Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wapinzani mnataka nini hasa?

314c13b59fe27badf7050fc957429087 Wapinzani mnataka nini hasa?

Wed, 28 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAREHE 19 Machi, 2021 haiwezi kusahaulika vichwani mwa watanzania na ulimwengu wote lakini zaidi kwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kuapishwa kwakwe kushika hatamu ya kuliongoza taifa hili lililobarikiwa na Mungu kwa kila kitu kuanzia rasilimali, ardhi na watu wake waliojaa ukaribu na ukarimu.

Kwa nyakati tofauti kama ilivyo kawaida ya wanasiasa salamu za pongezi zilikuwa nyingi huku wengine wakijaribu kutabiri aina ya kiongozi atakavyokuwa katika kuendesha nchi yetu hii pendwa.

Wanasiasa wetu nchini pia hawakuachwa nyuma katika hili; pamoja na kwamba nchi yetu ilikuwa kwenye maombolezo lakini salamu za pongezi hazikuzuilika. Baadhi yao walimtabiri kuwa kiongozi mwema ambaye watanzania walikuwa wakimhitaji kwa wakati husika.

Mfano mmoja wapo alikuwa Tundu Lisu ambaye pamoja na mambo mengine alisema “… Rais Samia ni mtu ambaye ni mpole na certainly, hatakuwa kama Rais Magufuli… nitamuunga mkono mimi mwenyewe na chama changu..”

Maneno haya aliyasema punde tu baada ya Samia kuapishwa kuwa Rais wa nchi. Naamini na badhi wengine waliungana naye kwa kutoa maneno kama hayo hayo.

Kama ilivyokuwa kwa wanasiasa wa kambi ya upinzani wengine baaada ya hotuba ya Rais Samia, huyu mtu alijitokeza tena na kusema “… Mambo yote ambayo amesema atayasimamia, yote ni masuala yaliyo kwenye hotuba ya mwaka jana Novemba ya Rais Magufuli…. Kwahiyo ni hotuba ya Magufuli… Kwa hotuba hiyo demokrasia siyo ajenda yake...”

Nimekuwa ninajiuliza hivi kweli alitegemea Rais Samia angeacha yale ambayo waliyapanga pamoja na Magufuli wakati akiwa makam wa Rais wake? Au alifikiri ni awamu mpya ya uongozi? Alisahau kwamba Mama Samia amerithi mikoba kufuatia kifo cha JPM?

Inawezekana pamoja na mambo mengine kwake na wanasiasa wenye mlengo kama wake wamefikiri kuwa Rais Smia hatokuwa na msaada kwa vyama vya upinzani.

Lakini msaada gani hasa wanaoutaka? Wa kuruhusu maandamano yasiyo na tija badala ya kujikita kujenga nchi baada ya kumalizika kwa uchagizi?

Pengine inawezekana hawajamwelewa kabisa Samia ni mtu wa aina gani! Au pengine bado hata wao wenyewe hawajaelewa ni kitu gani wanachokihitaji! Au pengine hawajaielewa hotuba yake vyema?

Ndiyo maana, siku chache tangu Rais ahutubie Bunge na kutaja vipaumbele kwenye utawala wake baadhi ya wanasiasa pinzania wanachowaza na kupigia kelele ni mikutano ya kisiasa.

Je, inawezekana hata wao wenyewe hawajaelewa aina ya mikutano wanayodai? Je, ni lini kiongozi yeyote, siyo tu Rais Samia bali hata Magufuli alitangaza kuzuia mikutano ya kisiasa? Na kimsingi kama ni mikutano ya ndani ya vyama vya siasa inaruhusiwa na imekuwa inafanyika! Pia mikutano ya wabunge ndani ya majimbo yao imekuwa ikifanyika pia na imeruhusiwa. Sasa mikutano wanayodai ni ipi? Au wanataka kila siku waendeshe kampeni? Yaani wameshindwa kuelewa kwamba alichokataa Rais Magufuli ni kuifanya nchi iwe muda wote kama iko kwenye kampeni. Kwamba baada ya uchaguzi kumalizika tunapaswa kufanya kazi na kuacha siasa hadi unapofika muda wake.

Pengine inawezekana hawaelewi maana ya kile wanachokidai. Haiwezekani nchi muda wote ikae kwenye kuendesha mikutano tu badala ya kufanya kazi. Ni lini wanasiasa wetu wataelewa kwamba maendeleo hayaletwi na maneno badala ya kufanya kazi? Nchi hii inahitaji wachapa kazi na siyo wapiga debe tu.

Nilifurahishwa na maneno ya mwisho ya Rais Samia wakati wa kuhutubia bunge pale alipotoa onyo.

“Nawaonya wale wote wanaodhani kuwa usimamizi wa rasimali za umma, kusimamia ukwepaji wa kodi, kusimamia mianya ya kupoteza mapato, kukemea uzembe na wizi, yameondoka kutokana kuondoka kwa Hayati Dk Magufulli.

Mheshimiwa, Spika nataka niseme hayati mpendwa wetu ameenda peke yake, na kama nilivyosema siku ile tunamsindikiza kwamba maono, falsafa na mikakati aliyotuachia tunaendelea kufanyia kazi. Hivyo basi wale wanaodhani yale ameondoka nayo, wanajidanganya, yapo na tunayatekeleza… Nataka niwaambie kuwa mwendo ni ule ule.”

