Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Walau Afrika tungekuwa na kauli moja kwa Covid-19

050ad0ebfece0372f05798d2ae1fb372 Walau Afrika tungekuwa na kauli moja kwa Covid-19

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

DHANA ya uzalendo ni pana sana na wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kutafsiriwa. Lakini kwa minajili ya makala haya ‘Uzalendo’ ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini, kuisitiri na kujitoa kwa ajili ya nchi yake.

Mzalendo wa kweli daima anaweka maslahi ya nchi mbele na ya kwake binafsi nyuma. Kwa maana hiyo, mzalendo ni mtu yeyote mzawa na mwenye kuipenda na kujitoa mhanga na saa nyingine ikibidi kufa kwa ajili ya nchi yake kwa maslahi ya wananchi walio wengi.

Uzalendo unabeba dhana nyingi sana ikianzia asili, utamaduni, lugha, siasa, historia, na mambo kadha wa kadha. Dhana zote zikifungwa kwenye dhana kuu ya utaifa.

Kuwa mzalendo ni zaidi ya kuifia nchi yako. Kwa sababu aidha kwa uzembe au kwa ujinga au kwa imani yake mtu aweza kufa lakini kumbe hakuipenda nchi ila kwa matakwa yake binafsi.

Shinikizo la kuifia nchi ni lazima liwe tunda la uaminifu, upendo wa kujitoa, kuipigania na kuitetea nchi yako. Wako wazalendo ambao wameitetea nchi yao toka utotoni, ujanani na uzeeni na hawakuifia nchi.

Watu wasio wazalendo ni hawa hapa: watu wanaoihujumu nchi kwa kuiba, kutumia rasilimali za nchi vibaya, kuharibu miundombinu, kuweka pesa nje ya nchi, kuisema vibaya nchi na viongozi au watu wake, kushabikia wizi na ufisadi, kuvunja sheria za nchi, kuthamini vitu na mambo kutoka nje na mengine mfano wa hayo.

Unaweza kweli ukawa mzawa, mwaminifu, mkweli lakini unakuwa kimya watu wanapoiba na kutumia vibaya rasilimali za nchi, wewe pia sio mzalendo kwa mfano huo.

Mara nyingi watu wengi hutumia neno la uzaledno kupotosha maana halisia ya dhana hii kwa wananchi. Wakati wa kupigania uhuru wa mataifa ya Afrika, kilichokuwa kinawaongoza na kuwasukuma wapigania uhuru ni uzalendo. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na wenzie walikuwa na uzalendo wa dhati kabisa kabisa kupigania utaifa na kuulinda utaifa wetu japo tu kwa njia ya amani ama vita.

Wakati huo lengo kubwa lilikuwa ni kutoa nchi zetu chini ya utawala wa mkoloni na kuleta maendeleo kwa waafrika wote kwa ujumla.

Wakati ule wapigania uhuru wote wa Afrika walikuwa na dhana sawa ya ‘utaifa’ wa Afrika. Na karibia kizazi cha kipindi cha umajumui kilikuwa na mitazamo sawa ya kumuondoa mkoloni Afrika na kuliunganisha Bara la Afrika ili kuifanya nchi moja yenye nguvu ya kuweza kupambana na mataifa makubwa ya kibeberu.

Hata hivyo, dhana ya usaliti ndani ya Afrika baina ya waafrika wenyewe haikuanza leo wala jana la hasha! Ilikuwepo hata kipindi cha mkoloni. Dhana, hii ikapelekea kuuawa kwa baadhi ya wanamajumui waliokuwa na lengo moja tu kuiunganisha Afrika. Walifanya vile tu kujinufaisha wao na mtumbo yao (wasaliti).

Kwa usaliti huo ndoto za kuliunganisha Bara la Afrika na kulifanya taifa moja ikaota mbawa. Wanamajumui wa kipindi hicho wakaanza kupigania uhuru wa nchi zao ambazo kipindi kile zilianzishwa na mkoloni kwa lengo pana sana la kuligawa bara la Afrika na hakika kwa kiasi fulani walifanikiwa.

