Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wahitimu ondoeni dhana ya kuajiriwa, mjiajiri

8e5dff02b23851dfc0a8c82a38155119 Wahitimu ondoeni dhana ya kuajiriwa, mjiajiri

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUTOKANA na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, yanayosababisha kundi kubwa la vijana kukosa kazi katika karne hii ya 21, ni vema vijana wakaondoa dhana ya kuajiriwa na kuwa na mawazo ya kujiajiri.

Kila mwaka wahitimu wengi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, wamekuwa wakihitimu, lakini wengi wao hubaki mtaani kwa kukosa kazi na wengine wamekuwa wakizunguka na bahasha za kaki kutafuta ajira bila mafanikio.

Kutokana na kutokuwepo kwa ajira hizo, ni vema vijana wakajiandaa kisaikolojia kuwa wapo tayari kufanya kazi katika mazingira yoyote ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

Hali ya kukosa ajira kwa wahitimu hao, imewafanya baadhi yao kukata tamaa huku wengine wakiwa wamejiingiza kwenye ujasiriamali ikiwemo kilimo, mitumba na biashara nyingine ndogo.

Hakuna ubishi kuwa serikali, walimu na wazazi wamejitahidi kwa sehemu yao kuhakikisha inamtoa mhitimu huyo ujinga, kwa kumpatia elimu bora itakayomwezesha kujitegemea ikiwa ni pamoja na kujumuika katika jamii kutafuta maendeleo ambayo yatachangia mabadiliko nchini na duniani.

Hivyo kutokana na kutokuwa na ajira, vijana waliohitimu wanatakiwa kutumia elimu waliyoipata, kama ushawishi kwa watu wote ili wawe chachu ya mabadiliko katika jamii.

Pia wakumbuke kuwa elimu waliyoipata ni mali ya umma, na pia kwamba elimu na maarifa haiwezi kuwa chachu ya mabadiliko yaliyokusudiwa, kama haitatumika katika kutatua matatizo ya jamii.

Ni imani kuwa kila mmoja wa wahitimu hao, ana jambo la kufanya katika kubadilisha maisha ya jamii inayomzunguka, taifa la Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.

Kutokana na kutokuwa na ajira, hakuna sababu kwa wahitimu hao kusubiri kuajiriwa na serikali, bali wawe wepesi kutumia vichwa vyao kufikiri jinsi ya kujikomboa na ukosefu wa ajira.

Ikumbukwe kuwa miaka ya nyuma, wahitimu walikuwa na nafasi kubwa ya kuajiriwa mara tu baada ya kumaliza masomo yao, kwani kazi zilikuwa zinawasubiri na pia walikuwa na uhuru wa kuzichagua.

Lakini kutokana na mazingira yaliyopo, wahitimu wanapaswa kuwa wepesi kuangalia ni wapi ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi, hata kama itakuwa ni kufanya kazi za kujitolea.

Kwa kufanya hivyo, watajenga kujiamini, ujuzi na mchango wao utatambuliwa na kuinufaisha jamii.

Wahitimu hao pia wanapaswa kujua kuwa wanaingia katika ulimwengu, unaobadilisha haraka mno, hivyo nao wanapaswa kuwa wepesi wa kujifunza mambo mapya na kubadilika kwa haraka ili wasiachwe nyuma na wakati.

Kwa hali ilivyo katika ulimwengu wa leo, wahitimu wanapaswa kuwa ni watu wa kutafuta fursa badala ya kuzisubiri ziwafuate, jambo ambalo si rahisi kutokea katika ulimwengu wa leo.

Ukweli ni kwamba kwa kutekeleza wajibu wao wa kujitafutia maisha mazuri na kuendeleza nchi, ni vema kuwa na hulka ya kuthubutu kujaribu mambo ambayo yanaonekana ni magumu.

Lakini hata ikitokea wakashindwa kufanikisha yale waliyoyatarajia, hawapaswi kufa moyo, bali kuendelea kuwa na ari ya kujaribu tena na tena hadi mafanikio yapatikane.

Wakati umefika kwa shule na vyuo mbalimbali, kutoa elimu itakayomkomboa mwanafunzi punde anapomaliza kwa ajili ya manufaa yake na taifa kwa ujumla.

Na kupitia elimu hiyo mwanafunzi aweze kuelimika kwa kujaribu kubuni mawazo chanya yatakayomwezesha kupata fedha ya kuendesha maisha yake.

Shime wahitimu muondokane na dhana ya kuajiriwa katika karne hii, bali muwe na fikra za kuwatoa hapo mlipo na kuwapeleka hatua nyingine zaidi ya kimaendeleo.

Columnist: habarileo.co.tz