Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wamechapika! mastaa wa ndondi vinara wa kupigwa nje

Twaha Kidukuu Mastaa wa ndondi vinara wa kupigwa nje

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati baadhi ya mabondia kama Dullah Mbabe, Ibrahim Class na Tony Rashid wakiwa na historia ya kutwaa mikanda ya ubingwa ya kimataifa wakicheza ugenini nje ya nchi, mambo yamekuwa magumu kwa ‘ndugu’ zao wengi ambao wamekuwa na rekodi kubwa ya kupigwa nje ya nchi kuliko kushinda.

Mbabe, Class na Tony wamefata nyayo za kaka zao, Rashid Matumla ‘Snake Man’ na Karama Nyilawila waliowahi kuwa mabingwa wa dunia wakizichapa nje ya nchi enzi zao.

Bondia namba moja nchini, Hassan Mwakinyo pia anaigia kwenye rekodi hiyo, ambayo aliiweka mwaka 2017 alipomchapa kwa TKO, Anthony Jarmann na kuwa bingwa wa WBA Pan African kwenye uzani wa super welter huko Gaborone, Botswana.

Pia pambano lake na Sam Eggington lilikuwa gumzo duniani, japo halikuwa la ubingwa, lakini kipigo cha Technical Knock Out (TKO) nyumbani, kwa Eggington aliyekuwa bondia namba moja nchini Uingereza na namba nane wa dunia kilimjengea heshima Mwakinyo nje ya nchi.

Class yeye alitwaa ubingwa wa dunia wa GBC kwenye uzani wa super feather huko Ujerumani alipomchapa Jose Forero mwaka 2017 wakati Tony akitwaa ubingwa wa Afrika (ABU) nchini Afrika Kusini miaka mitatu iliyopita.

Mbabe ambaye jina lake halisi ni Abdallah Pazi aliweka heshima hiyo nchini China alipomchapa Zulipikaer Maimaitiali kwa TKO mwaka 2020.

Nyota hao ni miongoni mwa mabondia wachache nchini wa kizazi cha sasa waliowahi kutwaa mikanda ya ubingwa kwenye mapambano yao ya nje ya nchini.

Wakati miamba hiyo ya Tanzania ikifanya yao ugenini, mastaa hawa wanaingia kwenye orodha ya mabondia vinara wa kupigwa kwenye mapambano yao ya nje ya nchi.

TWAHA KIDUKU

Katika mapambano yake manane aliyopigana nje ya nchini, amepigwa mara saba, pambano moja akipigwa kwa Technical Knock Out (TKO) na yaliyosalia kupigwa kwa pointi.

Pambano la Mei 20, 2021 ndilo lilikuwa la mwisho kwa Kiduku kuzichapa nje ya nchini na kupigwa kwa pointi na Bek Nurmaganbet huko Lokomotiv Arena, Novosibirsk, Russia.

Mapambano mengine aliyopigwa ni pamoja na lile la Misri dhidi ya Ulugbek Sobirov, lile la Ismail Iliev huko Jurmala, la Roman Zakorov nchini Russia na la Lukasz Wierzbicki huko,Radom Poland.

Kipigo kingine ni dhidi ya Kudratillo Abdukakhorov huko Tashkent na kile cha Przemyslaw Runowski huku akiwa na rekodi ya kushida kwa KO huko Lusaka, Zambia alipomchapa Mbiya Kanku.

MFAUME MFAUME

Staa huyu na bondia namba mbili nchini kwenye uzani wa super welter anaingia kwenye orodha ya vinara wa kuchapika nje ya nchi.

Katika mapambano yake saba aliyopigana kwenye nchi mbalimbali, Mfaume hajawahi kushinda tangu 2016 alipopigana pambano la kwanza nje ya nchi na kupigwa kwa TKO na Gabor Ventor huko Berne, Switzerland.

Rekodi hiyo iliendelea kwenye pambano na Rizvan Elikhanov huko Russia na lile la Abay Tolesh la Dubai, Falme za Kiarabu alikopata matokeo kama hayo.

Kipigo kingine ni dhidi ya Joshua Clottey nchini Ghana, cha Vaghinak Tamrazyan huko Vladimir, Russia na kile cha 2017 alipochapwa kwa KO na Georgii Chelokhsaev nchini humo huku Mikka Shonena akimpiga kwa pointi huko Windhoek, Namibia.

FRANCIS MIYEYUSHO

Mkongwe huyu ni miongoni mw mabondia waliopigana mara nyingi nje ya nchi na kupigwa mara nyingi zaidi, Miyeyusho au Chichi mawe kama anavyopenda kujiita katika mapambano 16 aliyopigana nje, amepigwa mara 13 na kushinda mara tatu.

Mara ya mwisho kucheza nje ya nchi ilikuwa ni 2018 alipochapwa kwa TKO na Sachin Dekwal huko Faridabad, bondia huyo pia amechapwa Ujerumani na James Cherej.

Wengine waliomchapa ni Martin Parlagi, Macbute Sinyabi, Gottlieb Ndokosho, Vyacheslav Gusev Luke Wilton, Thangthong Klongjan, AJ Banal, Zolani Tete, Nick Otieno, Andrei Isayeu na Isaac Ward.