Afrika ikashindwa kuungana na kuwa taifa moja lakini wana majumui wa kipindi kile kama vile Hayati Baba wa Taifa, Kwame Nkrumah na wengineo wakashirkiana kupigania uhuru wa nchi zao na mataifa megine ya Afrika.

Hata baada ya kupata uhuru kwa mataifa yaliyo mengi Afrika bado kiu ya kutaka Afrika kuungana na kuzungumza lugha moja kwa mataifa yote bado imeonekana kuota mbawa. Jambo ambalo linapelekea hata baadhi ya viongozi wa sasa kupata shida kuzungumzia dhana hii.

Mwanzoni mwa utawala wa Rais John Magufuli alizungumzia sana dhana hii ya kuunganisha bara la Afrika na kiu yake aliionyesha wazi ya kutaka bara hili liungane ili kupigana na mabeberu lakini kama ilivyokuwa enzi hizo hadi sasa bado umoja wa Afrika haujagusa vichwani mwa walio wengi.

Inawezekana kiu ya Magufuli ndiyo inampelekea wakati wote avae bendera ya Afrika ili kuonyesha wazi ndoto yake. Hata hivyo, kama ilivyokuwa enzi hizo bado hajaeleweka. Pengine kiongozi pekee anayeweza kumuelewa kipindi hiki kuhusu umajumui wa Afrika ni Mzee Museveni Yoweri Kaguta wa Uganda; ambaye kwa nyakati tofauti amaweka wazi msimamo wake juu ya kuungana kwa Afrika na kutengeneza masoko yao ya ndani dhidi ya yale ya mabeberu.

Kwa hali inavyokwenda inawezekana kizazi cha sasa kikawa kisaliti zaidi kwa dhana ya Utaifa wa Afrika kuliko hata kizazi cha usaliti wa kipindi cha umajumui. Siyo kwa sababu ni kizazi kilichokosa elimu la hasha! Ni kwasababu ni kizazi kilichojifunza uozo mwingi kuliko ubora.

Ni kizazi kilichojifunza ubinafsi kuliko ushirikiano, ni kizazi kilichokulia kwenye mazingira ya utengano kuliko muungano. Siyo kwamba jamii zee iliyopo sasa ni mbaya sana, hapana ni mazingira ya kibeberu yaliyopelekea yote haya.

Sitashangaa, miaka ijayo baadhi ya mataifa ya Afrika kujifanya sehemu ya mataifa beberu. Dhana ya usaliti wa waafrika wenyewe kwa wenyewe ilipelekea kuuawa kwa Kanal Muamar Gadaffi. Ndiyo dhana hiyo hiyo iliyotamani kumwondoa Rais Museven wa Uganda katika uchaguzi uliopita; na ndiyo dhana hiyo hiyo inafanya Rais Magufuli atumie nguvu nyingi katika kipindi cha uatwala wake.

Nashukuru kwa wasaidizi wake wa karibu kama Makamu wa Rais Mama Samia na Waziri Mkuu, Kasimu Mjaliwa Majaliwa wanamuelewa na kuendeleza maono yake vyema.

Kwa lengo la kuhusanisha kichwa cha makala haya, tangu kugundulika kwa ugonjwa wa COVID-19, mataifa mengi hasa ya Asia, Ulaya na Amerika yameonyesha kuathirika sana huku baadhi ya mataifa ya Afrika yakionyesha kukabiliana na janga hili linalosumbua ulimwengu vyema zaidi.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi wa Afrika, walijitokeza na kuonyesha dhamira yao ya kutaka kutumia dawa za asili katika kukabiliana na gonjwa hili. Hata hivyo, mataifa ya kibeberu yalionyesha dhahiri shahiri kabisa kutounga mkono jitihada hizi za mataifa ya Afrika.

