Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Watakapomaliza kumsitiri mpendwa wetu, turajea ziwani’

4e193142804113d16c2b6a6e4a80cad3 ‘Watakapomaliza kumsitiri mpendwa wetu, turajea ziwani’

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BAADHI ya wananchi wilayani Chato mkoani Geita wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wa samaki katika Ziwa Victoria na uchimbaji wa madini wameeleza kusitisha kwa muda kazi zao ili kupisha maombolezo ya kifo cha Rais John Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya wavuvi, mvuvi na mfanyabiashara wa samaki anayefanya shuguli zake katika mwalo wa Nyamilembe uliopo Kata ya Nyamilembe wilayani Chato mkoani hapa, Bashiri Mathias alisema hatua hiyo inatokana na watu wengi wanaojishughulisha na kazi hiyo kuguswa na msiba huo.

Bashiri alisema kifo cha Rais Magufuli kimewashitua wavuvi kiasi cha kuamua kusitisha kwa muda kuvua samaki kutokana na majonzi ya msiba yaliyowafanya kukosa nguvu ya kwenda ziwani kulingana na ukweli kuwa kiongozi huyo alipigania maslahi na mazingira rafiki kwa wavuvi.

Alieleza kipindi akiwa Waziri wa Uvuvi, Rais Magufuli alifanya kazi kubwa kupiga vita uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria kitu ambacho kimewasaidia wavuvi wengi hivi sasa kupata mazao mengi ya samaki na kujipatia kipato kikubwa kilichowawezesha kujikwamua kiuchumi tofauti na miaka ya nyuma.

"Baada ya kupata taarifa kuwa kiongozi wetu ametangulia mbele za haki, wavuvi wote wa Nyamilembe tumesitisha na uvuvi, hata nguvu za kwenda ndani ya maji hatuna kabisa, bado tunamlilia kiongozi wetu, hadi watakapomsitiri ndio tutaingia ziwani," alisema Bashiri.

Kwa upande wao wachimbaji wadogo wa madini wilayani Chato walisema wao ni miongoni mwa kundi ambalo limesikitishwa na kifo cha Rais Magufuli kutokana na ukweli kwamba kipindi cha uongozi wake aliwapa fursa ya kufanya shughuli zao pasipo kubughudhiwa.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Msasa uliopo kata ya Makurugusi wilayani Chato, Renutus Ngeleja ambaye ni mmoja wa viongozi alikiri kuwa ndani ya siku hizi za maombolezo ya msiba, mahudhurio ya watu kufanya kazi mgodini yamepungua kwani wengi wapo kwenye majonzi.

Ngeleja alisema wataendelea kumkumbuka Rais Magufuli kwa kuwahamasisha kufanya kazi kupitia kauli yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ na pia kwa utetezi wake dhidi ya haki za wachimbaji wadogo ambapo kwa sasa wananufaika na kazi yao.

Machimbaji katika mgodi wa Msasi, Christopher Katali alisema shughuli zimepoa mgodini hapo kutokana na msiba wa kiongozi huyo shupavu uliowagusa wachimbaji wadogo kwani alipoingia madarakani aliwapa uhuru wa kuchimba madini na alianzisha masoko ya madini kila mkoa, hivyo kuondoa adha ya wachimbaji kutapeliwa.

Columnist: www.habarileo.co.tz