiyo wale wafungwa 256, kwa mamlaka niliyopewa, nawapunguzia kifungo chao cha kunyongwa na sasa wafungwe maisha. Kwa sababu wapo waliohukumiwa kunyongwa kwa sababu waliua, labda mwingine aliua mtu mmoja au wawili au watatu, mimi sheria inaniambia niue 256, nani mwenye dhambi zaidi huyu aliyeua mmoja au wawili au mimi nitakayeua 256?” alisema.

Aliongeza kuwa, “ kwa hiyo nimeshindwa kuwaua, mnisamehe kwa hilo, kwa sababu mimi ndio nitakuwa muuaji wa kuuawa kwa sababu wenzangu wameua mtu mmoja au wawili au watatu na wakahukumiwa kunyongwa, halafu mimi niue 256, si nafuu mimi ninyongwe hapo hapo hata bila kupelekwa mahakamani!"

Columnist: habarileo.co.tz