Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wakiamua wanarudi Ligi Kuu

Wakiamua Wakiamua wanarudi Ligi Kuu

Sat, 19 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wachezaji wengi msimu huu wamekosa timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo suala zima la upungufu wa timu katika Ligi Kuu.

Kitendo cha kuwa na timu 16 kwenye ligi na ushindani uliopo kumewafanya wachezaji wengi kucheza Championship na wengine kukaa kabisa mtaani.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji ambao kama wakiamua kurudi Ligi Kuu kwenye dirisha dogo au msimu ujao wanarudi mapema tu.

HASSAN KIBAILO

Beki huyu ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza upande wa kulia na kupeleka mashambulizi kwa spidi kubwa. Msimu wa juzi alikuwa Coastal Union na aliuwasha moto wa kutosha kiasi kilichowafanya Mtibwa Sugar wamsajili kwenye msimu uliopita.

Akiwa na Mtibwa Sugar (msimu uliopita) alionyesha kiwango kikubwa lakini majeraha yakamtoa kwenye reli na kumuweka nje ya uwanja mpaka mwishoni mwa msimu.

Kibailo hakumalizia kabisa ligi, msimu huu hajasaini timu yoyote ile lakini kama akiamua kurudi uwanjani baada ya kupona goti kama ni kwenye dirisha dogo au kubwa basi anaweza kuendeleza moto wake ambao alionyesha.

DAVID MWANTIKA

Umbo lake ni wazi kabisa ni beki wa kati, msimu uliopita alikuwa na kikosi cha DTB (Singida BS FC) wakati inashiriki Championship na alikuwa sehemu ya wachezaji walioipandisha timu hiyo Ligi Kuu.

Baada ya timu kupanda, uongozi uliwakata wachezaji wengi hadi wale waliokuwa kwenye kikosi cha kwanza na kusajili wapya ambao awali walikuwa kwenye Ligi Kuu. Panga hilo lilimkuta na Mwantika ambaye hadi sasa yupo mtaani akijifua mwenyewe na kusubiri kuona ataangukia wapi.

JABIR AZIZ ‘STIMA’

Kiungo huyu ni miongoni mwa wachezaji wakongwe ambao wamekuwa kwenye kiwango kikubwa kila wanapokuwa wapo uwanjani. Alitamba na timu za Simba, Azam FC, Ndanda, Ruvu Shooting na nyingine lakini msimu uliopita aliamua kukaa pembeni huku akijifua kwenye kikosi cha Friends Rangers.

Stima kama akiamua kurudi kucheza kwenye Ligi Kuu bado ana uwezo wa kuonyesha kiwango chake kwani ni miongoni mwa wachezaji wanaojituma, kujilinda na kujiheshimu.

MOHAMED RASHID ‘T BETTER’

Mshambuliaji huyu aliwahi kutamba na kikosi cha Tanzania Prisons na baadaye akaziingiza Simba na Yanga kwenye vita ya kuwania saini yake na akaamua kujiunga na Simba.

Tangu aende kwenye timu hiyo alijikuta kwenye wakati mgumu wa kukosa namba na kuamua kwenda kwa mkopo KMC, ambapo safari yakeya soka ikawa inazidi kushuka na kuangukia JKT Tanzania.

Mshambuliaji huyu msimu uliopita alitaka kusaini moja ya timu za Ligi Kuu lakini akapata ajali ambayo ilimkosesha ulaji huo.

MOHAMED FAKHI ‘SOSHA’

Aliwahi kutamba tena akiwa nahodha wa kikosi cha JKT Tanzania na kuwafanya mabosi wa Simba wamsajili ambapo alianza kwa kuendeleza moto wake.

Akiwa na Simba alicheza na mkataba wake alirejea JKT Tanzania ambapo alicheza msimu mmoja na mkataba wake ulipomalizika hakuendelea na timu hiyo.

Inadaiwa kwa sasa amejikita zaidi kwenye suala zima la biashara zake nchini Dubai lakini alikuwa anaendelea kujishughulisha na soka kwenye timu za madaraja ya chini huko kwao Zanzibar.

Fakhi kutokana na kuendelea kucheza soka lake licha ya kujihusisha na biashara, kama akiamua kurudi tena Bara na kuamua kukipiga, uwezo huo bado upo kwani eneo lake analocheza bado linaonekana kuna matatizo kwenye timu nyingi.

MIRAJ ADAM

Mchezaji huyu ni miongoni mwa mabeki wa kulia wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi hata kucheza mipira ya faulo anapokuwa uwanjani.

Aliwahi kutamba na timu za Simba, Afrika Lyon, Singida United na Coastal Union kwa nyakati tofauti na kote akionyesha kiwango kizuri.

Miraj kwa sasa hana timu yupo anajifua katika Uwanja wa Stakishari Ukonga akijiweka fiti huku akidai matatizo ya nje ya uwanja ndio yamemfanya asionekane uwanjani.

WENYEWE WAFUNGUKA

Beki Hassan Kibailo alisema sababu kubwa ambayo imemuweka nje ya uwanja ni majeraha ya goti ambayo aliyapata katika msimu uliopita.

Kibailo alisema alipata ofa kutoka timu za Ligi Kuu na Championship lakini alishindwa kujiunga nazo kwa sababu alihitaji kukaa sawa zaidi.

“Naendelea vizuri nashukuru Mungu, nadhani mtaniona uwanjani tena kwenye dirisha dogo,” alisema mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alikuwa kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar.

Wakati huohuo, beki Miraj Adam alisema upande wake yeye hana wasiwasi na suala kurudi uwanjani kwani mambo yaliyomfanya asionekane ameshayamaliza.

“Nilikuwa na matatizo ya nje ya uwanja (kifamilia) lakini nimeyamaliza, nadhani nitarudi tu kwa sababu umri wangu bado unaniruhusu. Naamini naweza kuendelea kuchezakwani wachezaji wengi nilioanza nao bado wapo uwanjani,” alisema beki huyu ambaye msimu uliopita alisaini mkataba na klabu ya DTB ikiwa Championship lakini hakucheza mchezo wowote ule na kuamua kukaa pembeni ya timu hiyo.

Columnist: Mwanaspoti