Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wananchi walivyoloa ndani na nje ya uwanja Lupaso

IMG 4176 Yanga 1 2 Usm.jpeg Wananchi walivyoloa ndani na nje ya uwanja Lupaso

Wed, 31 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilianza kuwa siku mbaya kisoka kwa Wananchi pale walipoamka na mvua usiku wa kuamkia juzi. Ikaenda kuwa siku mbaya wakati shabiki wao mmoja alipokata kauli wakati akigombea kuingia uwanjani katika kile kinachoitwa kugombea kuingia uwanjani bure. Nashauri tuachane na soka la bure.

Siku ikawa mbaya wakati wachezaji wa pande zote mbili, Yanga na USMA Alger waliposhindwa kuonyesha uhodari wao katika uwanja uliojaa utelezi. Mpaka leo wanatuachia swali, hali ingekuaje kama uwanja ungekuwa katika ubora wake? Hatuwezi kujua.

Vyovyote ilivyo, kwa kile ambacho tulikiona kutoka katika mabao matatu safi ya pambano hilo ni wazi kwamba Yanga walistahili kupoteza mchezo. USMA Alger walipoteza nafasi za wazi kuliko wao. Walistahili kuondoka na ushindi walioupata kutokana na namna walivyoumiliki mchezo na kupoteza nafasi. Kama wangekuwa makini katika kuzitumia si ajabu fainali ingeishia Temeke.

Bao la kwanza. Limekuwa tatizo la nchi kwa sasa. Yanga na Simba wote wamekuwa wepesi kuruhusu mabao ya mipira ya kutengwa au faulo. Katika bao hili kipa mahiri wa Yanga, Djigui Diarra anahusika. Alipaswa kujua mpira utaangukia wapi walau auguse na kuupoteza mwelekeo. Hakufanya hivyo. Mpira ulipigwa nyuma yake.

Kama yeye alikuwa hajajipanga vizuri basi walinzi wake wawili walikuwa hawajajipanga vizuri zaidi. Waliruka na mfungaji lakini walichelewa. Sio mara ya kwanza. Yanga imeruhusu mabao mengi ya aina hiyo katika michuano hii. Waliruhusu mabao mawili ya Monastir pale Tunis na wakaruhusu bao moja dhidi ya Real Bamako pale Bamako.

Baada ya hapo Yanga wakaanza kazi nzito ya kujaribu kurudi mchezoni. Walijikuta wakicheza 10 kwa muda mwingi wa dakika 45 za kwanza. Kisa? Aziz Ki. Tangu aje nchini Aziz amekuwa akipunguza sauti za wanaomponda kwa kufunga mabao kadhaa muhimu. Lakini ukweli Aziz Ki huyu sio yule wa ASEC Mimosas ambaye aliilazimisha Yanga imfanye mchezajj anayelipwa zaidi nchini.

Unaweza kuwa na siku mbaya katika soka lakini ukweli ni kwamba Aziz anajitakia mwenyewe siku mbaya. Anapoteza mipira mingi kiurahisi kwa kutaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Hata kurahisisha mpira. Mbinafsi. Lakini zaidi ni kwamba hana msaada kwa timu pale ambapo inakuwa haina mpira.

Wakati ule anasajiliwa kwa mbwembwe na Yanga haikufikirika kwamba siku moja Mudathir Yahaya angewez kuwa mchezajj muhimu kikosini kuliko yeye. Wakati ule akisajiliwa kwa mbwembwe zote zile Mudathir alikuwa kwao Forodhani Zanzibar akipishana na watalii bila ya kazi.

Upande wake kulia katikati ambao anapenda kucheza ulikufa. Winga wake, Tuisila Kisinda naye akawa hana madhara kama kawaida yake. Alikuwa na mbio nyingi ambazo hazikuwa na madhara kwa wachezaji wa USMA Alger. Kilichowapa Yanga uhai ni upande wa kushoto ambako Fiston Mayele na Kennedy Musonda walikuwa wanatokea.

USMA Alger walionekana kuwa miongoni mwa timu bora za michuano ya CAF ambazo zimecheza Temeke katika msimu huu. Jumlisha hata na akina Wydad Casablanca, Monastir, TP Mazembe na wengineo, USMA Alger walikuwa bora zaidi uwanjani kwa namna walivyocheza.

Hawakujihami, hawakujiangusha bila ya sababu na walikuwa bora katika umiliki wa mpira na kupanga mashambulizi yao. Bao lao la kwanza lilikuwa la mpira uliokufa lakini wangeweza kufunga mabao kadhaa katika muvu za kawaida tu. Walistahili kuondoka katika dakika 45 wakiwa na uongozi.

Katika kipindi cha pili ilishangaza kuona Aziz Ki akirudi uwanjanj. Mara nyingi tunafahamu kwamba kocha Nasireddine Nabi akirudi na Aziz uwanjani. Lakini zaidi ni kwamba hakufanya mabadiliko yoyote ya haraka tofauti na tulivyomzoea. Yanga ikaendelea na mashambulizi ya kubahatisha mpaka pale mtu anayeamua mambo yao magumu kwa njia ngumu alipofanya mambo yake. Fiston Kalala Mayele.

Alisawazisha bao zuri ambalo lilikuwa gumu. Namna alivyoutuliza mpira kifuani na kupiga kwa haraka inamfanya Mayele awe mmoja kati ya washambuliaji wachache hatari wanaocheza soka la ndani barani Afrika. Sijui ataendelea kubakia Tanzania mpaka lini lakini natabiri kuna wakubwa wataitaka saini yake mara baada ya pambano la marudiano pale Algeria.

Columnist: Mwanaspoti