Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanasiasa heshimuni vyombo vya habari

SIASA Wanasiasa heshimuni vyombo vya habari

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu ukiendelea kushika kasi, joto limeanza kupanda kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo.

Takribani vyama vyote vyenye ushindani mkubwa kwenye uchaguzi huo, vimezindua rasmi kampeni. Vingine viko mbioni kuzindua kampeni ikiwa ni ishara ya kuwaandaa na kuwashawishi wananchi kuvichagua.

Hata hivyo, historia ya waandishi wa habari katika kushiriki kampeni hizo, mara kadhaa imeingia dosari kutokana na baadhi ya vyama, kuwa na tabia ya kuwapiga na hata kuwafukuza kwenye mikutano yao.

Miaka ya nyuma chama kimoja cha siasa, kiliwapiga waandishi wa habari na kuwajeruhi vibaya huku wengine wakinusurika na vitendea kazi vyao vikiharibika, kutokana na madai ya kutoridhika na namna walivyoripoti habari za chama hicho.

Hali hiyo imekuwa ikiwaweka waandishi wa habari katika hali ya tahadhari wanapohudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa.

Ikumbukwe kuwa kazi ya mwanahabari katika kampeni hizo za uchaguzi ni muhimu, kwa kuwa ndio kiunganishi kikubwa kati ya wanasiasa hao na wapigakura wao kupitia ripoti na uchambuzi wao wa sera za chama husika.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, dalili mbaya zimeanza kuonekana kutoka kwa wanasiasa dhidi ya wanahabari, ambapo chama kimoja cha siasa kilifukuza chombo cha habari kimoja katika mkutano wake wa kampeni, kwa madai ya kutoridhishwa na namna chombo hicho kilivyorusha matangazo ya mkutano huo.

Jambo moja ambalo wanasiasa wanatakiwa walifahamu ni kwamba siku zote chombo cha habari huendeshwa kwa kuzingatia sheria za nchi, sera ya chombo husika na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Tanzania kama ilivyo nchi nyingi za Afrika, vyombo vya habari huendeshwa kwa nadharia ya uwajibikaji kwa jamii, kwa maana ya kwamba kuna mfumo wa kisheria na sheria lukuki za vyombo vya habari, zinazodhibiti mfumo mzima wa uhabarishaji.

Pamoja na kwamba suala la sheria hizo linaendelea kupigiwa kelele na wanataaluma, lakini bado haiondoi ukweli kuwa sheria hizo zipo na ndizo zinazodhibiti vyombo hivyo vya habari na endapo chombo kitaenda kinyume, hatua stahiki huchukuliwa dhidi ya chombo hicho.

Moja ya sheria hizo ni kubana maudhui yanayorushwa na vyombo hivyo ambayo yanahatarisha amani ya nchi. Hivyo, ni wazi kuwa chombo chochote kitakapoona mtoa habari anaenda kinyume na sheria hizo, lazima kichukue hatua ya kujilinda.

Itoshe kueleza kuwa wanasiasa wanapaswa kufahamu kuwa hakuna chombo chochote cha habari duniani, siyo Tanzania pekee, kinachoruhusu matangazo au taarifa za matusi, kejeli na uchochezi.

Na ili chama au mwanasiasa aweze kuripotiwa ipasavyo kwenye kampeni zinazoendelea, hana budi kuhakikisha kuwa kampeni zake ziwe zimeshiba sera na maono yake kwa watanzania na si shutuma, matusi , kashfana kejeli dhidi ya wanasiasa wengine kinyume na maadili.

Kama ambavyo, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa Habari Tanzania (TEF) Deodatus Balile alivyosisitiza kuwa wanahabari kazi yao si kushiriki kwenye siasa, bali kazi yao ni kueleza wananchi chama kitawafanyia nini. Anasema TEF inasikitishwa na kitendo cha chombo hicho kufukuzwa katika mkutano wa kampeni, wakati kikiwa kinatimiza wajibu wake.

Columnist: habarileo.co.tz