Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Wanawake tuache kukumbatia ukatili’

76fd356dacf4ec91c0b1f9ae5cb3c619 ‘Wanawake tuache kukumbatia ukatili’

Tue, 15 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“WANAWAKE tuache kukumbatia ukatili.” Haya ni maneno mafupi lakini yenye ujumbe mzito anayoyarudia rudia Pili Kuliwa, Katibu wa asasi ya kiraia inayotetea haki za wanawake na watoto ya Tumaini Jipya la Wanawake Kilwa (Tujiwaki).

Akizungumza katika hitimisho la maandamano ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyojiri mwishoni mwa wiki, wilayani Kilwa, Pili anasema kama wanawake wakijitambua na kupaza sauti wataacha kuukumbatia ukatili.

Katika maadhimisho hayo, Tujiwaki ilitembelea kata tatu kwa ajili ya kutoa elimu ya kujitambua na kuhimiza wanawake kupaza sauti na siyo kufumbia macho ukatili wa kijinsia.

Anasema wanawake hasa wa Pwani wamekuwa wakijiendekeza kukaa nyumbani na kusubiri baba alete kitu chochote na yeye akipokee na wengine wamekuwa wakikaa kimya dhidi ya ukatili wanaofanyiwa uwe wa kisaikolojia, kingono ama kupigwa huku wakisema ‘hewala’.

“Huwezi kuwa unateseka katika nyumba unayoishi halafu, wakati mwingine baba anabaka watoto na unaishia kusema ‘Ahh atajua mwenyewe’,” anasema.

Mwanamke huyo anafafanua kwamba kuna mashauri mawili ya wazazi kutembea na maharimu wao chini ya miaka 13 na kuficha kadhia hizo.

Anasema hali ya ukatili Kilwa haipendezi na wanawake wamekuwa wakikubali kukaliwa na mfumo dume bila kutafuta njia ya kuukabili na kushawishi wanaume watambue kuwa wao ni wenza wao na wala si maadui wao wanaostahili kunyanyaswa na kubughudhiwa.

Ili kuacha kukumbatia ukatili, Pili anasema wanawake wanastahili kuanza kutumia sauti zao kuhakikisha wanapambana kuwa na maisha yenye msimamo, pamoja na kuwa na uhakika wa kutunza familia zao.

“Tatizo kubwa la Kilwa ni wanaume kuwanyanyasa kiuchumi wanawake,” anasema na kufafanua kwamba mali zinazochumwa kwa pamoja mara nyingi mwanaume huzing’ang’ania na kuzitumia binafsi wanawake kubaki mithili ya watumwa.

Anasema kimsingi wanawake ndio wanaohangaika na kilimo lakini mazao yakishauzwa yanaingizwa kwenye akaunti ya mwanaume na yeye anayeamua matumizi ya pesa husika.

Katika majadiliano wakati wa kilele cha siku ya kupinga ukatili mwaka huu kwamba hata mali kama nyumba na mashamba yanaponunuliwa huandikwa jina la mume pekee badala ya wote wawili, hatua ambayo humnyima haki mwanamke ingawa mambo hayo hufanyika wakati wa ndoa.

“Wengine wakishauza korosho au ufuta anamwambia mama, naenda mjini kutafuta bidhaa, kumbe anaondoka na mwanamke mwingine. Akirejea nyumbani hana hata zawadi na bidhaa zenyewe hazipo, mke akiuliza talaka ipo mlangoni,” anasema Pili Kuliwa.

Anasema huo ndio unaitwa ukatili wa kiuchumi ambapo wanawake wakiwa ndio wazalishaji wakubwa wa mali mashambani lakini wanaume ndio wanafaidi na waki mara nyingi wakibembelezwa kwa kuletewa khanga na kitoweo.

Tujiwaki katika tafiti zake inasema ni mali hizo na fedha zilizochangiwa na mwanamke, kutumiwa na mwanaume wakati mwingune kuolea mwanamke mwingine!

Anasema wanaume wanaogopa wanawake wenye uwezo kwa kujituma na kujitambua.

Anasema wanaume wamekuwa wakitumia umaskini wa wanawake kama fimbo ya kuwachapia, fimbo ambayo inaleta maamivi zaidi hasa kwa wanawake ambao hawana cha kufanya zaidi ya kusubiri mume alete kitu nyumbani.

Kwake, ukatili wa kiuchumi ni sehemu tu ya ukatili mwingi unafanywa dhidi ya wanawake, ukatili ambao unaweza kuondoka kwa elimu na kuwaweka pamoja wanawake katika utetezi wao.

Anasema changamoto zinazowakabili wanawake na watoto ndizo zilizofanya wanataka wanawake kuacha kukumbatia ukatili na badala yake wajitokeze na kuusema hadharani wakiupinga.

Ukatili mwingine anasema ni ndoa za utotoni zinazosababishwa na tamaa, huduma dhaifu za umma na ukware wa wanaume na utelekezaji wa familia.

Kuzagaa kwa watoto mitaani katika mji wa Kilwa Masoko na hata Kilwa Kivinje kunatajwa huenda kukawa kunasababishwa na tamaa.

“Watoto wengine katika umri mdogo kwenye makundi yao wanaambiana kuhusu watu wanaoweza kuwasaidia kupendeza, wanajivua utu wao kwa tamaa ya mali na mara wanajikuta wana mimba na hawasemi mpaka wamebanwa,” anasema Pili.

Anasema mara nyingi wazazi wamekuwa hawafikishi masuala hayo polisi bali wanamalizana na baada ya muda mtoto na mtoto wake wanaachwa solemba.