Katika mapambano ya nje, ana rekodi ya kumchapa Amos Ogutu nchini Kenya, Khatyza Sanashokov na kutoka sare na Sebastian Bytyqi.

BAINA MAZOLA

Staa huyu wa ndondi kutoka kwenye moja ya kambi maarufu jijini Dar es Salaam hajawahi kushinda nje ya nchi, katika mapambano yake matatu yote amepigwa kwa TKO.

Mara ya mwisho kuchapwa ilikuwa ni mwanzoni mwa mwaka huu aliporuhusu kipigo huko Dubai dhidi ya Frank Zaldivan, amewahi kukutana na kipigo kama hicho dhidi ya Evgeny Smirnov na kupigwa kwa kuokolewa na mwamuzi nchini Afrika Kusini dhidi ya Koos Sibiya.

COSMAS CHEKA

Ni miongoni mwa mastaa wanaotamba nchini, Cheka ambaye ni mdogo wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka amepigwa mara nyingi zaidi ya kushinda kwenye mapambano yake ya nje ya nchi.

Kwenye mapambano 10, amepigwa mara sita na kushinda mara nne katika nchi tofauti ikiwamo Kenya na DR Congo kwa Afrika, igawa nje ya Afrika pia amechapika mara kadhaa.

Cosmas ambaye Oktoba atapanda ulingoni huko Poland dhidi ya Radomir Obrusniak, mara ya mwisho kushinda nje ya nchi ilikuwa ni 2018 alipomchapa Geoffrey Nyamu nchini Kenya, kabla ya pambano hilo aliwachapa Kenneth Kidenga, Aphinan Rengron na Felesianu Albino.

Akicheza ugenini,Cosmas amechapwa na Bebe Rico Tshibangu huko Kinshasa, DR Congo, Ayanda Nkosi (Afrika Kusini), James Chereji (Ujerumani), Zoltan Kovacs, Mosses Paulus na Vyacheslav Gusev.

SAID MBELWA

Kwa kizazi kinachocheza ngumi kwa sasa, Mbelwa anaweza kuwa kinara wa kupigwa mara nyingi zaidi nje ya nchi ambako amepigwa mara 21 katika mapambano 22.

Mara ya mwisho aliruhusu kipigo cha TKO huko Moscow, Russia mwaka 2022 dhidi ya Artur Ter Israelyan, huku akiwa na rekodi ya kuchapwa na Nikita Solonin, Wuzhati Nuerlang, Batal Chezhia, Ainiwaer Yilixiati, Robert Parzeczewski, Rohan Murdock, Thomas Oosthuizen, Farouk Daku, Denis Ronert na Brijesh Meena.

Wengine ni Imre Szello, Farouk Daku, Sergel Ekimov, Vikapita Merroro, Bernard Donfack, Tamas Kovacs, Balazs Kelemen, Bilel Latreche, Amid Rahimi na Agron Dzila huku akimchapa Ken Oyolo huko Kisumu, Kenya.

MADA MAUGO

Katika mapambano 11 ya nje ya nchi, Maugo ameshinda dhidi ya Caleb Amianda na George Owano kwa TKO huko Kenya na Lubumbashi, DR Congo dhidi ya Dyson Mwisa.

Amepigwa Russia kwa KO na Batal Chezhia, alikutana na matokeo kama hayo dhidi ya Ainiwaer Yilixiati huko Zhengzhou na kingine dhidi ya Movsur Yusupov nchini Russia.

Wengine waliomchapa ni Stanislav Kashtanov, Aliklych Kanbolatov, Khetag Kozaev, Anton Novikov na Vincent Vuma katika nchi tofauti.

“Ngumi bado zina ile ‘Mtu kwao’ ni ngumu sana kushinda nje ya nchi, labda ushinde sana, kinyume na hapo ni ngumu sana kupata ushindi ukicheza nje ya nchi,” anasema Maugo.

Anasema nje ya nchi bondia mgeni ukicheza na kumaliza raundi zote hushindi, labda umpige mwenyeji haswa kuanzia raundi ya kwanza hadi ya mwisho.

“Ndio sababu unaona hata wageni wakija kucheza nchini hawashindi, labda iwe KO au TKO, lakini mkimaliza raundi zote, wenyeji kukupa ushindi ni nadra, bado kuna ile Mtu kwao.

“Hao wenyeji wako ndio wanakutumia tiketi, wanakulipia kula na kulala na kila kitu kwa ajili ya pambano hilo wanakugharamia, hivyo lazima gharama hizo ukazifanyie kazi haswa na ili ushinde ukaze umpige mwenyeji KO, TKO au umpige kuanzia raundi ya kwanza hadi ya mwisho, kinyume na hapo hushindi,” anasema Maugo.

Cheka bingwa wa zamani wa dunia wa WBF anasema ngumi za kulipwa ni biashara, ni kama mchezo wa nipe nikupe, hivyo hadi bondia ashinde anapokwenda kupigana huko, lazima ajipange ipasavyo.

Columnist: Mwanaspoti