Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanasoka na majeraha ya funiko la mguu

Rooney Injury Wanasoka na majeraha ya funiko la mguu

Fri, 22 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa wale wafuatiliaji wa soka kupitia Redio Tanzania neno funiko la mguu ni kawaida kulisikia kwa watangazaji mahiri wa mpira wa enzi za miaka ya 1980 na 1990 kina Charles Hillary, Aboubakar Liongo na Ahmed Jongo.

Mfano ulikuwa unaweza kusikia akisema anakanyagwa katika funiko la mguu au anapiga shuti kali la chinichini kupitia funiko la mguu.

Eneo hilo ni eneo nyeti kwa mwanasoka likiwa pamoja na kifundo cha mguu ambalo hutumika kusakata soka ikiwamo kwa mitindo ya kupiga mashuti, kukaba, kuruka, kukimbia na kucheza faulo.

Eneo hili ndilo ambalo hutumika kupiga mpira ya frii-kiki au mashuti mara kwa mara na vile vile ni eneo ambalo hukanyagwa kirahisi wakati wa mikikimikiki ya uwanjani ikiwamo kukabana kwa kutumia nguvu nyingi.

Moja ya majeraha yanayowapata wanasoka katika eneo hili mara kwa mara ni tatizo la kuvunjika au kupata nyufa kwa vifupa vidogo vidogo vilivyopo katika mguu wa chini.

Tatizo la uvunjikaji vifupa ya miguuni ndilo linalowaweka nje wanasoka kwani si tu kuvunjika bali pia huambatana na vijeraha vya tishu laini katika eneo hili hatimaye kuchelewa kupona.

Mastaa wa miaka ya nyuma wa Ligi Kuu England ambao waliwahi kupata tatizo hili la kuvunjika vifupa vya miguuni ni pamoja na David Beckham, Ashley Cole, Wayne Rooney, Steven Gerard na Jack Willshere.

Vifupa vya funiko na majeraha yake

Vifupa hivi hujulikana kitabibu kama metarsasal, vikiwa na idadi ya vifupa vitano. Kabla ya vifupa hivi huanza vifupa vya mwanzoni ambavyo ndivyo vidole vya mguuni.

Wakati wa kutembea, kukimbia kuruka na kutua, kifundo huweza kutua vibaya na kujipinda hivyo kujeruhi mfupa na tishu laini ikiwamo nyuzi ngumu ambazo hujivuta kupita kiasi na kusababisha kupata majeraha.

Majeraha haya yanaweza kusababisha kuleta nyufa katika mifupa, kututumka kwa mfupa na kuvunjika vifupa vidogo ikiwamo ile ya vidoleni mwa mguu. Uwapo wa mejaraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogo vidogo huweza kuambatana na majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu.

Kurudia kutumia funiko la mguu kupiga mpira ni mojawapo ya jambo linalochangia kutokea kwa majeraha ya funiko la mguu pamoja na kifundo cha mguu kwa ujumla. Vile vile kujirudia kuchezewa faulo eneo la kifundo kunachangia majeraha ya mara kwa mara ya eneo hili. Ni vigumu kwa mwanamichezo anayeshiriki michezo kukwepa kuchezewa faulo.

Kundi la kwanza kitabibu huitwa pharenges ipo sehemu ya mbele ambayo ni mifupa ya vidole vya mguu na huku sehemu ya nyuma hupakana na kundi la kundi jengine la mifupa itwayo tarsal.

Makundi haya matatu ya mifupa ya mguu yaani sehemu ya chini ndio inaunda sehemu inayojulikana na wanasoka kama funiko. Sehemu hii ndio tunayotumia kupiga mpira mara nyingi.

Makundi haya ya mifupa ya miguu sehemu ya chini huweza kuunda maungio madogo kwa vifupa hivi kuungana kama vile mnyororo.

Endapo shinikizo litakuwa kubwa kiasi kwamba litazidi uwezo wa mifupa hii kustahimili ndipo majeraha ya kunjika yanapojitokeza. Unaweza kuvunjika mfupa mmoja kama ama ikavunjika zaidi ya miwili.

Kuvunjika kwa mifupa hii kunatofautiana katika eneo la mfupa, ukubwa wa jeraha na aina yake ikiwamo kapata nyufa, kutawanyika vipande vipande, kuvunjika na kutoka nje ya ngozi, kupasuka na kugawanyika au kutogawanyika sehemu mbili, kuvunjika na pande mbili kupishana na kupinda.