Naamini kwamba kauli hii imewavuruga vichwa wapinzani walio wengi pamoja na marafiko zao mafisadi kwa kuwa walitegemea kwamba kwa sasa mambo yatakuwa ni mteremko tu!

Kuna wakati huwa nashindwa kuwaelewa kabisa mfano wakati wa utawala wa awamu ya nne walimsema mzee wetu JK kwamba ni mpole mno, akaja JPM wakasema ni dikteta, amekuja mama Samia wanashangaa eti mbona anaendeleza yale yale ya Magufuli sasa sijui walitakaje?

Naomba nigusie pia hapa skendo ya wabunge wa viti maalumu kutoka Chadema ambao chama chao kinadai hakiwatambui japo naamini ruzuku wanapokea!

Sasa utasemaje huli nyama ya mbuzi unakunywa mchuzi? Vitu vingine tunahitaji kufikiria kwa kina. Kama wanawakana kabisa basi na ruzuku warejeshe. Mbona hatujasikia wakitangaza kurejesha ruzuku zao zinazopatikana tokana na wabunge hao?

Nilichekeshwa na mmoja wao alipokuwa anamshauri Rais Samia ati, amuite Lisu arejee nchini. Kwani ni nani alimfukuza? Yaani mtu aikimbie nchi kwa sababu kashindwa kutimiza matakwa ya mabeberu walio mtuma, eti tuhangaike kumrejesha nchini? Hii itakua kali ya mwaka.

Nafikiri kuna umuhimu mkubwa wa kuwapa semina wanasiasa wa upinzani kwamba, upinzani siyo kupinga hata pasipo na hoja ya kupinga; badala yake ni kutoa mawazo mbadala pale unapoona serikali imekwenda kinyume. Hata kama haijaende kinyume, upinzani unaweza kuja na mbadala mzuri zaidi.

Nafikiri kuna umuhimu mkubwa wa Rais Samia kubaki na msimamo wake wa kwamba yeye na Magufuli ni kitu kimoja maana watu hawa hawa wanopiga kelele sasa za kupotosha mambo ndio hao hao watakaopotosha wakati wa uchaguzi ujao wa 2025 ili wapate angalau viti vichache vya kuwaongezea ruzuku na kuwafanya waendelee kuishi mjini.

Kuna mtu mmoja kwenye mitandao ya kijamii amezungumzia pia hoja ya demokrasia inayopigiwa kelele na wapinzani, uzuri na hatari zake katika jamii kama yetu.

Anasema kimsingi demokrasia ni 'kuendeana na upepo wa wengi huku wachache wakivumiliwa na kulindwa'

Kwa mantiki hiyo anasema demokrasia iliyokomaa, maamuzi ya wengi ndio hutakiwa kutekelezwa bila kujali ni mazuri au mabaya. Aidha, ili uchaguliwe kuongoza umma, unatakiwa kuendeana na mapigo ya wengi hata kama hao wengi wanataka ufanye jambo la kijinga.

Anasema kwa bahati mbaya sana kwenye jamii yetu bado tuna watu wengi wanaopenda kushangilia ujinga kuliko mambo ya maana. Hivyo, kama Watanzania hawatapata elimu ya kutosha, inaweza kufikia wanaotaka kuchaguliwa wakajikuta wakiwajibika kufanya mambo ambayo hayaingii akilini na pengine ya kijinga ili kuridhisha kundi hili ili wachaguliwe.

Pili, anasema tunaweza kufika hatua tukakuta nchi iwe inasimamia mawazo ya ajabu kwa sababu tu ndio mawazo ya wengi.

Anasema Tanzania bado ina watu wengi sana ambao hupenda kusikia habari mbaya kutoka kwa wenzao kuliko habari za mafanikio.

“Watu hawa hupata raha sana kuona walioko juu wanashushwa chini kuliko wanavyofurahi wao wenyewe wakinyanyuliwa juu,” anasema.

Anasema, huku wapinzani wakiongoza kwa hili, Tanzania tuna watu ambao hawakubali kabisa hoja za ukweli “na ndio maana tumekuwa watu wa cheap propaganda na ndio maana hata kwenye mitandao ya kijamii mijadala ya maana haina wafuatiliaji wala wachagiaji kulinganisha na ile ya hovyo.

“Kwa hiyo katika demokrasia kamili ambayo ni upepo wa wengi, ukitaka kushika wengi unatakiwa uwe unaongea umbea, ujingaujinga na uzandiki.”

Kwamba hata Rais wa awamu ya Tano, John Magufili alipokuwa akisema ukweli mara nyingi wapenda umbea na uzandiki walikuwa hawamwelewi!

Anasema Tanzania tuna watu ambao wako tayari kumuunga mkono mtu wa darasa la saba kwa kuwa anachekesha na kumkataa profesa ambaye amefanya uchunguzi kwenye jambo la kitalaamu kwa vile anatoa ukweli ambao watu hawakuzoea kusikia!

Mtu huyo anatutaka ndugu zangu kwamba tunapozungumzia demokrasia, tuliangalie na hilo pia. Tusijilinganishe na nchi za wenzetu kama Ubelgiji au Marekani.

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili. +255-71224-6001 [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz