Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanyonge walivyojiona hii ni nchi yao

400cb503df890bed3db0539add0ed664 Wanyonge walivyojiona hii ni nchi yao

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAREHE 1, Februari mwaka huu nikiwa njiani kutoka Dodoma kuelea Dar es Salaam katika shughuli binafsi, niliamua kupita sehemu kupata chakula na wenzangu.

Wakati tunasubiri kwenye gari, akapita mzee mmoja ambaye kimsingi alionekana kachoka sana. Kwa kumwonea huruma, mwenzangu akamwita ili tumpe fungu la kumi letu.

Cha ajabu yule mzee hakuitika haraka kuchukua fungu hilo la kumi. Baada ya kumwita tena mara ya pili kwa kusisitiza alikuja na kupokea fungu hilo.

Cha kushtua ni kwamba neno lililotoka ndani ya kinywa chake baada ya kupokea fungu hilo alisema: ‘Mmemsaidia Magufuli”. Kwa wakati huo sikuelewa maana ya kauli ile nzito.

Nilijiuliza mzee yule aliamaanisha nini bila mfanikio. Mwenzangu niliyekuwa naye alikuwa Profesa lakini naye alibaki akijiuliza maana ya sentensi ya yule mzee aliyoitoa huku akitutazama usoni. Kisha akashika njia yake na kuondoka.

Wakati naendelea kutafakari kauli ile ili niiandikie makala, mara tarehe 17 Machi, taifa likapokea habari nzito, habari ya mshtuko mkubwa kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kwamba niliyeambiwa kumsaidia na yule mzee ambaye hata sikupata jina lake, Dk Magufuli hatunaye tena.

Iliniuma sana, machozi yasiyo na kifani yalinitoka kama maji. Sikuona aibu kulia hata mbele ya watu kwa kuwa niliumia sana. Hata kama ningeona aibu nisingeweza kwa sababu nilikuwa sina uwezo wa kuzuia machozi.

Ratiba za kuaga mwili wa Hayati Magufuli ndizo zilizonipa majibu ya ajenda ya yule mzee aliyonipatia. Kitendo cha vikundi vya mama lishe, machinga na wafanya biashara ndogo ndogo kulia wakiuliza ni nani atawapigania tena viliashiria ya kwamba Hayati Magufuli alikuwa na mtazamo wa kuwasaidia maskini wa Tanzania kwa kuwatengenezea mazingira ya kufanya biashara zao bila bugdha yoyote.

Nikakumbuka kauli yake aliposema: “sijaona sheria yoyote Tanzania inayozuia mama lishe au baba lishe kuuza chakula barabarani.”

Pengine yule mzee alimaanisha kwamba kila mtendaji wa serikali anawajibu wa kumsaidia mtanzania wa hali ya chini kwa nafasi aliyo nayo? Au pengine alimaanisha kwamba Hayati JPM alikuwa na jukumu kubwa la kuwahakikishia watanzania wote mlo mzuri na uhakika wa kuishi pasi na shaka?

Najiuliza kwamba au pengine alimaanisha kwamba JPM alikuwa na jukumu kubwa la kuwafikia watanzania wote walio na maisha duni sana? Au pengine alimaanisha JPM alikuwa na kazi kubwa na kwamba asingeiweza peke yake bali alihitaji kuwahimiza wasaidizi wake kutimiza majukumu ya kuwasaidia watanzania wote kwa kadri wanavyoweza!?

Mara nyingi viongozi wakubwa hupenda kuwaridhisha tabaka fulani la watu hasa walio mijini, wasomi na wafanyakazi ambao huwa ni wachache lakini kelele zao husaidiwa na mitandao ya kijamii na hivyo kuonekana wako wengi!

Lakini tofauti na aina hiyo ya viongozi JPM alitamani kumgusa kila mtanzania. Kila mradi ulioanzishwa ulilenga kuwasaidia watanzania walio wengi na bila shaka hili ndilo lililofanya watu wengi wampende.

Unaweza kusikia watu wakilalamika kwamba hajaongeza mishahara, lakini hili kundi la wafanyakazi ni dogo sana kulingana na Watanzania walio wengi ambao alikuwa ‘bize’ kuhakikisha wanapata maji salama, wanapata barabara na matibabu.

Kuna mtu aliwahi kuandika kwamba alipokuwa akiishi Kimara kabla ya Magufuli kuingia madarakani alikuwa anatumia kati ya Sh 150,000 hadi 200,000 kwa mwezi kununua maji kwenye maboza lakini baada ya kupatiwa maji ya uhakika ya bomba na serikali ya JPM, wanatumia kati ya Sh 15,000 hadi 25,000 tu kwa mwezi.

