Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watanzania tuungane kuombea amani, uchaguzi

PhotoGrid 1600687087442 Watanzania tuungane kuombea amani, uchaguzi

Fri, 23 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMATANO ijayo Watanzania watafanya Uchaguzi Mkuu wa sita katika mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini ulioanza mwaka 1992. Uchaguzi Mkuu wa kwanza katika mfumo huu ulifanyika mwaka 1995.

Kimsingi, Watanzania kwa umoja wao wanastahili pongezi kwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na wa mwaka 2015, hawajawahi kuchezea amani.

Sisi tunasema hali hii inatokana na Watanzania na wote wenye mapenzi mema, kumgeukia na kumlilia Mungu aingilie kati maisha yao na kuwasaidia kuhakikisha kuwa tunu hii ya amani kwa taifa haipotei, bali inalindwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote.

Pia tunasema amani ya Watanzania imedumu kutokana na Watanzania kukomaa kiimani na kisiasa, kiasi cha kutambua ukweli kuwa siasa, dini na kabila ni kwa ajili ya watu na siyo watu kwa ajili ya siasa, dini wala kabila lolote.

Mambo hayo mawili tunaamini ndiyo yamekuwa miongoni mwa nguzo za kudumu za amani ya Tanzania, yakichagizwa na ukweli kwamba Watanzania wanataka maendeleo na hivyo wanazingatia ukweli kuwa amani ni tunda la haki na haki ni tunda la amani.

Watanzania wanatambua ukweli kuwa bila amani ni vigumu mtu au kikundi chochote kiwe cha kidini, kisiasa au kikabila, kutafuta na kupata haki ; na ndiyo maana kila Mtanzania mwenye utashi mema, anatanguliza amani ili wapate haki na maendeleo.

Ni kwa msingi huo, tunasema kwa Watanzania kipindi hiki kinahitaji maombi na kumlilia Mungu kupitia imani mbalimbali kuliko kipindi kingine chochote.

Tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi, kwa namna wanavyotimiza wajibu wao kwa weledi katika kipindi hiki cha kampeni. Pia, tunawashukuru viongozi wa vyama vya siasa na wanasiasa ambao wamekuwa makini, kuhakikisha kuwa hawafanyi jaribio lolote la kutaka kutikisa amani ya nchi, wala kuonesha dalili za kutaka kuvuruga amani.

Hali kadhalika, tunawapongeza viongozi wa dini kwa kuwa mstari wa mbele kuendelea kuhimiza waumini wao, kuhakikisha wanalinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Viongozi wa dini na waumini wameendelea kuliombea taifa livuke salama kipindi hiki, bila kushawishiwa na mtu au taifa lingine lolote, maana Tanzania itabaki kuwa ya Watanzania.

Kwa namna ya pekee, tunapongeza taarifa ya juzi ya viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini, kwamba watafunga kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo hadi kesho kutwa Jumapili Oktoba 25 kuombea Uchaguzi mkuu huu.

Maombi hayo yatafanyika katika makanisa na misikiti kwa siku walizokubaliana. Hatua hiyo inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania kwa sababu itawezesha Tanzania kuendelea kudumu katika amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Tunasisitiza kuwa hiki ni kipindi sahihi kwa Watanzania kuungana kuombea amani na uchaguzi mkuu wa wiki ijayo ili ufanyike kwa amani na kuzaa matunda yanayotarajiwa

Columnist: habarileo.co.tz