Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waliorejea shule, vyuoni wajihadhari corona bado ipo

CBE Waliorejea shule, vyuoni wajihadhari corona bado ipo

Tue, 2 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JANA wanafunzi wa vyuo na wa kidato cha sita walirejea vyuoni na shuleni, baada ya serikali kuruhusu kutokana na kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa, Machi 17, mwaka huu ilitangaza hatua mbalimbali za kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa huo, ikiwamo kuzifunga shule na vyuo, kwa lengo la kuepisha misongamano hadi itakapotangazwa tena, baada ya kasi ya maambukizo kupungua.

Hata hivyo, takribani wiki mbili zilizopita, Rais John Magufuli alitangaza kufunguliwa kwa vyuo na kidato cha sita Juni Mosi (jana), ili wanafunzi wa kidato hicho wanaokabiliwa na mitihani ya taifa kujiandaa.

Rais Magufuli alifanya uamuzi huo ikiwamo kuruhusu kurejea kwa michezo hususan Ligi Kuu, FA Cup, Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili, huku akifanya uchambuzi wa takwimu mbalimbali katika hospitali nchini zilizokuwa zikionyesha kasi ya kupungua kwa wagonjwa.

Wanafunzi hao kukaa muda mrefu nyumbani takribani miezi mitatu kutakuwa kumeathiri kwa kiasi fulani programu za masoko kwa wanafunzi, walimu na wahadhiri.

Hata hivyo, tunaamini kuwa menejimenti za vyuo na shule zitabuni na kutekeleza mipango na mikakati mizuri kuhakikisha kwamba programu za masoko zilizopangwa kufundishwa zinakamilishwa bila kusababisha athari zozote.

Tunawashauri wanafunzi na wanavyuo kutambua kuwa wana kazi ya ziada ya kufidia viporo vya masomo. Jambo la kufanya ni kusoma kwa bidii na kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi wa taasisi zao.

Kikubwa ambacho tunashauri kwa taasisi hizo na wanafunzi ni kutambua kuwa bado ugonjwa wa corona upo, hivyo kuchukua tahadhari zote muhimu ambazo zinaendelea kutolewa na wataalamu wa afya.

Kwa kuwakumbusha baadhi ni kunawa mara kwa mara kwa kutumia maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kutumia vitakasa mikono (sanitizer). Tahadhari nyingine ni kukaa umbali wa angalau mita moja, kuepukana na misongamano, kuepuka kushikana mikono na kubusiana.

Uongozi wa vyuo na shule umeshapewa maelekezo na serikali kupitia mwongozi uliotolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, hivyo tunatarajia kuona tahadhari zote zikiwekwa kwa kipindi chote cha tishio la maambukizo.

Tunatarajia kuona taasisi hizo ziliweka ndoo zenye maji tiririka, sabuni, vikatasa mikono vikiwekwa katika milango ya kuingilia na hata ndani ya ofisi, mabweni, vyooni na maeneo mengine.

Vile vile, itakuwa vizuri kama taasisi hizo zitakuwa zikiwapima joto la mwili wanafunzi, wafanyakazi na watu wengine wanaoingia ndani.

Upo umuhimu pia wa wataalamu wa afya kwenda katika taasisi hizo kufuatilia kama maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya yanatekelezwa, na pale itakapobainika vinginevyo, hatua kali za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Kadhalika, tunaona kuwa kuna umuhimu wa wataalamu wa afya kuweka utaratibu wa kwenda kutoa elimu na msisitizo kwa wanafunzi kuendelea kuchukua tahadhari. Ni matarajio yetu kuwa kila mmoja aliwajibuka na kuzingatia maekelezo ya wataalamu wa afya, ugonjwa huo tutaushinda, na tutavuka salama.

Columnist: www.tanzaniaweb.live