Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanaosimamia foleni kwenye daladala waungwe mkono

Foleni Dar Es Salaam Wanaosimamia foleni kwenye daladala waungwe mkono

Sun, 23 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA kituo cha mabasi ya daladala cha Mbezi Mwisho katika halmashauri ya Ubungo jijini Dar es Salaam, inaonekana misururu mirefu ya watu. Ni abiria waliopanga mistari mitatu tofauti wakisubiri kuingia kwenye vyombo vya usafiri wa umma.

Mstari wa kwanza ni wa abiria wanaopanda mabasi ya ‘mwendo kasi’ kwa ajili ya kusafirishwa hadi kituo cha Kimara tayari kwa kwenda maeneo mbalimbali hususani Kariakoo, Kivukoni na Morocco.

Inafahamika na imezoeleka kwa abiria wa mabasi hayo hupanga foleni katika kituo hicho cha Mbezi Mwisho, hata kabla ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayotokana na virusi vya corona (covid-19) kulipuka nchini Mstari wa pili na wa tatu ni mgeni machoni mwa wengi.

Foleni moja ni ya abiria wa daladala zinazofanya safari kati ya kituo hicho cha Mbezi Mwisho na Tandika kupitia Barabara ya Morogoro.

Nyingine ni ya abiria wanaopanda daladala zilizotengeneza ruti kwenda Kariakoo kwa nauli ya Sh 1,000.

Wanaonekana vijana (wapiga debe) wakisimamia kwa umakini foleni hizo. Taarifa zinasema kwamba vijana hao wa kujitolea, kila wanapokamilisha kusimamia daladala kujaza abiria, wanajipatia Sh 1,000 (bila shaka wanagawana).

Utaratibu huo mpya umeleta ustaarabu miongoni mwa abiria juu ya suala zima la kuingia kwenye daladala. Umeondoa ubabe na mabavu yaliyokuwa yakitumika miongoni mwa abiria kiasi cha wengine kuingilia madirishani.

Chini ya utaratibu huo, ina maana wa kwanza kukfika kituoni ndiye wa kwanza kupanda basi na kuondoka tofauti na hali ilivyokuwa kituoni hapo. Kutokana na nguvu kubwa iliyohitajika kupanda magari hayo, wale wasio na nguvu walijikuta wakikaa kituoni hata zaidi ya saa mbili.

Wajawazito, wenye watoto, wenye ulemavu na wazee ndiyo waathirika wakubwa kwa usafiri huo usio wa ustaarabu. Kwa jumla, abiria wasio na nguvu hawakuwa na uhakika wa muda wa kuondoka kituoni.

Isitoshe, katika purukushani ya kuingia kwenye mabasi, wapo walioibiwa fedha na vitu hususani simu za mkononi. Hali iligeuka kuwa mbaya zaidi baada ya Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji Ardhini (Latra) kutangaza kuanza kwa utaratibu wa abiria kukaa kwenye mabasi kulingana na idadi ya viti kwenye daladala.

Kutokana na uchache wa daladala, kituoni hapo paligeuka uwanja wa vita kutokana na kila abiria kupigania kuingia awahi kwenye shughuli zake. Nikirejelea hali ilivyokuwa, nashawishika kupongeza ubunifu wa sasa wa kuingia kwenye daladala kwa foleni.

Wale wenye ‘vifua’ vya kugombania usafiri, inawezekana wakaona si utaratibu mzuri kutokana na kulazimika kupanga foleni. Maana kutokana na uwezo wa kupigania, hao wenye nguvu hawakukaa muda mrefu kituoni.

Walitumia nguvu zao na kujikuta wakitangulia kuingia huku abiria wengine wakibaki kituoni muda mrefu bila kujua hatma yao. Kama ambavyo wengi wa watumiaji wa daladala wanashauri utaratibu wa ‘level seat’ uwe endelevu, vivyo hivyo kupanga foleni kuhalalishwe kwa kusimamiwa ipasavyo na mamlaka zinazohusika na usafiri huu wa umma.

Pongezi ziwafikie vijana hawa waliojitolea kusimamia utaratibu huu ambao wengi walitamani kusikia mamlaka zikihimiza ufanyike na kuusimamia. Vijana hawa waungwe mkono na utaratibu uhalalishwe kwa vituo vyote hususani kwenye ruti ambazo zimezoeleka kuwa na abiria wengi wanaolazimika kugombania kuingia kwenye daladala.

Aidha, wakati JICHO langu likihimiza Latra na mamlaka nyingine kukaza uzi juu ya level seat kwenye daladala, vile vile zitafute suluhisho la kudumu la tatizo la usafiri huu hususani kwa abiria walio katika vituo vya njiani.

Suluhisho la kudumu liwe ni la kufanya mapitio ya namna walivyopanga ruti za daladala na wakati huo huo waendelee kukaribisha usajili zaidi wa magari ya kutoa huduma ya usafirishaji abiria kwenye njia zenye kero kubwa ya usafiri. Lengo liwe ni kufanya usafiri huu uwe wa ustaarabu.

stella.nyemenohi@tsn. go.tz

Columnist: habarileo.co.tz