Baadhi ya viongozi wa Afrika kwa uchu wa fedha za kibeberu wakaanza kuingia mkenge huku wakionesha kwao hali kuwa mbaya ili tu wapewe fedha za misaada na mikopo.

Cha kusikitisha, kama ungefanyika ukaguzi sasa utagundua kwamba fedha zile walizopewa ziliishia kwenye mifuko ya walio wachache. Kwa kupokea fedha zile wakalazimika kutoa taarifa wakati mwingine zisizo sahihi ili kuyafurahisha mataifa ya kibeberu.

Furaha yangu ni kwamba msimamo wa mwanamajumui wa Tanzania ulikuwa thabiti huku akiungwa mkono na wanamajumui wenzake katika kuliongoza taifa akiwepo Mama Samia na Majaliwa.

Kitendo cha baadhi ya watendaji kutumiwa na mataifa ya ubeberu katika kutoa taarifa feki za wagonjwa kikamuamsha Mzee Magufuli na kupeleka sampo za papai n.k. na kukomesha uozo huo.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa enzi za umajumui wa Afrika na usaliti ndani mwake, hadi sasa Rais Magufuli anaonekana kubaki peke yake katika kuonyesha msimamo imara wa watanzania juu ya kupigania kile tunachokiamini na kulinda maslahi na uchumi wetu.

Pengine, anayeonyesha kumuelewa kwa sasa ni Rais Museven wa Uganda kwa kuwa naye anayo kiu bado ya muungano wa bara la Afrika.

Kama kuna kipindi waafrika tulipaswa kuungana na kuwa na kauli moja dhidi ya mabeberu, ni kipindi hiki cha COVID-19. Wakati mabeberu bado wamefunga mipaka na kujifungia, sisi tungeungana na kuendeleza kuimarisha chumi zetu kupitia biashara za sisi kwa sisi.

Hata hivyo, kwa ubinafsi na mambo kadha wa kadha baadhi ya mataifa ya Afrika yanaungana na mabeberu katika kuendeleza vita ya kiuchumi.

Juzi Kenya imetangaza kwamba mahindi yanayotoka Tanzania na Uganda yana sumu na hivyo hayafai kwa matumizi ya chakula nchini mwao. Lakini cha kusikitisha ni kwamba tangu enzi na enzi mataifa haya yamekuwa yakifanya biashara hii baina yao pasipokuwa na shida yoyote.

Kimsingi, siyo mara ya kwanza taifa hilo kutaka kusitisha uhusiano wa kibiashara baina yake na Tanzania hasa kwenye kipindi hiki cha covid-19.

Kwa hali inavyokwenda inaonyesha kwamba COVID-19 ni njama moja wapo katika kuimarisha vita ya kiuchumi baina ya mabeberu sawa na alivyokuwa akieleza Rais Magufui katika nyakati tofauti; kama waafrika huu siyo wakati wa kutengana na kuumana sisi kwa sisi bali ni wakati wa kuungana na kupambana dhidi ya mabeberu hawa tukirejea kwenye asili yetu.

Swali lingine la kujiuliza; ni lazima kutumia chanjo za kibeberu? Kwa nini angalau katika kipindi hiki tusingeungana na kumuonyesha mbeberu kwamba hatumhitaji katika hili na kwamba tunaweza kupambana wenyewe bila yeye?

Nimalizie kwa maneno aliyoyasema Patrice Lumumba mnamo tarehe 22 Machi, 1959 katika Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria; kwamba “Afrika tuamke! Afrika tuungane! Afrika twende mkono kwa mkono katika kulifanya bara letu huru na lenye haki”.

Pasipo kufanya hivyo kama waafrika tutakuwa tumewasaliti waliopigania uhuru wetu na haitakuwa haki kwao na vizazi vijavyo. Inatosha sasa kushiriki kwenye vita ya mabeberu ambayo tunajiumiza wenyewe kwa kuwaruhusu watuendeshe na kutupangia namna ya kuishi.

Mungu Ibariki Afrika.

: +255 712 246 001; HYPERLINK "mailto:[email protected]" [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz