Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watanzania tujitokeze kumuaga Rais Mkapa

497cb2cdc683241bbdfdd9bd45e1f771 Watanzania tujitokeze kumuaga Rais Mkapa

Mon, 27 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATANZANIA wanaendelea kuomboleza kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye atakumbukwa kwa mengi aliyofanya katika uongozi wake katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Rais huyo ambaye wakati wa uhai wake aliongoza kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa na anatarajiwa kuzikwa kijijini kwake Lupaso mkoani Mtwara keshokutwa, Jumatano.

Ni wazi kwa kizazi cha kipindi cha uongozi wake hakuna ambaye hakuutambua weledi wake vyema katika uongozi wake, hasa pale alipojipambanua kwa dhana ya uwazi na ukweli iliyoleta mafanikio chanya ya sekta mbalimbali.

Serikali imepanga ratiba ya kuaga mwili wa Mkapa na wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuaga mwili huo ambao unatarajiwa kuzikwa kijijini kwake Lupaso.

Mkapa atakumbukwa kwa mengi ambapo wapo wanaozungumzia sekta ya uchumi kuimarika, wananchi kujitambua na kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea kwani alihamasisha kufanya kazi akisema mtaji wa masikini ni nguvu zake.

Wakati wa uhai wake, Mkapa atakumbukwa kwa mfumuko wa bei za bidhaa kutokupanda mara kwa mara, kutokuwepo migomo ya vyombo vya usafiri wa umma na kuwahimiza watu kufanya kazi kwa bidii kuleta maendeleo.

Aidha, wakati wa uhai wake, Mkapa alianzisha taasisi mbalimbali, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA).

Alianzisha pia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mawasiliano (TCRA).

Pia alijenga uwanja mkubwa wa mpira wa Taifa na alianzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF), Mkukuta na nyingine nyingi ambazo sasa zinatoa manufaa kwa Watanzania.

Mkapa aliyafanya hayo kwa upendo akiwa na lengo chanya kwa Tanzania akiwakumbuka Watanzania kwa nyanja mbalimbali ili kuweza kunufaika na kuona matunda ya nchi yao.

Kwa kuzingatia uongozi wake na aliyoyafanya, serikali imetoa siku tatu za kuaga mwili wa kiongozi huyo kwa jiji la Dar es Salaam kuanzia Julai 26 hadi Julai 28 kabla ya mwili huo kupelekwa kijijini kwake kwa ajili ya maziko.

Ni kweli wananchi kila mmoja ana majukumu yake lakini katika hili la kuaga kiongozi huyo atakayekumbukwa kwa mchango wake mkubwa, ni vyema watu wengi kujitokeza kuaga siku ya leo na kesho ambayo ataagwa kitaifa kwa utendaji wake usiosahaulika.

Mkapa ameondoka kipindi ambacho anahitajika kwa ushauri,mawazo na busara zake utendaji wa maeneo mbalimbali, hivyo siku zilizopangwa Watanzania kuaga mwili huo ni muhimu kujitokeza kama ishara ya upendo wetu kwake.

Yapo mengi ya kujifunza kwake sehemu mbalimbali alizopitia kwenye siasa jambo ambalo litatoa mwanya viongozi katika nyanja mbalimbali kujifunza na hata kuweza kuiga na kuwa na mwelekeo wa utawala ulio bora nchini.

Columnist: habarileo.co.tz