Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Washindi hongereni, mliokosa toeni ushirikiano

Ffdef9429a2d1a2dedf8dff4a6ad83fb Washindi hongereni, mliokosa toeni ushirikiano

Fri, 30 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANGU kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani juzi ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao wa miaka mingine mitano, siku ya jana na leo yanaendelea kutangazwa majina ya walioibuka na ushindi.

Hadi jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinaendelea kuongoza katika nafasi hizo. Ni muda muafaka sasa kwa wale mliokosa kutoa ushirikiano wa kuijenga Tanzania yetu.

Binafsi napenda kuchukua kuwapongeza walioshinda katika nafasi hizo za ubunge na udiwani kutoka vyama vyote vilivyoshiriki. Hakika ushindi huo ni sauti ya wananchi wa maeneo waliyogombania.

Wananchi hao kwa kuwachagua viongozi wao hao hakika wameamua kuchagua maendeleo, hivyo basi wao ndio watu wa kwanza kuhakikisha maendeleo hayo yanapatikana kwa kuanza na uimarishwaji wa amani na utulivu.

Jukumu hilo la amani na utulivu sio la waliopiga kura au waliochagua viongozi tu bali hata wale ambao hawakuwachagua washindi hao na hata ambao hawakupiga kura kabisa.

Wote pamoja mnapaswa kutambua kuwa mna wajibu wa kuendeleza amani na utulivu hasa kwa kujiepusha na kila aina ya vishawishi kutoka kwa wasioitakia mema amani ya nchi hii.

Epukeni kauli za chuki na uchochezi kutoka kwa wanasiasa ambao hawajachaguliwa, hawa wanaona njia pekee iliyobakia ni kuhamsha vurugu.

Wananchi waepukeni wanasiasa wa aina hii kwa kuwa wanachotaka ni kutumia nguvu zenu kuhamsha vurugu kwa maslahi yao binafsi.

Iwapo vurugu zikitokea asilimia kubwa ya waathirika ni nyie wananchi ambapo mtajeruhiwa na wengine hata kupoteza maisha huku mkiwaacha wategemezi wenu wakihangaika.

Kama mawakala wa vyama vya siasa waliowawakilisha wagombea katika uhesabuji wa kura wamekubaliana na matokeo na kusaini fomu za Tume ya Uchaguzi (NEC), ina maana washindi hao wamepatikana kiuhalali.

Hivyo basi hakuna haja ya kuwasikiliza wanaohamasisha vurugu.

Kwa kuwa maendeleo hayana chama basi wananchi kwa ujumla mnapaswa kuwatumia waliochaguliwa kupigania maendeleo ya nchi.

Huu sio muda wa kugawanyika ila ni muda wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuisogeza nchi katika hatua bora zaidi ya kimafanikio.

Ifahamike kuwa bado nchi inayo mengi ya kuyatekeleza kwa maslahi ya wananchi kama vile kuimarisha sekta za afya, maji, miundombinu na masuala mengine muhimu hivyo kuna haja ya kuwapatia ushirikiano washindi watakaotangazwa.

Navishauri vyombo vya dola kuendelea kuwa makini katika kuwashughulikia watu ambao wataonekana kuhamsha hisia za vurugu kwa wananchi.

Uwepo mkakati wa kuwakamata mmoja mmoja na kumwajibisha kwa mujibu wa sheria tena kwa haraka zaidi kabla ya sumu zao za chuki kuenea.

Zipo nchi ambazo zimeingia kwenye machafuko baada tu ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu na tena machafuko hayo yametokana na kauli za wanasiasa walafi.

Hapa nchini hilo lisipewe nafasi kabisa tena hasa ikizingatiwa kuwa wasioitakia mema nchi wamekuwa wakitafuta mwanya wa kuhamasisha vurugu, wanatamani kuutumia mwanya huu wa uchaguzi kuhamsha vurugu.

Nawashauri wale ambao kura hazikuwatosha, mtoe ushirikiano kwa waliochaguliwa ili tuijenge nchi yetu kwani Tanzania ni moja na ni yetu sote.

Columnist: habarileo.co.tz