Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wakiukwaji wa matumizi ya Silaha wafichuliwe

19dca0da7a14672a725b042a4541e038.jpeg Taarifa kwa watumiaji wa silaha

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HIVI karibuni mkoani Dar es Salaam, mtu mmoja aliripotiwa kujiua kwa kujipiga risasi akiwa katika baada moja eneo la Sinza.

Kabla ya kujiua, mtu huyo anadaiwa kutishia kuua watu na kisha, kwa kutumia bastola, akamuua mwenzake kwa kumpiga risasi tatu katika paja, kichwa na tumboni.

Juzi Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saam, Jumanne Muliro aliuambia umma kuwa, polisi wanawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kutishia watu kwa bastola wanazozimiliki kihalali.

Kwamba, Isack Wile akiwa katika baa iitwayo 99 Vibes iliyopo Sinza, anadaiwa kutoa bastola aina ya Browning na kuanza kutishia watu huku akiwa amelewa.

Mtuhumiwa mwingine, Rashid Mshana alionekana kwenye video fupi katika mitandao ya kijamii akitishia kwa bastola aina ya ‘Browning.’

Kwamba, polisi walifanya upelelezi na kumkamata akiwa na bastola yenye namba AP 06929TZCAR 113729 ikiwa na risasi 10.

Silaha hiyo inamilikwa na kaka yake anayefahamika kwa jina la Mussa Mshana anayetuhumiwa kwa kosa la uzembe wa kumwachia silaha mdogo wake aliyejirekodi akitishia watu kwa silaha na kutuma ‘clip’ kwenye mitandao ya kijamii.

Mtuhumiwa mwingine aitwaye Ibrahim Shaibu kwa mujibu wa Kamanda Muliro, anadaiwa kutishia kumuua kwa silaha jirani yake wakati wakigombania mipaka ya kiwanja huko Vijibweni Kigamboni.

Mtuhumiwa huyo anayemiliki silaha hiyo kihalali, alikamatwa akiwa na bastola yenye risasi sita.

Miliro alisema watuhumiwa wote silaha zao zinashikiliwa na Jeshi la Polisi na taratibu za kisheria zitafuatwa ikiwamo kuwafutia umiliki wa silaha hizo.

Kwetu sisi, hali hii inaonesha kuwa, baadhi ya watu wanataka kujaribu kurudisha enzi za ‘mwaka 47’ ambapo baadhi ya watu walitaka kujigeuza kuwa miungu katika jamii kwa kutaka kumiliki usalama na maisha ya watu.

Hao walikuwa wakitishia kuwaua wenzao na wengine kutekeleza mauaji kwa sababu tu, wanamiliki silaha na kwamba, wanaweza kuwalipa fidia hata wakiwajeruhi au kuwaua.

Matukio haya yanaonesha kuwa, ‘ugonjwa’ huu umeibuka japo baadhi hawajatajwa wala kukamatwa.

Ndio maana tunasema, wananchi waanzishe utaratibu makini wa kuwafichua wamiliki wa silaha wanaozitumia vibaya ama kwa uhalifu wa ujambazi na utekaji hata kwa kukodishia wahalifu, au kwa kutishia watu katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya makazi au starehe kama baa.

Tunasema, ni vema polisi wafanye uhakiki mpya kwa wamiliki wa silaha ili kuhuisha taarifa zao kupitia vyombo vilivyotumika kuwapa umiliki wa silaha hizo.

Aidha, tunashauri mtu anapofanya uhalifu wa kutishia watu kwa silaha, jamii itoe taarifa haraka na kwa siri kwa jeshi la polisi ili atiwe mbaroni, badala ya kujaribu kumsemesha kwa kuwa anaweza kutekeleza uhalifu kadiri ulevi unavyomtuma.

Ndio tunasema: ‘Wamaotumia vibaya silaha wafichuliwe.’

Columnist: www.habarileo.co.tz