Chanzo kuvunjika metatarsal

Mara nyingi hutokana na mambo ambayo yapo kila siku katika soka ikiwamo kifundo cha mguu kujivingirisha au kujipinda, kuchezewa faulo, kuruka na kutua vibaya.

Pia majeraha haya yanaweza kutokea pale unapokuwa unakimbia na kuruka na kubadili mwelekeo wa ghafla kama ilivyo katika mchezo wa soka.

Vilevile mifupa hii inaweza kuvunjika endapo kutakuwa kuna shinikizo la mara kwa mara katika eneo hilo na pia endapo kutakuwa kuna matumizi yaliyopitiliza ya mguu pasipo kupumzishwa.

Dalili na viashiria

Mgonjwa kuhisi maumivu makali ya ghafla, kuhisi hali ya mguu kuvuta na kujaa. Mjeruhiwa anaweza kuhisi mlio wa kuvunjika wakati wa tukio la kumjeruhi wakati linapotokea.

Maumivu huwa makali kiasi cha kumfanya mgonjwa kuchechemea au pengine akashindwa kuhimili uzito wa mwili na kutoweza kuukanyagia mguu.

Maumivu haya huwa na kawaida ya kuongezeka nyakati za usiku na asubuhi sana. Mguu huweza kuwa na viashiria vya michubuko, kuvimba na kuumia pale unapomgusa eneo hilo. Maumivu hayo yanatoneseka na kuhisi kuuma pale anapojaribu kuutembelea na mguu huo.

Kama jeraha la kuvunjika litakuwa kubwa kiasi kwamba mfupa uliovunjika kuhama kabisa eneo lake umbile la mguu seheme ya funiko huweza kuonekana lisilo la kawaida.

Uchunguzi na matibabu

Baada ya mjeruhiwa kufikishwa katika kituo cha afya au vituo maalum vya tiba ya wanamichezo ndipo huduma nyingine za juu hufanyika.

Vipimo vya picha ya xray hutumika kuthibitisha kama kuna kuvunjika na pia kujua ukubwa wa jeraha

Vipimo vya juu zaidi vya baadaye ambavyo ni picha za uchunguzi zinazotoa picha nzuri zaidi za majeraha ikiwamo MRI na CT.

Kama ni kuvunjika kwa katikati ya mfupa na kuifanya mifupa ipishane matibabu huwa ni njia isiyo ya upasuaji ambayo mguu huvutwa na kunyoosha kuendana na umbile asilia la mguu.

Mbinu hii inaurudishia mfupa mahali pake na baadaye kuimarishwa kwa kutumia kiatu maalum ili mguu usitetereke au kufunga P.O.P fupi majuma kadhaa kati ya 6-8.

Kama kuvunjika kwa mfupa hakutahusisha kupishana kwa pande mbili zilizovunjika matibabu yanaweza kuhusisha uvikwaji kifaaa maalum mguuni au kupewa kiti maalum cha kutembelea ili kuulinda mguu usiutumie kukanyagia.

Upusuaji hufanyika ili kuweza kuunganisha mfupa huo kwa kutumia vyuma tiba ambavyo huwa ni pini, waya na screw maalum zinazopachikwa.

Majeruhi wa aina hii hutakiwa kupumzika sana na kutojihusisha na chochote ikiwamo kukimbia, kutembea na kuruka. Kupumzika kunachangia jeraha kuunga haraka na kupona mapema.

Kupuuza na kutojali maelekezo baada ya maumivu kupotea na kuanza kuufanyisha kazi mguu kunaongeza ukubwa wa tatizo na kuchelewesha kupona.

Majeruhi huwekwa katika vituo kwa ajili ya uangalizi maalum ili kupewa program maalum za mazoezi tiba yasiyosababisha maumivu ikiwamo ya kunyoosha eneo hilo na mazoezi ya kuuweka mguu uweze kuwa sawa.

Wataalamu wa mazoezi ya viungo hutoa huduma kama za uchuaji na usingaji, uimarishaji wa ungio, tiba ya kuchua kwa vifaa vya umeme na uvikaji vifaa maalum katika jeraha ili kuutuliza mguu.

Chukua hii Mara nyingi majeraha ya mifupa hii yana matokeo mazuri, mchezaji huweza kupona kabisa na kurudi uwanjani kuendelea na soka.

Columnist: Mwanaspoti