Kuhusu huduma dhaifu za umma Pili anajielekeza kwenye huduma za maji. Anasema sehemu kubwa ya wilaya ya Kilwa haina maji ya uhakika, hivyo wanawake na watoto huhangaika sana kutafuta maji.

Anasema watoto wanajikuta wanaingia kwenye kishawishi au kubakwa kutokana na shughuli ya kutafuta maji kuifanya wakiwa peke yao bila wazazi wao.

“Mama anatoka shamba anahangaika anakuwa na ndoo moja ya maji, ndoo hiyo haitoshi anamtuma mtoto wake, mtoto naye anachukua hali hiyo kama fursa,” anasema Kuliwa

Pia watoto kwa kuwa peke yao, wamekuwa wakijitumbukiza katika tamaa za kimwili kwa kushindwa kudhibiti mihemko na kutaka mteremko katika maisha.

Kwa kutoa elimu kwa wanawake na watoto Pili anaamini kutawafanya wanawake kujitambua na kutambua matendo ya ukatili wa kijinsia, kupinga na kutofanya unyanyasaji kwani wapo pia baadhi ya wanawake wanafanya visa hivi kwa wanaume.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Grace Mwambe, akizungumza katika kilele cha siku 16 kupinga ukatili mjini Somanga, anasema wanawake wanapaswa kushikamana iwapo watataka kukabiliana ipasavyo na matatizo yanayowakabili, kujitambua na hata kumwelekeza mwenza namna ya kuishi vyema.

Ofisa huyo anawataka wanawake kujiamini na kudai haki zao za msingi wanapohisi hawapewi. Anasisitiza kwamba katika hilo inatakiwa busara kubadili mwendo wa mume na jamii kwa upole na kutambua nafasi ya kila mmoja katika malezi.

“Ndoa ni makubaliano, ndoa ni urafiki basi sote tuwe marafiki kwa heshima na mazingira. Tuwaweke hawa wanaume karibu nasi kwa kutekeleza wajibu wetu kwa upendo,” anasema Grace wakati akizungumzia wajibu na fadhaa ya familia kutokuwa pamoja kutokana na matendo na mazingira ya wanakaya.

Anasisitiza kwamba wanawake hawatakiwi kuwa nyuma bali mbele kupambania haki zao ziwe za kindoa, kifamilia au kiuchumi.

Ingawa wazo la kupinga ukatili kwa pamoja lilikuwa hadharani mwaka 2009, na hasa kutokana na ukimya wa wanawake katika madhila yanawasibu, Tujiwaki imezidi kupata mafanikio na mwaka huu pekee katika kampeni yao ya kupinga ukatili ambayo imewafikia watu 8,700 kupitia njia mbalimbali ikiwamo mikutano, makongamano, semina na vipindi katika Radio Mashujaa.

Elimu iliyotolewa inalenga kuwezesha namna ya kujitambua na kupaza sauti.

Mabango mengi yaliyokuwa katika maandamano ya amani Somanga yaliyoshirikisha kata nne zikiwemo za Somanga, Miteja, Kivinje na Masoko yalikuwa yanaeleza ukatili wa aina mbalimbali ambao unaotokea katika wilaya hiyo ukiwamo wa kisaikolojia ambapo matusi na dharau huelekezwa kwa mwanamke na kutelekezwa kwa watoto.

Mmoja wa wanawake walioshiriki katika maandamano hayo, Salma Mohamed anasema kwamba jukumu la malezi ni la watu wawili; hivyo wazazi lazima washirikiane kulea watoto wao.

Salma anapinga vikali tabia ya wanaume ya kuacha wake zao na kutekeleza familia wakiamua kujipatia nyumba ndogo.

Naye Sijali Juma anasema kwamba matusi ya nguoni kwenye vijiwe wanayopachikwa wanawake yanaleta ghadhabu kubwa na kudhalilisha wanawake hivyo lazima vijana wajitambue na kuheshimu watu wengine iwe kwenye vijiwe au kwenye maeneo ya kazi hasa sokoni.

Katibu wa Tujiwaki, Kata ya Somanga, Husna Kikope akizungumza na wanawake wenzake alielezea haja ya wanawake kujikomboa wenyewe na kujipangia mikakati ya maendeleo na wala si suala la kuwezeshwa.

“Hali hii itatufungua minyororo na sisi kusonga mbele katika kutafuta haki zetu na za familia zetu,” anasema Kikope.

Akizungumzia kampeni wanazofanya sasa Theodora Mkundi, mwenyekiti wa Tujiwaki alisema kwamba wanachosambaza wao ni maarifa ya kubadilisha maisha ya wanawake na mwonekano wao katika jamii akiwataka wasimame imara kujenga Kilwa mpya yenye amani na maendeleo.

Anasema wilayani Kilwa, ukatili wa wanaume unajionesha zaidi katika umiliki wa mali, dharau katika ustaarabu wa kuishi pamoja na hulka za kupenda kuoa kila wakati mali inapoongezeka katika familia.

Pamoja na kuwapo na haja ya tafiti za kutosha kubaini kwamba wanawake wanahitaji msaada mkubwa wa kisheria ili kukabili ukatili uliopo sasa ukiwamo wa kisaikolojia, kupigwa, kunyima fedha alizozalisha mwenyewe na kutelekezewa watoto, wakati wanaume wanapoenda kuoa wake wengine mara tu baada ya msimu wa mavuno, bado jukumu la kujiondoa katika kadhia hii ni la wanawake wenyewe, wakiacha kukumbatia ukatili.

Columnist: habarileo.co.tz