Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wamesepa na mabao

Saido Simba Ths Wamesepa na mabao

Thu, 29 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Januari 15 dirisha la usajili Ligi Kuu Bara linafungwa baada ya kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu, tayari baadhi ya timu zimefanya usajili kuboresha vikosi.

Wakati timu zikipambana kuboresha vikosi kupitia dirisha dogo la usajili kuna baadhi ya timu zimebomolewa na baadhi ya mastaa wamejikuta wanahama timu na kuibukia kwingine.

Dirisha hili limeibua vicheko na simanzi kwa baadhi ya timu, wengine wamekuwa na vicheko huku wengine wakiwa na huzuni kuondokewa na mastaa waliofanya kazi kubwa.

Kuhama kwa mastaa hao ambao pamoja na mchango mkubwa waliouonyesha ndani ya timu wameamua kusepa na mabao yao na asisti.

Mwanaspoti linakuletea orodha fupi ya nyota waliohama na mabao yao kutoka timu moja hadi nyingine, baadhi wakitimka kabisa kwenye Ligi Kuu kama utani vile.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’

Kiungo mshambuliaji huyo mkongwe, ndiye aliyekuwa nahodha msaidizi na tegemeo ndani ya Yanga, lakini ghafla tu ametangaza kasepa zake na inaelezwa anaelekea Azam FC ili kukipiga ndani ya timu hiyo.

Fei Toto amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka mitatu na fundi huyo mkali wa mashuti ya mbali, majuzi alizua sekeseke baada ya kuelezwa ameilipa timu hiyo ili aweze kuvunja mkataba, ameondoka Yanga akiwa ameipachikia timu hiyo mabao sita katika mechi 17 akicheza 15. Hakuna anayejua ndani ya Azam FC atafanya nini, lakini kutokana na uwezo alionao ana nafasi ya kuingia kikosi cha kwanza moja kwa moja kama dili lake litafanikiwa.

SAIDO NTIBAZONKIZA

Mshambuliaji wa Burundi, Saido Ntibanzokiza ambaye Geita haitamsahau kutokana na uwezo na rekodi alizoziacha ndani ya timu hiyo, amevunja mkataba na matajiri wa dhahabu Geita Gold na kujiunga na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Kiungo huyo mshambuliaji fundi wa mipira iliyokufa amefanya uamuzi huo na juzi alionekana akiwa jukwaani wakati Simba wakiichapa KMC mabao 3-1 kwenye Dimba la CCM Kirumba.

Straika huyo ameondoka Geita Gold na mabao yake manne na asisti sita akihusika kwenye jumla ya mabao kumi kati ya 18 yaliyofungwa na timu yake ya zamani Geita akiwa ameichezea mechi 12, sasa ataanzia hapo akiwa na uzi mwekundu na mweupe.

GEORGE MPOLE

Straika wa zamani wa Geita Gold, Mpole alivunja mkataba wake wa miezi sita na timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Saido, ambaye walikuwa wanakipiga pamoja kwenye timu hiyo.

Mpole alivyovunja mkataba alipata dili la kujiunga na FC Lupopo ya Congo, straika huyo aliondoka kwa matajiri wa dhahabu akiwa amewafungia mabao mawili.

Mpole ambaye alimaliza kinara wa mabao msimu uliopita akifunga mabao 17, msimu huu amezifunga timu mbili tu kabla ya kutimka Ligi Kuu akiifunga Polisi Tanzania timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 na Singida Big Stars timu yake ikilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani.

NICKSON KIBABAGE

Kitasa wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ pamoja na udogo wa umri wake amebahatika kupata uzoefu mkubwa kwenye soka akipata bahati ya kutoka nje ya Tanzania na kwenda kujaribu soka la kulipwa nchini Morocco, ambako alishindwa kudumu.

Achana na stori hiyo, Kibabage ni beki haswa alikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar, mbali na jukumu lake la kukaba alikuwa ni mchezaji wa kupandisha mashambulizi na kufunga.

Msimu huu amekuwa miongoni mwa mabeki waliofunga mabao mengi zaidi, ambapo ametupia manne kwenye ligi kuu hadi sasa ambayo ametimkia nayo Singida United, akiwa Mtibwa alizifunga Namungo mechi ikimalizika kwa sare ya mabao 2-2, Ihefu FC akiiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 na alitupia dhidi ya Mbeya City wakimaliza dakika 90 kwa sare ya mabao 2-2.

WENGINE

Juma Mahadhi wa Geita Gold naye amesepa katika timu hiyo na kutua Coastal Union akiwa na bao moja kama ilivyo kwa Yusuph Kagoma aliyekuwa Geita Gold aliyeamua kurejea Singida Big Stars ambapo aliitumikia Singida United ile ya enzi zile. Pia, wamo Adeyum Saleh aliyekuwa Geita Gold na kuondoka na bao lake kwenda kucheza Dodoma Jiji sawa na Silvino da Cruz aliyetimkia nchini kwao Brazil na Dejan Georgijevic ambaye alivunja mkataba wake na Simba na kwenda kwao Serbia.

Columnist: Mwanaspoti