Mtu huyo akahoji: “Sijaongezwa mshahra lakini hatua hiyo ya kupata maji na gharama za maji kupungua ni kama nimeongezewa mshahara zaidi ya Sh laki moja kwa mwezi.”

Ni wazi kwamba Magufuli aliwafanya watanzania waione nchi kama ni yao yaani alirejesha nchi mikononi mwa wananchi wenyewe na kuwafanya wajione kuwa sehemu ya nchi yao katika utoaji wa maamuzi.

Alirasimisha biashara ambayo awali ilionekana siyo rasmi. Jambo hili lilithibitishwa na Mzee wetu mstaafu Ali Hassan Mwinyi katika hotuba yake siku ya mazishi aliposema: “amestawisha uwekezaji na ufanyaji biashara nchini kwa kurahisisha mawasiliano. Hata masoko makubwa yameanza kuchipuka kama uyoga nchini mwetu. Kijana wetu huyu ameondolea wamachinga fedheha ya kuwingwa kando za barabara…

Rais huyo mstaafu akaendelea: “Ni kweli mwana huyu anaheshimu na kuhurumia wanyonge, nani angepata taabu yote hiyo? Lakini amewainua. Machinga amewaondolea manyanyaso ya kuwindwa kama ndege watundu…”

Pengine ndiyo maana ya kauli ya ‘umemsaidia Magufuli!’ Bado naendelea kutafakari.

Kilichichonishtua kingine ni hiki. Mnamo tarehe 24 mwezi Machi nikiwa kituo cha mabasi ya mikoani, nikapata nyepesi kwamba siku mbili nyuma yake mama lishe walifukuzwa kituoni hapo na walinzi wa kituo hicho cha mabasi hadi mkurugenzi wa kituo alipoingilia kati na kuamuru waachwe waendelee kujitafutia riziki.

Pengine wale walinzi walighafilika siku hiyo. Au pengine kuna aliyetaka kuharibu ratiba ya kuaga mwili wa Hayati Magufuli! Mama lishe mmoja wakati tunapiga stori akasema walilia wakisema mbona mnatunyanyasa hata baba yetu kabla hajazikwa? Nahisi hilo ndo lilimshtua mkurugenzi wa kituo.

Kauli ya yule mzee bado inaniandama hasa baada ya kifo cha jembe letu, shujaa wa Afrika kutokea. Je, inawezekana ukawa mwisho wa yale yote ya JPM kwa watanzania hawa wanyonge waliokuwa na imani kubwa naye?

Lakini Rais wetu mpya, Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri. Tuna imani kwamba hatoirejesha nchi kwenye uozo ule uliozoeleka kabla ya ujio wa JPM.

Kwamba watanzania hawa maskini hawawarejea maisha ya kuishi kwa shida tena, machingwa wakiwandwa utadhani majambazi.

Nilifarijiwa sana na hotuba yake wakati wa kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) tarehe 28 Machi iliyofanyika Ikulu Chamwino.

Hatua yake ya kuchukua hatua dhidiya uongozi wa Mamlaka ya Bandari ilionyesha kwamba yuko tayari kuendeleza kasi ya JPM, mintarafu suala zima la kulinda raslimali za nchi na ubadhirufu.

Pengine anaweza asiwe na lugha ya ukali kama JPM lakini maneno yake na tafsiri ya uso wake (facial expression) yalionyesha wazi kwamba suala la rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma hatolifumbia macho.

Huu ni mwanzo mwema kwa Rais wetu. Pengine, anahitaji muda ili aweke serikali yake sawa na pia watendaji wamsome na kuendana na kasi yake. Pengine, hotuba yake atakayotoa bungeni kwa wakati atakaoamua pia itazidi kutoa mwanga zaidi wa nini anachokwenda kuwafanyia Watanzania.

Wakati kama huu natambua mabeberu watakuwa wamefumbua macho yao kuona mchezo unavyokwenda ili waweze kujipenyeza na wakati mwingine watatumia ‘ma-double agent’ ambao ni watanzania wenzetu wasio na nia njema na nchi yetu kutekeleza ajenda zao mbaya. Kinachohitajika ni kushikamana na kuenzi misingi aliyoiacha JPM.

Nakumbuka maneno ya JPM ya kwamba katika kila jambo tumtangulize Mungu na pia tuitangulize Tanzania kwanza. Natambua ya kwamba wapinzani wetu kiuchumi na vibaraka wa mabeberu wanapenda kuandika mabaya kuliko mema ya nchi yetu kwa kuwa na mrengo wa uliberali lakini kama alivyosema Rais Samia wakati wa hotuba yake pale Dodoma kwamba tunahitaji kuwa wamoja katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote.

Tanzania ni yetu sote, tuipende, tuilinde kwa maslahi ya watanzania wote. Mungu atusaidie katika kipindi hiki kigumu.

Columnist: www.habarileo.co.tz