Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Walioteuliwa wasibweteke

9a8923e9ced180b2031a0f34503b2b2b Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Sun, 9 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri jana. Katika mabadiliko hayo, baadhi ya mawaziri na manaibu waziri wameondolewa na kuweka wapya huku wengine wakihamishwa wizara.

Chini ya mabadiliko hayo Rais Samia amebadilisha muundo wa wizara tatu, amewabadilisha wizara mawaziri tisa na wakati huo huo kuwapa uwaziri kamili manaibu waziri watatu.

Vile vile amefanya uteuzi kwenye nafasi za Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu na baadhi uteuzi wao umetenguliwa kwa kuingiza wapya. Tunapenda kuwapongeza wote walioteuliwa hususani wapya na wakati huo huo tukiwapongeza walioendelea kuaminiwa na Rais na kupewa nafasi hizo nyeti kutumia wananchi.

Lakini pia kwa upande wa walioachwa, tunawapongeza kwa kipindi walichoshiriki kutumikia Taifa katika nafasi hizo nyeti. Kwa kuwa Rais ameona ipo haja ya kuingiza watu wengine kwenye gurudumu la hili la maendeleo ya nchi, viongozi walioondolewa waendelee kutumikia nchi bila kinyongo kwa nafasi nyingine walizo nazo.

Tunaamini uteuzi huu umefanyika kwa nia moja ya kuhakikisha anapata wasaidizi watakaoshirikiana naye katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

Kama alivyosema hivi karibuni alipokuwa akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19, Rais Samia anachotazama kwa sasa ni maendeleo ya Watanzania.

Kwa kuwa matamanio ya Rais ni kuona nchi inapaa kimaendeleo kwa maslahi ya wananchi, tunawaasa wote walioteuliwa kuonesha utumishi uliotukuka kwa kuchapa kazi.

Sote tunashuhudia mikakati mbalimbali inayowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha si tu inakuza uchumi wa nchi bali inakuza uchumi huo hadi kwa wananchi .

Kwa hiyo timu hii iliyoaminiwa na Rais haina budi kufanya kazi kwa bidii kutimiza malengo yake kwa Watanzania. Inawapasa wateule hawa wadhihirishe kwamba lengo la Rais Samia kuwateua ni kupata utendaji thabiti kwa maana ya kutoa huduma iliyotukuka ili wananchi waendelee kuiamini na kuipenda serikali yao.

Kinachotegemewa kwenye mabadiliko haya, ni wateule kuchapa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi. Kama alivyowahi kusema wakati akiwaapisha mawaziri wapya kwenye mabadiliko mengine madogo aliyowahi kufanya, uteuzi wa hawa wachache hauna maana kwamba wao ni wazuri kuliko wengine.

Nasi tunasisitiza kwamba uzuri wa wateule hawa, utaonekana katika kazi kwa vitendo na si kwa maneno. Tunaendelea kuwapongeza tukihimiza wakachape kazi kwa nguvu zao zote.

Columnist: www.habarileo.co.tz