Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wametua TPL jioni kabisa

SAIDO001 Saido Ntibanzokiza

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dirisha la usajili kwa klabu za Tanzania Bara, lilifungwa usiku wa Agosti 31 huku ikishuhudiwa Yanga ikimrudisha nyumbani, Tuisila Kisinda aliyekuwa akiichezea RS Berkane ya Morocco ambayo ilikuwa ikinolewa na Florent Ibenge aliyehamia kwa sasa Al Hilal ya Sudan.

Tetesi za Kisinda kuachana na Berkane zilianza kuzagaa kipindi kiungo Clatous Chama alipoamua kurejea zake Simba, awali winga huyo mwenye kasi alikuwa akihusishwa na Azam FC lakini mabosi wake wa zamani wakaona si mbaya kumrudisha kundini.

Achana na Kisinda, hapa chini ni nyota wengine waliosajiliwa dakika za mwisho na kuingia kwenye klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara bila hata kutarajiwa kama ilivyokuwa kwa Mkongoman huyo aliyetarajiwa kuwasili nchini alfajiri ya leo kuungana na nyota wemzake wa Yanga.

RAJAB ZAHIR

Licha ya Singida Big Stars katika eneo lake la beki ya kati kuwa na Pascal Wawa, Biemes Carno, Daudi Mbweni na Abdulmajid Mangalo, imeamua kumuongeza kundini Rajab Zahir Mohammed ambaye amewahi kuhudumu kwenye klabu hiyo.

Zahir aliyecheza Ligi Daraja la Kwanza ambalo kwa sasa linafahamika kama Championship akiwa na Singida BS amerejea nyumbani, atakuwa na kibarua cha kupigania namba mbele ya Wawa na Biemes ambao wamekuwa wakianza kwenye kikosi cha kwanza cha Hans van der Pluijm.

Baadhi ya timu alizowahi kuzitumikia beki huyo wa kati kwa vipindi tofauti ni pamoja na  Mbeya City, Stand United, Yanga SC na Ruvu Shooting.

TUISILA KISINDA

Wakati akiondoka Jangwani mashabiki wa Yanga waliumizwa kwani alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi chao, ilikuwa ngumu kwa viongozi wa timu hiyo kuwagomea RS Berkane na kwakuwa mchezaji alionyesha nia ya kuondoka walimfungulia milango.

Baada ya kutoka kwa taarifa kuwa Kisinda ameamua kuachana na waajiri wake hao wa zamani (Berkane), Yanga ilimfungulia milango tena ya kumkaribisha nyumbani Jangwani.

Licha ya Yanga kuwa na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni, vigogo wa timu hiyo iliwabidi kuitana fasta na kukaa vikao ili kufanya maamuzi juu ya nani akatwe kati ya Jesus Moloko (DRC), Lazarous Kambole (Zambia), Heritier Makambo (DRC) au Gael Bigirimana (Burundi) kabla ya muafaka kupatikana usiku mnene.

Nasreddine Nabi atakuwa na uwanja mpana wa kufanya machaguo ya nani aanze kwenye winga ipi, wapo ambao wameanza kuvuta picha ya winga moja akicheza Kisinda huku nyingine akiwa Bernard Morrison mbele Aziz Ki na Fiston Mayele nini kitatokea? muda utaongea.

SAIDO NTIBANZOKIZA

Godfader wa Bujumbura, Saido Ntibanzokiza naye ni kati ya wachezaji ambao sajili zao zilikuwa za jioni licha ya kwamba uvumi kuwa anaweza kutua Geita Gold ulikuwa ukivuma kwa kipindi kirefu huku mazungumzo yakichukua nafasi kwa zaidi ya wiki.

Uzoefu wake unaweza kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikiongozwa na George Mpole ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.

MESHACK SELEMAN

Inawezekana likawa jina geni kwa mashabiki wengi wa soka la Tanzania lakini ni mmoja wa wachezaji wa Kitanzania ambao wamekuwa wakifanya vizuri nje ya nchi akiwa na Nyasa Big Bullets ya Malawi.

Ni winga msumbufu hivyo mabeki wa pembeni wajipange, anaweza kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ya Maafande wa Tanzania Prisons ambao msimu uliopita haukuwa mzuri kwao.

MOHAMMED HASSAN

Anatajwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kati huko Uganda, ni shupavu mwenye uwezo wa kutumia nguvu na akili, amewahi kupata shavu la kuichezea timu yake ya taifa kabla ya kuamua kuja kucheza soka la kulipwa Tanzania.

Hassan anapewa nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Mbeya City ambayo msimu uliopita iliwafanya mashabiki na wadau wa soka Mbeya kujivunia wao kutokana na kufanya kwao vizuri wakati wenzao Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza zikitaabika.

JOEL MADONDO

Wakati zikihesabiwa saa kabla ya dirisha la usajili kufungwa, Polisi Tanzania ilinasa saini ya mshambuliaji, Joel Madondo kutoka timu ya Singida Big Stars kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Nyota huyo raia wa Uganda alikamilisha dili hilo baada ya kupitia kipindi kigumu cha kucheza kwenye timu yake kutokana na ushindani wa namba huku ikielezwa yeye mwenyewe aliomba kuondoka ili akatafute changamoto mpya sehemu nyingine.

Mbali na Singida, Madondo amewahi pia kucheza klabu mbalimbali kama Hippos FC ya kwao Uganda pamoja na Wydad Casablanca ya Morocco.

Tofauti na usajili huo ila klabu hiyo pia imekamilisha usajili wa beki wa kati Mkenya, Sosteneth Idah aliyetokea Coastal Union na beki wa kulia, Blanchard Ngabonziza kutoka Aigle Noir FC ya Burundi.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz